26 Apr 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Muungano: Tuangalie mbele kwa matumaini
 
2007-04-26 10:17:37
Na Hamis Mzee

Muungano wa Tanzania Bara na Visiwani leo unatimiza miaka 43. Miaka hiyo kwa umri wa mtu bila shaka ni mkubwa na kwa nchi pia si mdogo.

Katika makala haya Hamis Mzee anaelezea maendeleo ya Muungano huo na mambo mbalimbali yaliyojitokeza katika kipindi hicho na haja ya kuuboresha na kuuimarisha zaidi.

Wakati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa Rais wa Tanganyika na Mzee Abeid Amani Karume akiwa rais wa Zanzibar walipotia saini ya kuanzisha Muungano uliozaa Tanzania Aprili 26, 1964 bila shaka walifanya kitendo cha kihistoria.

Kwa mtazamo wa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, hatua ya viongozi hao ambao pamoja na kusaini hati ya muungano, walichanganya udongo wa Bara na wa Visiwani kuashiria kuanza kwa Muungano wa pande hizi mbili, ni kuimarisha mshikamano wa nchi pamoja na watu wake.

Zanzibar iliingia katika Muungano na Tanzania Bara ikiwa karibu miezi mitatu baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Leo, miaka 43 baada ya hatua hiyo ya waasisi hao wa Muungano hali ikoje? Muungano umeimarika zaidi ama umekuwa na mitikisiko na purukushani.
Ni ajabu kwamba mambo yote hayo yametokea.

Kwa watu waliozaliwa baada ya Muungano, wao hawajui kitu kingine bali wamezoea hali waliyoikuta – Tanzania moja yenye pande mbili Bara na Visiwani.

Kwa mtazamo wa watu hawa Muungano umeimarika ama unaimarika kila kukicha.
Hatua mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha kuwa hali inakuwa hivyo. Viwango vya biashara kati ya pande hizi kimekuwa ambapo watu wa pande hizi wanachangamkia biashara katika kila upande.

Kwa bara sasa ni kawaida kuwakuta Wapemba ambao bila ya Muungano wasingeonekana kwa kiwango cha sasa, wanafanyabiashara.

Kijamii mambo yamezidi kuimarika kwani ndoa za watu wa Bara na Visiwani zimezidi kuimarisha mshikamano na kujenga udugu kati ya watu wa pande hizi mbili za Muungano.

Vikwazo kama vile vya kuwataka watu wanaotoka Bara kwenda Visiwani kutumia hati za kusafiria –Pasipoti- sasa ni historia. Havipo tena.

Watu wanaweza kwenda ama kutoka Visiwani kila wanapojisikia.
Hali hii inayodhihirisha kuimarika kwa muungano haikufikiwa kirahisi.

Kumekuwepo na mitikisiko wakati mwingine mikubwa iliyotishia msingi ya Muungano.
Wakati mmoja katika miaka ya 1980 hali ya kisiasa ilichafuka visiwani ambapo ililazimika kiongozi wa juu ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar, Alhaji aboud Jumbe kung`olewa madarakani.

Alhaji Jumbe na kundi la watu waliokuwa na mawazo kama yake walikuwa wanahoji muundo wa Muungano wakidai kuwepo na serikali tatu.

Hatua hiyo ya Jumbe na wenzake ilimkera sana mmoja wa waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere ambaye wakati huo akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Mwenyekiti wa CCM alisimama kidete na kuhakikisha Jumbe na wenzake wanazimwa.
Mwalimu akiwa mtetezi mkubwa wa mfumo wa Muungano wa serikali mbili – ya Muungano na ile ya Zanzibar alionyesha dhahiri kushangazwa na madai ya Jumbe na wenzake ya kutaka serikali tatu – yaani ya Muungano, wa Bara na ya Zanzibar.
Mgogoro unafafana na huo uliibuka tena katika miaka ya 1990 ambapo kikundi kimoja cha wabunge waliojulikana kama G 55 walipokuja na mpango wao wa kudai serikali ya Tanganyika.

Suala hilo liligawa wabunge na baadhi yao kung’ang’ania kama ikishindikana basi kuwepo na serikali moja tu ya Muungano.

