|
Dawa bandia za malaria zidhibitiwe nchini
2007-04-24 09:37:19
Na Mhariri
Shirika la Afya Duniani (WHO) hivi karibuni lilitoa ripoti inayoonyesha kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinaathirika sana na matumizi ya dawa bandia zinazotumika kutibu ugonjwa wa homa za malaria.
Taarifa hizi zinakuja wakati idadi kubwa ya wagonjwa wanaokufa kutokana na ugonjwa wa malaria ikizidi kuongezeka siku hadi siku tena kuzidi hata watu wanaokufa kutokana na ugonjwa wa UKIMWI!
Kumekuwepo na sababu kadhaa ambazo zimekuwa zikihusishwa na kuongezeka kwa ugonjwa huu wa malaria, baadhi yake ikiwa ni uchafu wa mazingira, gharama kubwa za dawa na uelewa mdogo wa kupambana na ugonjwa huo kwa baadhi ya wananchi.
Tunafahamu kwamba serikali mara nyingi imekuwa ikiwataka wananchi kuweka mazingira yao katika hali ya usafi ili kuondoa uwezekano wa kuwepo maeneo ya mazalia ya mbu.
Hata hivyo katika baadhi ya maeneo tena hata mijini, hali ya mazingira inatisha ikiwa ni pamoja na kuzagaa kwa takataka ovyo, madimbwi ya maji na majani marefu.
Mazingira kama haya kwa hakika yanaweza kuwa sababu kubwa ya kuenea kwa ugonjwa wa malaria kwa kasi kubwa kutokana na mbu kuweza kuzaliana kwa wingi zaidi.
Lakini tukiachilia mbali hatua mbalimbali za kinga, wananchi wengi wamekuwa wakishindwa kununua dawa bora zinazoshauriwa na madaktari kutokana na dawa hizo kuuzwa kwa bei kubwa.
Hali kama hii ndiyo ambayo inaendelea kuchangia wajanja wachache kutengeneza dawa bandia za malaria ambazo badala ya kutibu huleta usugu zaidi kwa mtumiaji wa dawa hizo.
Ripoti hiyo ya WHO imesema kwamba katika nchi za Tanzania, Cambodia na Cameroun, asilimia hadi 90 ya dawa zilizochanganywa kwa ajili ya kutibu malaria ni za bandia!
WHO imesema kwamba dawa hizo ambazo huuzwa holela madukani hazina viambatanisho vyovyote vya dawa halisi mbali na kuwekwa unga wa mahindi na poda!
Shirika hilo limeendelea kufafanua kwamba linakadiria kwamba vifo 200,000 kati ya milioni moja vinavyotokana na kuugua malaria vingeweza kuzuilika kama wagonjwa wangetumia dawa zilizo sahihi.
Tunadhani kwamba pamoja na serikali kuanzisha dawa mseto kwa ajili ya kutibu malaria, kuna haja ya kufanya uchunguzi wa kina katika maduka yanayouza dawa ili kubaini kuwepo kwa dawa bandia za malaria.
Bila kufanya hivyo Tanzania itaendelea kukabiliwa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaokufa kwa ugonjwa huu ambao unaweza kudhibitiwa iwapo hatua sahihi zinachukuliwa mapema.
|