|
PATA:Uharamia wa vitabu sawa na wizi mwingine
2007-04-24 09:36:34
Na JACKSON KALINDIMYA
Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA) kina mkakati maalum wa kukabiliana kikamilifu na uharamia wa vitabu kwa kuwaelimisha watekelezaji wa sheria na kuuelimisha umma ili ushiriki kikamilifu katika vita hivyo muhimu.
SWALI:Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA), hivi karibuni kilifanya mkutano wake mkuu. Je, ni mambo gani hasa yaliyojitokeza au kuamuliwa katika mkutano huo?
JIBU:Miongoni mwa ajenda za mkutano huo, ni kuchagua viongozi wapya wa Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA), baada ya viongozi waliokuwepo madarakani katika kipindi cha miaka sita kumaliza muda wao. Uongozi uliomaliza muda wake ni aliyekuwa mwenyekiti wetu Bw. Khalaf Rashid wa Macmillan Aidan.
Viongozi wapya waliochaguliwa Mwenyekiti ni Bw. Elibariki Moshi wa Mture Educational Publishers na makamu wake ni Bibi Anitha Rwehumbiza wa Longman Tanzania Ltd.
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na kampuni zao kwenye mabano, Bw. Walter Bgoya (Mkuki na Nyota Publishers), Bw. Lipangala T.Minzi (Dar es salaam University Press), Bw. Abdullah Saiwaad (Readit Books Ltd), Bibi Neema Jones (Longhorn Tanzania Publishers) na Bw. Khalaf Rashid (MacMillan Aidan Ltd).
SWALI:Ajenda gani nyingine iliyojadiliwa katika mkutano huo?
JIBU:Agenda nyingine ilikuwa ni mpango wa utekelezaji wa mwaka 2007.
Mojawapo ya malengo hayo ni kutokomeza uharamia wa vitabu uliokithiri nchini, ili kuhakikishia kuwa uharamia huo unabakia kuwa suala la kihistoria tu.
Katika kuhakikisha kuwa mpango huo kamambe unafanikiwa, PATA inatarajia kukusanya michango kwa wanachama wake na kutafuta wafadhili wenye nia njema ya kutuunga mkono katika vita hivi, ili kupata angalau sh. milioni 18 za kukabiliana kikamilifu na uharamia wa vitabu nchini kwa mwaka 2007.
SWALI:Kwa muda mrefu sasa, nimekuwa nikisikia PATA ikifanya kampeni ya kudhibiti uharamia wa vitabu.
Je, kuna tofauti gani kati ya kampeni zilizopita na hii ya sasa?
JIBU:Lengo la kampeni zilizopita na hii ya sasa ni kudhibiti uharamia wa vitabu.
Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza katika kampeni hizo, ni kuwa watuhumiwa au maharamia wa vitabu walipokamatwa na kupelekwa polisi au mahakamani baadhi ya polisi, mahakimu na wadau wa sheria hawakuwa na uelewa wa kutosha kuwa uharamia wa vitabu ni wizi sawa na wizi wowote mwingine.
Kesi zilifunguliwa na baadhi walifikishwa mahakamani.
Mathalani kuna kesi moja ya mtuhumiwa wa uharamia wa vitabu iliendeshwa kwa kipindi cha miaka mitatu, lakini kwa mshangao mtuhumiwa aliachiwa huru, licha ya kuwa ulikuwepo ushahidi madhubuti wa kumtia hatiani.
Kwa hiyo mkakati wa sasa tutawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali , Kamanda wa Polisi nchini (IGP) na uhamiaji ili tupatiwe polisi na mahakimu, ambao watapigwa msasa wa kuielewa vyema sheria ya Copyright and Neighbouring rights ya mwaka 1999.
Watu wa uhamiaji tumeamua kuwashirikisha wapigwe msasa huo, kwa sababu kuna baadhi ya vitabu vinafanyiwa uharamia toka nje na kuingizwa nchini.
Utekelezaji wa sheria hiyo, umekuwa mgumu kwa sababu hawana uelewa au mwamko wa kutosha kuhusu sheria hiyo hata kuitumia.
Mpango huo wa kuwapa semina, tunatarajia kuanzia katika mikoa miwili ya Dar es salaam na Mwanza.
Tunaamini kuwa, baada ya kuwapiga msasa huo, mtu akikamatwa na ushahidi unaojitosheleza, sheria ichukue mkondo wake.
Hatua ya pili, ni kuuelimisha umma kutambua tunapozungumzia uharamia wa vitabu maana yake ni nini.
Tofauti kati ya vitabu vilivyofanyiwa uharamia na vile ambavyo hajifanyiwa.
Tahadhari gani wachukue na ikitokea wamekutana na mtu anayefanya uharamia wachukue hatua gani.
Kuuelimisha umma, tutashirikiana na vyombo mbalimbali vya habari, tutabandika mabango na matangazo ya aina mbalimbali yanayolenga kuufikishia umma taarifa hiyo muhimu.
SWALI:Kufanikiwa kwa jambo lolote lile kuna gharama zake. Je, nani hasa atabeba gharama hizo za kufanikisha kampeni hiyo?
