23 Apr 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Hoja ya vyeti bandia si ya kupuuza
 
2007-04-23 10:07:24
Na Mhariri

Hivi karibuni, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe alielezea wasiwasi wake kwa Tanzania kuweza kuachwa nyuma miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki iwapo haitatafuta dawa ya kudhibiti ongezeko kubwa la watu wanaotumia vyeti bandia ili kufanikisha malengo yao mbalimbali.

Mbunge huyo aliyasema hayo mbele ya kikao cha Bunge la Jamhuri mjini Dodoma wakati akichangia mjadala wa Taarifa za Kazi za Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje 2006 na Kamati ya katiba, Sheria na Utawala mwaka huohuo.

Inatulazimu kuliandikia suala hili kwa vile kwa muda mrefu matumizi ya vyeti bandia yamekuwa ni donda ndugu nchini mwetu.

Zipo taarifa kwamba hapo nyuma majeshini (JWTZ, Polisi na Magereza) hali ilikuwa mbaya zaidi, lakini tunashukuru kusikia kwamba siku hizi wahusika wanajitahidi kufuatilia vyeti vya vijana wanaoomba kazi za kijeshi.

Baadaye tatizo la matumizi ya vyeti bandia lilianza
kujitokeza kwa wanafunzi waliotaka kujiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu. Wapo waliofanikiwa kusoma kwa mtindo huo na kuwazibia nafasi wale wenye sifa sahihi.

Lakini siku zilivyozidi kwenda hata viongozi walio kwenye ngazi za juu kama mameneja, wakurugenzi na hata baadhi ya wabunge wamekuwa wakituhumiwa kushika nyadhifa zao hizo kwa kutumia vyeti bandia!

Rais Jakaya Kikwete mwaka jana wakati alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini alipata kuulizwa kwamba ni hatua gani serikali imepanga kuwachukulia wabunge ambao watabainika kuwa walipata Ubunge kutokana na taarifa za uongo, hususan wasifu wao kielimu.

Rais alijibu kwamba Bunge lina taratibu zake ambazo zinaweza kufuatwa iwapo baadhi ya wabunge watagundulika kudanganya kuhusiana na wasifu wao.

Wasiwasi wetu ni jinsi udanganyifu huu unavyoweza kuzigusa hata taasisi nyeti kama za tiba ambapo ni hatari sana kuwa na daktari ambaye ni `kihiyo` kwa sababu anaweza kusababisha vifo vya watu wengi.

Kuna taarifa kwamba hata vyeti vinavyotolewa na vyuo mbalimbali vilivyopo nje ya nchi, Ulaya na Marekani, navyo vinaghushiwa kirahisi na kutumika kwa ajili ya usaili katika taasisi mbalimbali hapa nchini.

Mbali na matumizi ya vyeti `feki`, zipo habari za shule au vyuo, hususan vya binafsi, kuwasaidia wanafunzi wao katika mitihani na kuonekana wamefaulu vyema.

Kuna madai kwamba vyuo au shule nyingi za binafsi zinaamini katika kufaulisha wanafunzi wengi ili kuvutia wazazi wengi kupeleka watoto wao huko, na hivyo huwa na mikakati ya kufanya udanganyifu kwenye mitihani ili watoto wengi zaidi wafaulu.

Tunadhani kwamba tatizo la vyeti feki nchini mwetu ni kubwa kutokana na sura hizo mbili na hivyo kauli ya Dk. Mwakyembe inatakiwa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa zaidi.

Pengine ni wakati mwafaka sasa watunga sera na sheria kuja na mikakati ya kudhibiti hali hii.

Vinginevyo tutakuwa na wataalamu wengi feki ambao wataturudisha nyuma kimaendelo huku wakiwa wameziba nafasi za vipaji halisi. Na kwa mantiki hiyo tutatoa picha kwa nchi za kigeni kwamba Tanzania ni nchi ya watalaamu feki.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.