30 Apr 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Awamu ya nne na staili yake ya kuibuka na mpya kila mara
 
2007-04-30 09:55:13
Na Hamisi Mzee

Tangu kuingia madarakani baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita, serikali ya awamu ya nne imekuwa ikiendesha mambo kwa staili ya kipekee.

Katika Makala haya Hamisi Mzee anaelezea suala hilo na ombi la wabunge la kutaka Waziri Mkuu awajibu wabunge papo hapo.

Serikali ya awamu ya nne ina staili ya kipekee kuendesha mambo. Hiyo ilijionyesha mara baada ya kutinga madarakani na kuteua watendaji kwa maana ya viongozi wa kada mbalimbali, mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu wakuu wa wizara.

Kiongozi wa awamu hiyo, Rais Jakaya Mrisho Kikwete alianza na mpya kwa kutembelea kila Wizara na kuzungumza na watendaji kwenye wizara zao.

Katika wizara hizo alibaini mambo mbalimbali na yeye kwa upande wake alitoa msisitizo na msimamo wa mambo ambayo anataka yatekelezwe kwa kutoa na kuboresha huduma kwa wananchi.

Kama hiyo ilikuwa haitoshi, Rais aliwakusanya mawaziri na watendaji wakuu wote kwenye semina elekezi ambayo malengo na majukumu ya serikali yake yaliwekwa bayana.

Wakati bado mambo hayajatulia, serikali hiyo imekuja na jipya jingine.
Kila mwaka imekuwa kawaida ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa serikali kuwasilishwa Bungeni.

Ripoti hiyo imekuwa ikionyesha udhaifu na ubadhirifu na matumizi ya hovyo fedha za serikali katika Wizara na idara za serikali na serikali za mitaa.

Safari hii Rais aliitisha kikao maalum kupitia na kujadili ripoti hiyo ambayo kama kawaida ilionyesha udhaifu wa usimamizi na ubadhirifu wa fedha za umma.

Ingawa baada ya kujadili ripoti hiyo haikutolewa amri ya kukamatwa watu wanaowezekana kuhusika na madhambi yaliyobainika, Rais aliagiza kila wizara na idara kuangalia sehemu inayowahusu na kushughulikia.

Mambo haya yote yanatokea katika kipindi kifupi cha uongozi wa serikali hii ya awamu ya nne.

Wakati haya yakitokea, wabunge nao kwa upande wao wamekuja na ombi lao.

Bila shaka ni katika moyo ule ule wa kuendeleza mambo mapya! Wao wanataka mabadiliko Bungeni, wanamtaka Waziri Mkuu awe na fursa ya kujibu maswali papo hapo.

Hili wanasema linafanyika katika mabunge mengine waliyotembelea kwenye nchi nyingine.

Waziri Mkuu anayefahamika zaidi kwa mtindo huu wa kujibu maswali papo hapo ni Waziri Mkuu wa Uingereza.

Kwa utaratibu wao waliojiwekea, Waziri Mkuu hutumia muda wa nusu saa kila siku ya Jumatano kuanzia saa sita mchana kujibu maswali ya wabunge.

Muda huo kwa kawaida huanza kwa maswali kuhusu shughuli za Waziri Mkuu ambapo wabunge wanauliza maswali ya nyongeza kuhusu jambo lolote.

Wabunge kwa kawaida hutoa maswali yao kuhusu shughuli za waziri mkuu na wanapofanya hivyo majina yao huorodheshwa kwenye kitabu cha maswali.

Baada ya kuulizwa swali la kwanza kuhusu shughuli za Waziri Mkuu, wabunge wengine wote waliojiorodhesha kuuliza swali kama hilo huitwa kuuliza swali lingine jipya la nyongeza.

Kinadharia chini ya utaratibu huu Waziri Mkuu anakuwa hajui swali atakaloulizwa.

Hata hivyo kwa kawaida Waziri mkuu huwa anapewa maelezo na idara husika za serikali kuhusu mambo ambayo yanaweza kuulizwa.

Utaratibu huu unaotakiwa na wabunge wa Tanzania unawezekana kabisa ukawa mzuri lakini ni muhimu kabla ya kujitosa na kuanza kuutumia ni muhimu tukaangalia mazingira , mfumo wa serikali na utamaduni.

