|
Mabwana shamba watakaoajiriwa wasitokomee mijini, watulie vijijini
2007-04-29 09:44:41
Na Mhariri
Serikali inasema inakusudia kuajiri mabwana shamba 2,500 mwaka huu, ikiwa ni mkakati wa kuboresha kilimo nchini.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Stephen Wassira anasema hatua hiyo inafuatia kukosekana kwa uhusiano kati ya wataalam wanaomaliza Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na wakulima, ambao ndio hasa walengwa wa chuo hicho.
Katika mpango huo, Wassira amesema serikali itajenga nyumba katika vijiji kwa ajili ya mabwana shamba ambao wamekuwa wakikimbilia mijini badala ya kwenda mashambani kuonyesha ujuzi wao kwa vitendo lakini hukaa maofisini wakipigwa na upepo wa viyoyozi.
Mpango huu wa kuajiri wataalam hao wa kilimo, tunaamini utachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha kilimo chetu.
Kwa miaka mingi wakulima na wananchi kwa jumla wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa wataalam wa kilimo mashambani, hali inayochangia mavuno kidogo yanayochangiwa na kilimo duni.
Hata hivyo, uhaba huu wa mabwana na mabibi shamba upo sio kwa sababu hakuna wataalam hao nchini.
Sababu kubwa ni wataalam hao kukwepa kwenda mashambani, huku wakirundikana mijini ambako tunadiriki kusema hakuna shughuli za kilimo.
Nchi yetu ina vyuo au vituo vingi vya utafiti wa kilimo ambavyo hutoa watalaam kila mwaka, lakini cha ajabu ni kwamba watalaamu hao hawaonekani.
Ndiyo maana wakati tukiipongeza serikali kwa mpango wake huo wa kuajiri mabwana shamba 2,500 mwaka huu, ipo haja pia ya kuhakikisha wataalam hao wanakwenda vijijini ambako wanasubiriwa kwa hamu na wananchi wenye nia na uchu wa kilimo cha kisasa.
Zipo sababu kadhaa zinazowakimbiza mabwana shamba vijijini, mojawapo ikiwa ni kutokuwepo kwa nyumba bora za kuishi.
Bw. Wassira amesema serikali itahakikisha inajenga nyumba vijijini kwa ajili ya mabwana shamba.
Mpango huo ni muafaka kwa sababu tunaamini mabwana shamba wengi watavutiwa kwenda kuishi vijijini kwa sababu watakuwa wamehakikishiwa makazi bora.
Nyimbo za kuboresha kilimo chetu zimeimbwa kwa miaka mingi sana, lakini ajabu ni kwamba kilimo chetu kinazidi kwenda chini, hadi wakati mwingine nchi kukumbwa na balaa ya njaa licha ya utajiri wa ardhi yenye rutuba, mito, maziwa na kadhalika.
Ifike wakati sasa tuone aibu kuomba chakula kutoka nje wakati kwa utajiri tulionao sisi ndio tungepaswa kutoa msaada wa chakula.
Ni matarajio yetu kwamba mkakati huu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika unaoanzia kwa kuajiri mabwana shamba hao, hautakuwa maneno matupu.
Hata hivyo, serikali isiishie kuajiri tu mabwana shamba hao, bali ihakikishe wanakwenda mashambani kutoa msaada kwa wakulima.
Yafaa wafuatiliwe kwa karibu kuona wote wanachapa kazi ipasavyo vituoni wanakopangiwa ili mapinduzi ya kilimo yawe dhahiri.
|