|
Mpango huu wa HABITAT hakika utawakomboa wanawake wengi
2007-04-22 10:57:24
Na Mhariri
Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (HABITAT), kwa kushirkiana na benki ya Azania ya hapa nchini, zimeingia mkataba ambao unaweza kuwa mkombozi mkubwa kwa wanawake hapa nchini.
Mkataba huo unalenga kuiwezesha benki hiyo kutoa mikopo ya ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu kwa wanawake wa hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa HABITAT ambaye ni Mtanzania, Profesa Anna Tibaijuka, anasema lengo la mpango huo ni kuijengea uwezo benki hiyo wa kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wanawake kwa ajili ya kujenga nyumba hizo.
Profesa Tibaijuka alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa Baraza Kuu la shirika hilo Jijini Nairobi, Kenya.
Alisema hata hivyo, ufanisi wa zoezi hilo unaweza kupatikana iwapo sekta zinazohusiana na maendeleo ya makazi ya watu zitatoa ushirikiano kwa shirika hilo.
Kwanza kabisa tunapenda kulipongeza shirika hilo la HABITAT na Benki ya Azania kwa kuingia mkataba huo ambao tunaamini utakuwa faraja kubwa kwa wanawake hapa nchini. Ni kundi ambalo limekuwa nyuma kwa miaka mingi, lakini hivi sasa liko mstari wa mbele katika kujiletea maendeleo kwa jumla.
Ni ukweli usiopingika kwamba katika miaka ya karibuni wanawake wamekuwa ndio wajasiriamali wakubwa hapa nchini, wakitoa upinzani mkali kwa wanaume ambao walikuwa wamehodhi shughuli za maendeleo ya kiuchumi kwa muda mrefu.
Hivi sasa wanawake wengi wanashiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama biashara, kilimo, ajira na nyinginezo.
Tunafarijika kwamba shirika la HABITAT limeona mageuzi hayo miongoni mwa wanawake kiasi cha kuamini kwamba wanaweza kukopesheka katika mpango huu wa ujenzi wa nyumba.
Ni dhahiri kama mpango huu utafanikiwa, wanawake wengi watakuwa wanamiliki nyumba zao wenyewe na hivyo kuchochea zaidi wenzao wengine kujiingiza katika shughuli za maendeleo ili nao waweze baadaye kupata mikopo hiyo.
Hata hivyo, tunaishauri benki iliyopewa jukumu hilo kuwa makini na kazi hiyo ili malengo yaliyokusudiwa na shirika la HABITAT yaweze kufanikiwa.
Hiyo ikimaanisha haitarajiwi uwepo usumbufu katika upatikanaji wa mikopo hiyo. Wanawake watakaoomba baada ya kukamilisha taratibu zote za mikopo hiyo, ni bora wapewe haraka ili kujenga imani kwa wananchi, hususan wanawake, kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa.
Aidha, tunatoa wito kwa wanawake kuchangamkia mikopo hiyo ya HABITAT mara tu itakapoanza kutolewa. Wale wanaoona wana uwezo wa kukopa, wafanye hivyo, kwani hiyo ni moja ya njia za kujiletea maendeleo.
|