27 Apr 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mkazo uwekwe uendelezaji nishati mbadala
 
2007-04-27 09:04:44
Na Felix Andrew

Tanzania ina vyanzo vingi sana vya nishati. Hata hivyo, bado havijatumika ipasavyo matokeo yake nchi yaendelea kukabiliwa na matatizo mbali mbali yanayohusiana na nishati.

Miongoni mwa nishati ambazo nchi imejaliwa kuwa nazo ni maji, makaa ya mawe, gesi asilia na nishati zinazotokana na majani.

Hata hivyo, wingi huo wa nishati haujafanikiwa kuifaidisha nchi kwa kiasi kikubwa.Umeme wake umekuwa sio wa kuaminika sana ambapo yawezekana ni watu wachache sana wanaoendelea kufaidika na mazingira hayo.

Kupanda bei kwa nishati ya mafuta ya mitambo maana yake ni kupandisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu matokeo yake kutumiwa na watu wachache hivyo kurudisha nyuma ukuaji wa uchumi.

Inakadiriwa kuwa ni asilimia kumi tu ya watanzania ndio wanaonufaika na nishati ya umeme unaozalishwa kutokana na maji.

Serikali kwa upande wake, imeelekeza nguvu zake katika utafiti wa nishati ya gesi asilia,ambapo mafanikio yameanza kuonekana, huko SongongoSongo na Mnazi bay.

Tayari wananchi kadhaa wa Dar es Salaam na Mtwara wameanza kunufaika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na biashara , Bw.William Shellukindo,akitoa taarifa Bungeni, alisema kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kwamba utafiti unaongezewa nguvu kwa lengo la kugundua gesi asilia nyingine zaidi ili kuongeza matumizi katika maeneo mengi hata kuwahudumia watu wengi zaidi.

“Kazi hii iende sambamba na kuifikisha gesi hiyo mapema kule inakohitajika.

Kwa sasa wenye viwanda wengi nchini, Jijini Dar-es-Salaam,mikoani na hata nje ya nchi wangependa kutumia nishati ya gesi katika michakato yao ya uzalishaji,” alisema .

Kwa upande mwingine alisema, Serikali ifanye maamuzi ya haraka kuhusu matumizi zaidi ya rasilimali hiyo, kama vile matumizi ya kupikia majumbani na kuendeshea magari.

Aidha, matumizi hayo ya gesi asilia yaende sambamba na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi, ili waweze kukubali kutumia gesi badala ya mkaa.

Hata hivyo, watalaam wamekuwa wakishauri Serikali iweke vivutio maalum kwa wawekezaji katika shughuli za utafutaji wa gesi na vifaa vinavyotumia gesi.

Kama hiyo haitoshi, wamelitaka pia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kuwa na mkakati wa muda mrefu wa utafiti wa mafuta nchini kwa kushirikiana na mashirika makubwa ya kimataifa.

Kutokana na kupanda kwa bei za nishati ya mafuta katika soko la dunia na mahitaji ya nishati mbadala nchini, Shirika linatakiwa kufanya shughuli nyingi na kwa uharaka zaidi.

Shughuli za Utafiti ni muhimu sana kwa vile kuna kila dalili za kuwepo mafuta na gesi asilia kwa wingi nchini.

Katika mazingira hayo, ni vizuri kuongeza kasi ya utafiti ikiwemo kuipatia TPDC uwezo wa kushirikiana na wawekezaji katika sekta hii.

Taarifa za kupatikana kwa gesi asilia Tanzania ni ukombozi mwingine ambao sio tu utatumika kama chanzo cha nishati, gesi nyingine inaweza kutumika kwa matumizi mengineyo muhimu kulingana na ushauri au mapendekezo ya wataalam.

Mathalani unaweza kufanyika utafiti wa kina kwa gesi ya Mnazi Bay ili kupanua wigo wa matumizi yake ikiwemo ambayo inaweza kutumika pia katika uzalishajiwa mbolea za chumvi chumvi na bidhaa nyingine.

Wataalaam pia wamekuwa wakishauri,kuwa kutokana na kupanda mara wa mara kwa bei za mafuta katika soko la dunia, Tanzania haina budi kuelekeza nguvu zake kwenye tafiti za nishati mbadala kama vile maganda ya miwa kwa ajili ya nishati ya ethanol.

Mafuta ya petroli, umeme wa maji na mkaa wa mawe, ndiyo vyanzo vikuu vya nishati ya kibiashara nchini Tanzania.

Aina nyingine ya nishati itokanayo na kuni na mkaa kutoka katika miti, inachangia asilimia 93 ya matumizi yote ya nishati. Mafuta ya petroli yanaagizwa kutoka nchi za nje.

Sekta ya usafirishaji ndiyo inayotumia sana mafuta haya, ambayo ni asilimia 70 tu ya mahitaji yake ndiyo iliyofikiwa mpaka sasa.

Yako makampuni machache yanayofanya utafiti wa kugundua mafuta hapa nchini, lakini mpaka dakika hii, hakuna ugunduzi wa uhakika uliokwishapatikana.

Hivi karibuni zilisikika habari njema kwa watanzania hasa kuhusiana uwezekano wa kuelekeza nguvu katika nishati mbadala ya ethanol.

Ilisemwa kuwa, zaidi ya watanzania laki saba wanatarajiwa kupatiwa ajira katika sekta hiyo, baada ya Tanzania kuanza kutumia nishati ya ethanol inayotokana na miwa, badala ya petroli katika magari.

Nishati hiyo ya ethanol, ambayo itaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuitumia Barani Afrika, inatarajiwa kuanza kuzalishwa na kutumiwa kwa majaribio katika eneo la Bagamayo na katika bonde la Mto Rufiji, mkoani Pwani.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya SEKAB, Bw. Per Carstedt, aliyasema hayo katika mazungumzo yake na Rais Jakaya Kikwete wakati wa ziara yake ya kiserikali nchini Sweden.

`Tunatarajia, kama mambo yote yatakwenda sawa, tuanze uzalishaji wa majaribio mwezi Septemba huko Bagamoyo.

Baada ya hapo, tutahamia katika bonde la Mto Rufiji ambako tumepata eneo kubwa kwa ajili ya uzalishaji mkubwa,` Bw. Carstedt alimweleza Rais Kikwete.

Kufanikiwa hadi kukamilika kwa mradi huo huenda kutaisaidia serikali kubana matumizi ya fedha zake za kigeni katika kuagiza mafuta kutoka nje.

Pamoja na habari hizo njema , habari au ushauri wote unaweza kuwa ni kazi bure endapo serikali haitaweka mkazo wa kufuatilia kwa makini na kuyachukulia kwa uzito mapendekezo yote.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.