Mwalimu kama kawaida yake ambaye wakati huo hakuwa madarakani na wala hakuwa Mwenyekiti wa CCM, alikuja juu na suala hilo likazimwa.

Ingawa kwa kipindi kirefu suala hili la serikali tatu ama serikali ya Tanganyika limezimwa, lakini kumekuwa na kelele na madai ya kuonyesha kuwa sehemu moja ya Muungano inapunjwa na nyingine.

Wanasiasa wa Zanzibar wamekuwa mstari wa mbele katika kuonyesha kuwa sehemu yao inapunjwa katika maeneo mbalimbali.

Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa ni mgawo wa misaada kutoka nje na rasilmali kama mafuta ni masuala ya Muungano ama la?, na wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili Zanzibar na Bara.

Kwa mujibu wa taarifa za kiserikali ya Muungano, masuala ya ugawanaji wa mapato yatokanayo na misaada kutoka nje yameshughulikiwa na Tume ya Pamoja ya Fedha.
Tume hiyo tayari imekwishatoa taarifa yake kwa Serikali zote mbili. Serikali hizo zinapitia ushauri uliotolewa na kisha kupata muafaka.

Habari hizo zimeeleza kuwa licha ya kupatikana vigezo kuhusu mgao kuna mapato yanayopatikana katika Serikali ya Muungano ambayo Zanzibar nayo inapata, ingawa siyo moja kwa moja kama gharama za uendeshaji wa mambo ya Muungano, kwa mfano balozi za Tanzania, Jeshi, polisi na kadhalika.

Sehemu kubwa ya kugharimia mambo hayo inatoka katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Hata mapato kutoka katika madini yanatumika kuendesha serikali ya Muungano, katika kugharimia Ulinzi na Usalama (Jeshi na Polisi) na Mambo ya Nje na balozi za Tanzania nje.

Kuhusu mafuta na gesi habari hizo za kiserikali zinasema kuwa haya ni moja ya``mambo ya muungano` ambayo ni nyongeza iliyo katika katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Kumekuwa na maneno hasa kutoka Zanzibar kuwa kama mafuta ni suala la Muungano, basi madini nayo (ambayo upande wa Bara umejaaliwa nalo liwe suala la muungano.

Lakini kama inatakiwa iwe hivyo, lazima jambo hilo liongezwe kwenye mambo ya Muungano. Na hii itahitaji mabadiliko katika katiba.

Hata hivyo, kwa vile kuna dalili za kupatikana mafuta Zanzibar na hata upande wa Bara, serikali hizi ( ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar) zimekubaliana atafutwe mtaalamu mwelekezi atakayeshauri juu ya utaratibu bora wa kugawana mapato yatakayotokana na mafuta kwa manufaa ya pande zote mbili, bila ya kujali yako wapi.

Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano, Dk. Hussein Mwinyi akielezea suala hili la mgao wa mafuta katika kipindi kimoja cha televisheni hivi karibuni alisema hivi sasa serikali inaangalia uzoefu wa nchi zingine zenye muungano kama vile Uingereza ambapo mafuta yanapatikana Scotland na Canada ambapo mafuta yanapatikana jimbo la Quebec la nchi hiyo.

Kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kuwa wanatozwa kodi mbili wanapoleta bidhaa Tanzania Bara baada ya kuwa wamelipa Zanzibar,suala hili kulingana na habari hizo za kiserikali limetatuliwa kwa kuwekwa utaratibu ambao unahakikisha kuwa endapo mfanyabiashara atalipa kodi kikamilifu Zanzibar, hatatozwa tena Bara.

Katika jitihada za kuimarisha Muungano na kuondoa kero, viongozi wakuu wa serikali za pande hizi mbili yaani Waziri mkuu kwa upande wa serikali ya muungano na Waziri Kiongozi wa Zanzibar wameelekezwa kukutana mara kwa mara na kushughulikia masuala ya muungano.

Licha ya hatua hiyo, serikali ya awamu ya nne imeteua waziri maalum Dk. Mwinyi kushughulikia masuala ya Muungano.

Mpasuko wa kisiasa huko Visiwani ambapo baadhi ya watu wanapenda chama kimoja tu na wengine chama kingine hali inayojenga chuki na uadui siyo kisiasa tu bali hata kijamii, umevaliwa njuga na serikali ya Muungano imelivalia kwani inahofu likiachwa kuendelea bila shaka linaweza kuleta athari kubwa kwa Muungano.

