|
Kauli za `njoo kesho` bado zimeshamiri ofisi za serikali
2007-04-23 10:06:24
Na NELSON GOIMA
Sekta ya utumishi wa umma nchini inakabiliwa na matatizo makubwa mawili; ambayo ni rushwa na kauli za `njoo kesho`.
“Tumeanza safari. Safari ya kuelekea kwenye mageuzi. Utumishi uliotukuka ni nyenzo muhimu ya kufikia azma yetu hiyo.
Utumishi huo ndiyo utakaoifanya serikali ifanikiwe kuendesha sekta nyingine zote muhimu,“ alisema aliyekuwa Katibu Mkuu katika ofisi hiyo, Bw. Joseph Rugumyamheto.
Alisema hayo mapema mwaka huu, wakati wa sherehe za kumuaga, zilizofanyika katika viwanja vya Leaders Club, Jijini Dar es Salaam.
Sherehe hizo ziliandaliwa na watumishi wenzake wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Rugumyamheto ambaye jina linalotokana na maneno mawili ya kwao, yaani “Rugumya“ ambalo maana yake mpiganaji na “mheto“ ambalo maana yake upinde, alikuwa Katibu Mkuu kwa miaka 11.
Aliajiriwa kwa mara ya kwanza serikalini Machi 17, 1971, mara tu baada ya kuhitimu masomo yake ya Chuo Kikuu.
Aliajiriwa kwa cheo cha Afisa Mipango ya Utumishi na baadaye kupanda ngazi mbalimbali, hadi kuwa Katibu Mkuu .
Siku hiyo Rugumyamheto, alikabidhiwa zawadi mbalimbali na katika hotuba yake alisema“ Safari ya kuleta maendeleo ni ndefu. Hali kadhalika safari ya kufikia utumishi uliotukuka serikalini ni ndefu. Safari bado ni ndefu. Inahitaji ujasiri mkubwa.“
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Hawa Ghasia, amekuwa akizunguka mikoa mbalimbali nchini kuelezea “safari hiyo” ya kuboresha utumishi wa umma.
Huko mikoani Bi. Ghasia amekuwa akikagua utendaji wa kazi za serikali na kuzungumza na watumishi.
Anasema katika ziara zake hizo, amebaini kuwa wananchi bado wanakabiliwa kero nyingi, wanapokwenda kutafuta huduma katika ofisi za serikali.
Lakini, kuna matatizo makubwa mawili, ambayo waziri huyo amekuwa akiyataja kila anakokwenda; nayo ni ulaji rushwa na urasimu, uliojaa kauli za `njoo kesho`.
“Pamoja na mafanikio tuliyoyapata katika mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, bado utumishi wa umma una changamoto kubwa mbele yake. Upatikanaji wa huduma katika baadhi ya maeneo ya utumishi wa umma, bado hauridhishi.
Bado huduma hazitolewi kwa kuzingatia muda. Lugha ya `njoo kesho` bado ipo; na hata ukiuliza baadhi ya wananchi, watakuambia kwamba bado wanaombwa kutoa kitu chochote, ili kupata huduma ambayo kimsingi ni haki yao kama walipa kodi,” anasema Bi. Ghasia
Kimsingi, baadhi ya matatizo hayo yanatokana na kutotimiza wajibu pamoja na kukosekana kwa mawasiliano sahihi, kati ya watoa huduma (watumishi) na wapokea huduma(wananchi).
Watumishi wa umma wanatakiwa kupambana na kero zote, zinazokabili utumishi wa umma.
Inatakiwa watumishi wa
serikali wawe na ari, moyo na msimamo wa dhati katika kutoa huduma bora kwa wananchi. Lazima wabadilike ili kutekeleza majukumu yao.
Jambo lingine ambalo Waziri Ghasia amekuwa akilielezea ni mikataba ya huduma kwa mteja. Mikataba hiyo ya huduma kwa mteja, imeanzishwa na serikali chini ya Programu ya Kuboresha Utumishi wa Umma.
Imeanzishwa kwa kila wizara, idara zinazojitegemea, wakala wa serikali na halmashauri. Kwa sasa sehemu kubwa ya asasi za serikali, tayari zina mikataba ya huduma kwa mteja.
“Lengo kuu la mikataba hii ni kuweka viwango maalum vya muda kwa asasi za serikali kutoa huduma kwa wananchi.
Kuwepo kwa muda maalum wa kutoa huduma, kutaondoa ubabaishaji, `njoo kesho` na hata kupunguza ukubwa wa tatizo la rushwa,” anaeleza Bi Ghasia.
Hata hivyo, Waziri Ghasia anasema mikataba mingi haijulikani kama ipo. Wahusika wakuu wa mikataba hiyo hawaijui. Hata muda wa utoaji wa huduma ulioahidiwa na asasi husika na hata watumishi wa asasi yenyewe, hawaielewi na kuitumia mikataba hiyo.
Kinachotakiwa ni kwa wizara zote, idara zinazojitegemea, wakala na halmashauri, ambazo mikataba yao ya huduma kwa mteja ipo tayari, waandae mikakati ya kuitangaza kwa wadau wao mara moja.
Mabadililo yanayoendelea katika Sekta ya Utumishi wa Umma, yanalenga kuleta mchango thabiti katika maendeleo ya nchi.
Sekta binafsi, mashirika ya dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, wahisani na wananchi, wakipata huduma bora, watachangia sana kukua kwa uchumi na kuondoa umasikini.
Ni vema kufanya kazi kwa kuweka mbele maslahi ya taifa, badala ya maslahi binafsi.
Watumishi wanapaswa kuelewa kuwa maendeleo ya Taifa ya sasa na miaka ijayo, yataletwa na watumishi wa sasa.
Utumishi wa umma kwa maana ya mifumo, sheria, taratibu, sera na kanuni, hauwezi kufanya kazi yake bila kuwa na watumishi wenye sifa za hali ya juu, waadilifu na wenye kuheshimu na kutumia mifumo, taratibu na sheria zilizowekwa ili kutekeleza majukumu yao.
Bi. Ghasia anasema ni muhimu sera, sheria, kanuni na taratibu zote zilizoandaliwa na serikali, kama sehemu ya kuboresha utendaji wake, zikawafikia na zikaeleweka kwa waajiri na watumishi wote katika utumishi wa umma, yaani wizara, idara zinazojitegemea, mikoa, wilaya na taasisi za umma.
Nyaraka hizo ni sehemu ya mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa masuala ya kiutumishi na utawala, yanayofanywa na serikali.
Nyaraka hizo zina maeneo yafuatayo:Taratibu za ajira, kupandishwa vyeo, mabadiliko mbalimbali katika utumishi wa umma, upimaji na utendaji kazi, mafunzo na malipo ya mishahara.
“Katika safari zangu za mikoani ambazo nimefanya kuhamasisha utendaji kazi kwa watendaji mbalimbali, kilio cha watumishi wengi na baadhi ya wakuu wa maeneo ni kutokujua nini kinafanywa au kuamuliwa na serikali kuhusu wao au majukumu yao, kwa sababu hawapatiwi nyaraka na taarifa yoyote ile inayowahusu,“ anaeleza Waziri huyo wa Utumishi.
|