JIBU: Wanachama wetu, yaani wachapishaji wameamua kujitolea kujaribu kubeba gharama hizo.Hii ni kutokana na ukweli kuwa, ni wao ndio wamekuwa wakiathiriwa sana na maharamia hao.
Wanatumia gharama na muda wao mwingi kutayarisha na kuchapisha vitabu, lakini wanajikuta hawawezi kuuza kwa sababu masoko yanakuwa yamefurika vitabu.
Wanaona kuwa, ni vyema wakaingia gharama ya kuchangia kampeni hii, kuliko kuiacha hali kama ilivyo, kisha wakapata hasara kwa muda mrefu katika biashara zao.
Halikadhalika, tutaomba ufadhili kwa mashirika mbalimbali yakiwemo World Intellectual Property Organisation (WIPO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) ili yachangie kuimarisha juhudi hizo.
SWALI:Kumekuwa na madai kuwa baadhi ya wachapishaji wanashiriki kufanya uharamia wa vitabu.Unazungumziaje tuhuma hizo?
JIBU:Inasikika hivyo, lakini hakuna ushshidi wa kukamatwa kwa mchapishaji hata mmoja. Tuhuma nyingi zinaelekezwa kwa baadhi ya wauza vitabu na baadhi ya wachapaji, ambao wamekuwa wakivirudufu vitabu bila ya idhini ya mchapishaji.
Wanaandaa vitabu kwa kuzingatia teknolojia ya sasa, baadhi ya vitabu vinafanana sana na vitabu halisi.Kwa hiyo, ni vyema sana wananchi wakaelimishwa ili waweze kuichukua tahadhari.
SWALI:Unazungumziaje kuhusu hali ya mshikamano ndani ya chama chenu na pengine wadau wa sekta ya vitabu?
JIBU:Tumekubaliana kwamba tujenge mshikamano wa dhati ndani ya chama chetu. Pia watendaji wakuu wa sekta mbalimbali za vitabu kama vile wauza vitabu, waandishi wa vitabu, wakutubi, wachapaji na wengineo wawe wanakutana mara kwa mara ili kuzungumzia masuala ya kitaalamu, kuhusu maendeleo ya sekta ya vitabu.
Tunaamini kuwa, hali hii itaongeza mshikamano na mahusiano mazuri kwa wadau wa sekta ya vitabu.
Dhamira hasa ni kuwa na mshikamano, mtazamo mmoja na mwelekeo mmoja.
SWALI: Kampeni za uharamia wa vitabu zimekuwa zikifanywa sana na PATA. Je, serikali ina mtazamo gani kuhusu hali hiyo?
JIBU:Tunaishukuru serikali inatambua na kuunga mkono juhudi zetu. Sasa imekuwa ikitoa matangazo kuufahamisha uuma kuhusu madhara ya kununua vitabu vilivyofanyiwa uharamia.
Serikali kwa sasa, inatambua uwepo wa PATA ikiwa pamoja na katika ofisi za serikali. Katika Kamati ya Kuidhinisha vifaa vinavyotumiwa mashuleni (Education Material Committe-EMAC) sisi ni wajumbe.
Hatua hiyo imechukuliwa ili kuleta uwazi wakati wa kupitisha maamuzi ya kuamua vitabu au vifaa gani vinafaa au kukidhi viwango vya kutumiwa mashuleni.
PATA pia, ni mjumbe wa Baraza la Ushauri la Elimu (Education Advisory Board) ambalo lina jukumu la kumshauri Waziri wa Elimu na Mafunzo masuala yote yanayohusu elimu.
Tunaishukuru serikali na Wizara ya Elimu kwa ujumla kuona umuhimu wa chama chetu na kukishirikisha
SWALI: Nini mipango yenu ya baadaye?
JIBU: Kuzalisha bidhaa ambazo ni bora zaidi ili kukidhi mahitaji ya walengwa katika zama hizi ambazo teknolojia inazidi kusonga mbele.
Tutashiriki katika matamasha na maonyesho mbalimbali ya sekya ya vitabu na elimu ikiwemo World Copyright Day,Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (DITF),Tamasha la Vitabu la Taifa ambalo hufanyika mwezi Septemba wa kila mwaka.
Mkakati wetu mwingine ni kutoa mafunzo mbalimbali kwa wanachama wetu,wahariri wa vitabu na wataalamu wengineo wa fani hii.
Sisi ni wanachama wa Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania (BAMVITA) ambayo ni mwanachama wa Baraza la Maendeleo ya Vitabu la Afrika Mashariki (EADBA) ambao hunufaika kwa kupewa fursa za kuandaa mafunzo yanayolenga kuboresha uchapishaji.
Kwa sasa hapa nchini, hatuna chuo cha uchapishaji. Kwa hiyo kozi na semina zinazotolewa, zina mchango muhimu wa kuboresha sekta hii.
SWALI: Je una maoni yoyote mengine?
JIBU:Serikali iendelee kutoa ushirikiano katika kukabili na kudhibiti uharamia wa vitabu.Wananchi wanatakiwa kuunga mkono juhudi hizo.
Natoa wito kwa watumiaji wa vitabu wakiwemo walimu, wawe makini na wahakikishe kuwa, wafanyabiashara wananunua vitabu kwa kufuata utaratibu na maduka yanayoendeshwa kwa kuzingatia sheria.
|