Kwa upande wa vyama, Makatibu Wakuu wa CCM na CUF wanaendelea na mazungumzo ya kuondoa mpasuko huo ambao unashangaza kuwa licha ya jitihada kubwa zinazofanywa kupunguza uhasama, kati ya vyama hivyo unaibuka kwa nguvu wakati katika uchaguzi. Pamoja na kuwa Wapemba, kwa mfano, wanawekeza na kuishi Tanzania Bara bila bugudha na hata kufanya shughuli zao vizuri Unguja, lakini kuna maneno kuwa wanabaguliwa na kunyanyaswa na wakati wa uchaguzi ni Pemba tu ambako CCM inakataliwa karibu kwa kiasi kikubwa katika namna ambayo haiko katika sehemu nyingine yoyote katika Jamhuri ya Muungano.

Bila ya shaka inahofiwa,wanasiasa wa CUF Pemba wanawachochea wafuasi wao kuichukia CCM kiasi hicho na hii ni moja ya sababu za huo mpasuko!

Hali hii inatupeleka katika suala la Upemba na Uunguja ambapo ingawa kwa mtazamo wa kiserikali Wapemba na Waunguja wote ni raia wa Jamhuri ya Muungano, inahofiwa kuwa chuki za kisiasa, ndiyo zinaleta ``Upemba na Uunguja``.

Mmoja wa waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere aliwahi kuonya wakati mmoja kuwa ubaguzi wa aina hiyo ni wa hatari kwa kuwa hapatarajiwi kuwe na tofauti ya Wapemba na Waunguja, kwa sababu wote ni Wazanzibari na wote ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.

Endapo ubaguzi wa aina hiyo utaendelea kukua, basi utagundua hata Wapemba wataendelea kubaguana kwa koo na asili na hatimaye ubaguzi utakuwa kati ya Wapemba wenye asili ya Kiarabu na wenye asili ya Kiafrika (Kibantu).

Hali kama hii inaweza kutokea Unguja pia na hata kwa Bara, sumu ya ubaguzi ikikua utakuta Watanzania Bara nao hawako sawa; kuna Wabantu na wasio Wabantu na hata hao Wabantu wenyewe pia utakuta kuna Wazaramo na/au Wachaga!

Wakati huu ambapo harakati zinapamba moto kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki, linaibuka suala kuhusu nafasi ya Zanzibar ama Jamhuri ya Muungano kwa pamoja katika Shirikisho la Afrika Mashariki litakalokuwepo?

Ni wazi kwamba endapo Shirikisho la Afrika Mashariki litaundwa, Tanzania itaingia kama Tanzania ( Jamhuri ya Juungano wa Tanzania) na siyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Hili kwa mujibu wa habari za kiserikali litakuwa Shirikisho la Nchi na siyo la Serikali.
Tanzania inaingia kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hata katika Jumuiya za Kikanda. Inategemewa kuwa itakuwa hivyo katika Shirikisho la Afrika Mashariki kwa sababu ``mamlaka ya nchi:`` (sovereignty) ya ile iliyokuwa Tanganyika na ya Zanzibar ilimalizika Aprili 26, 1964 baada ya Muungano.

Katika kuangalia, ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki – Wizara husika za pande mbili ziliagizwa kuunda kamati ambayo pamoja na mambo mengine itabainisha miradi ya maaendeleo ambayo nchi itanufaika kutokana na kuwa mwanachama wa Jumuiya hiyo ili pande zote za Muungano zinufaike. Miradi hiyo ni pamoja na ya bandari; viwanja vya ndege na nishati.

Leo wakati tunaadhimisha miaka 43 ya Muungano, ni wakati muafaka wa kuangalia mbele kwa matumaini.

Ni wazi juhudi zaidi zinahitajika kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuendelea na kudumisha Muungano kwani hii ni kama safari ndefu ambayo bila shaka haiwezi kukosa vizingiti na majaribu.

Ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa kuweka mbele maslahi ya nchi na ya wananchi na kuhamasisha kupatikana mafanikio zaidi na kuboresha Muungano.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.