|
Eti baadhi ya walinzi wa usiku hugeuza viwanja vya ofisi walindazo gesti bubu?
2007-04-29 09:43:45
Na Anti Flora
``Nimesoma article yako ya tarehe 22/4/2007 kuhusu kichwa cha habari ``Kuliko niache kazi, heri nikuachilie mbali wewe!`` Hivi ndivyo anavyoanza msomaji wetu aliyesoma safu hii Jumapili iliyopita....anaendelea na email yake;
``Kusema kweli haya mambo yaliyompata bosi yapo, si ofisini tu hata majumbani mwetu mume kutembea na housegirl, mke kutembea na dreva wa mumewe, bahati mbaya huyo bosi kapatikana. Kwa hiyo mimi kwa maoni yangu wote wana makosa.
``(a) Kwanza huyu mama bila shaka hakujua kama mumewe ana binti huko ofisini kama si umbeya wa mtu aliyekwenda kumwambia. Huyu mbeya ndiye mbaya zaidi, maana mke asingejua bila kuaimbiwa.
``Sasa aliposikia kuwa yule mke kafa kwa kipondo, katika binafsi yake anajisikiaje? (huyo mbeya). Hapa nina maana yule mke wa bosi bila kuambiwa, asingeenda kufumania.
Hata kama alikuwa katika harakati za kupima uaminifu wa mumewe, ina maana walikuwa wanaishi kwa kuchungana na kuwekeana mitego bila kuaminiana ndani ya nyumba?
``(b) Mke wa bosi naye alichukulia jazba kumbe hasira hasara, alipozipata habari hizo toka kwa mbeya wake huyo, yeye angeenda kutafuta mtu mzima, mwenye busara, au bestman wa mume wake na kumwelezea hilo tatizo angeona jinsi ya kumsaidia, kuliko alivyo kwenda kichwa kichwa matokeo yake yakawa mauti.
``(c) Bosi naye umwamba wake umempeleka pabaya, alikuwa na hasira za kufuatwa ofisini na mke wake, pia alikuwa anamwonyesha binti kwamba anampenda kuliko mke wake, lakini hiyo yote ilikuwa bure.
Maana hiyo tabia kwa wanaume wakifumaniwa wanakuwa wakali sana kwa wake zao, sasa naye aende akakipate huko aliko.
``(d) Huyo binti, kusema kweli mabinti wa kisasa wana tamaa sana, wewe kama unajijua una mchumba, halafu unakwenda kufanya mambo yasiyokuwa na maana.
Namsifu kijana aliyetaka kumwachisha kazi pale na kutaka kumtafutia kwingine, maana yeye alitaka kuepusha shari na hilo li- bosi. Sasa binti yamemkuta ya kumkuta, sidhani huyo bosi kama atamuoa, na kijana kishamkosa.
Anamaliza kwa kusema, ``hayo ndiyo maoni yangu huko ofisini, gesti, sokoni, usione mambo hayaanikwi, lakini kuna mambo ya ajabu. Pia walinzi usiku wanafanya viwanja (campus) vya ofisi kuwa gesti.
Kwaheri.
Msomaji mwingine anaanza email yake namna hii:-Aunt Flora, Asalam aleikum. Mie ni mpenzi wako mkubwa kusoma safu zako. Imenigusa ile yakusema ni heri aachwe kuliko kuacha kazi yake.
Unajua watu kama hao wapo kwenye society zetu, tena sana. Lakini mie kilichonitia hofu ni kwamba kati ya jamii yetu hayo mambo yapo, tena sana. Utakuta baba mtu mzima, mheshimiwa mzima ana watoto wanaolingana nawe anakutaka kimapenzi. .
Regardless- hajali kwamba wewe ni mke wa mtu au la na isitoshe huyo mumeo anamfahamu fika.
Kweli society yetu imeoza, mtu unamtizama usoni na kama hayupo we tayari unatongoza mkewe.
Vibaya kweli jamani. Lakini na sie wanawake tunatakiwa tuwe na msimamo. Mume unaye halafu hilo jibaba linakuzingua.
Kuna maradhi tele na mengine hayana hata dawa. Learn to say no women(wanawake jifunzeni kusema hapana), tusiwe chombo cha kuchezea. Believe Iam talking from experience(niamini nazungumzia uzoefu wangu kwa hili).
Kabla sijaolewa it was understandable(kabla sijaolewa ilieleweka), watu wananitaka kila upande lakini sasa hivi tayari nina watoto wanne, bado mambo hayo yanaendelea. Hao sio wanaume bali ni wahalifu, wanataka kukuharibia maisha. Anamaliza email yake msomaji huyu.
Mpenzi msomaji, hayo ndiyo maoni ya wenzetu hao kuhusiana na mada ya wiki iliyopita.
Kumbe ndani ya familia zetu yapo mambo kibao yaliyofichika lakini tu hayaanikwi hadharani kama alivyobainisha msomaji katika email ya kwanza hapo juu.
Eti siyo katika baadhi ya ofisi zetu tu hufanyika ufirauni, bali hata walinzi nje ya ofisi hizo! Haya, jambo limezua mambo.
Ndiyo maana safu hii imetoa fursa kwa wasomaji kuchangia maoni au kupasua mambo yanayotokea ndani ya jamii ambayo yanaathiri maisha yetu ya kila siku.
Kwamba walinzi katika baadhi ya maofisi nao ni moto wa kuotea mbali nimewahi kudokezwa na jamaa fulani, wakionyesha kuwa huo ni mradi mkubwa wa mabwana hao(walinzi).
Hata baadhi ya mama ntilie wamejikuta wakirubuniwa na walinzi huku wakijidanganya ni wateja wao wa chakula kumbe, hata wao wanaliwa kijanja. Kumbuka wengine wao ni wake za watu lakini vishawishi huwakumba(si wote) ingawa wanajitahidi kujiongezea kipato.
Walinzi wengine nasikia hutumia maeneo ya nje za ofisi wanazolinda kuhifadhi wasichana walioamua kujitumbukiza katika ukahaba. Pindi wanapokosa mawindo ya usiku huwaangukia mabwana hao(walinzi) kuomba hifadhi.
Ibilisi wa ngono hachezi mbali. Baba fulani kwenye lindo(mwenye mke na watoto nyumba) anapomuona mrembo aliyevalia kiuchokozi(nusu uchi), ulimi nje.
Matokeo yake anajitosa, tena wakati mwingine bila kifaa cha kinga. Si ajabu wengine wamekwaa maradhi mabaya kutokana na kukiuka miiko ya kazi.
Mpenzi msomaji, Maisha ndivyo Yalivyo. Lakini yafaa sote tuvunje ukimya tuzungumze kwani athari za mambo haya kwa jamii yetu ni makubwa sana.
Maadam tumebaini dosari hizi, tutafakari namna na kuondokana nazo kwa ajili ya ulinzi kamili wa taifa letu.
Tusiyatizame tu yakitokea na kuyaona ni ya kawaida. Aliyegundua athari asikae kimya, zungumza, na safu hii iko wazi kwa ajili yako.
Wasalaam.
Email: fwingia@yahoo.com
|