Wakati Uingereza Waziri Mkuu ni mtendaji mkuu na kiongozi mkuu wa nchi, ingawa malkia ni mkuu wa nchi wa heshima, Tanzania Waziri Mkuu ni mkuu wa shughuli za serikali katika Bunge.

Waziri mkuu wa Tanzania madaraka yake si ya ukuu wa nchi kwani hayo ni madaraka ya Rais.

Katika hali hii utaratibu wa yeye kujibu moja kwa moja maswali ya wabunge unaweza kuwa mzuri au unaweza kuwa na athari zake.

Awali ya yote ni muhimu ifahamike kuwa Waziri Mkuu kwa kawaida huwa anajibu maswali Bungeni. Hujibu maswali kuhusu ofisi yake moja kwa moja au kupitia mawaziri wake wa nchi katika ofisi ya Waziri Mkuu na mara nyingine hutoa maelezo ya ziada na hata maamuzi pale majibu yanayotolewa na Wizara nyingine yanapoonekana kuwa hayakidhi swali la msingi au la nyongeza la mbunge ama wabunge.

Ingawa utaratibu huo unatakiwa na wabunge kwa Waziri Mkuu kujibu maswali moja kwa moja unaweza ukafaa, lakini kuna upande wa pili yake.

Faida kubwa ya kwanza ya utaratibu huo ni kwamba wanapata majibu yao haraka baadala ya utaratibu wa sasa wa maswali kuchukua muda mrefu kabla kujibiwa.

Tatizo linakuja pale majibu ya Waziri Mkuu yatakapokuwa ama kuonekana kuwa hayakidhi ama pale Waziri mkuu atakuwa nyota katika kujibu maswali.

Kinadharia hisia zinaweza kujengeka ama anafanya vizuri ama anamwangusha rais kutokana na udhaifu wake ingawa haya si mambo yanayotegemewa sana kuzingatia umahiri wa utendaji wa Waziri mkuu wetu wa sasa.

Uzoefu wa karibuni umeonyesha matatizo kidogo katika matamshi yanayotolewa na Waziri Mkuu kwa upande mmoja na Rais kwa upande mwingine.

Kwa mfano katika suala la matatizo ya umeme kutokana na maji kupungua katika bwawa la Mtera, Waziri Mkuu alikaririwa akisema kusingekuwa na mgawo lakini siku chache baadaye Rais alitangaza mgawo!

Suala la mikopo ya mabilioni ya Kikwete nalo lilizua jambo. Wakati Waziri Mkuu alikariiriwa akisema mikopo hiyo haina masharti, Rais mwenyewe akasema ina masharti!

Kwa mtazamo wa baadhi ya wachunguzi wa kisiasa, inawezekana kabisa wapo wabunge wanaotaka kutumia utaratibu huo wa kumuuliza Waziri Mkuu moja kwa moja wana lengo lao.

Imedaiwa katika duru hizo kwamba ni kutaka kumpa maswali ambayo hataweza kuyatolea majibu kutokana na kuwa nje ya uwezo wake hali ambayo bila shaka itampunguzia hadhi.

Vile vile kama utaratibu huo wa waziri mkuu utaigwa kwa mfumo na mambo yanavyoenda Uingereza, bila shaka utaleta kasheshe aina yake!
Kinachotokea Uingereza ni Waziri Mkuu anapokuwa akijibu swali, baaadhi ya wabunge hupiga kelele kama vile wanazomea.

Kwa upande mwingine katika duru hizo za kisiasa yapo madai kwamba wapo watu wanaotazama kwa mbali uchaguzi wa urais wa mwaka 2015 na kuna hofu hapa ya kutaka kuharibiana iwapo mtu ana matumaini kwamba anataka kuwania ofisi kuu ya nchi wakati huo.

Hata hivyo uko upande ambao unaona kwamba baadhi ya wabunge wanataka utaratibu huo kudakia na kuuliza maswali ya masuala ya kitaifa yanayowatangaza kibinafsi badala ya kushughulikia kero za majimbo yao.

Kwa mtazamo wowote ule ni muhimu mambo haya mapya yaliyoanzishwa na yanayokusudiwa kuanzishwa yashughulikiwe kwa umuhimu na uzito wake na matokeo yawe ni kuboresha huduma kwa wananchi na kuhamasisha maendeleo kwa jumla.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.