|
Mradi wa walimu unastahili kuigwa
2007-04-30 09:56:43
Na Mhariri
Rais Jakaya Kikwete hivi majuzi alizindua mradi wa jengo linalomilikiwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) jijini Dar es Salaam ambalo limejengwa kama kitegauchumi cha chama hicho.
Jengo hilo refu ambalo lipo katikati ya barabara za Kawawa na Uhuru, wilayani Ilala lilianza kujengwa tangu Aprili, 2004 na lilikabidhiwa rasmi mwezi Aprili mwaka jana.
Kulingana na taarifa ambazo zilitolewa na Katibu Mkuu wa CWT, Yahya Msulwa, fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo lenye thamani ya Shilingi bilioni 5.6 zilitokana na michango ya walimu pamoja na ada zao za uanachama.
Alisema kwamba lengo kubwa la kuwa na mradi huo ni kuboresha maisha ya wanachama wao ambao ni walimu waliotapakaa kila pembe nchini Tanzania.
Kwa hakika siyo Rais Jakaya Kikwete tu ambaye alivutiwa na ubunifu bora wa walimu katika kujitafutia suluhu ya kutatua matatizo yao mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.
Msulwa alisema kwamba ni matarajio yao ya baadaye kwamba jengo hilo ambalo gharama zake za ujenzi zitakuwa zimerejeshwa baada ya miaka kumi, faida yake isaidie kupanua shughuli za matawi mengine ya CWT nchini pamoja na kufungua miradi mingine.
Sisi tunadhani kwamba hii inawezekana hata kwa watumishi wa fani nyingine nchini kama vile wahasibu, wanasheria, waandishi wa habari, wauguzi, madaktari, makandarasi na kadhalika.
Tuna hakika kwamba hakuna linaloshindikana katika ubunifu wa miradi kama hii ambayo inaweza kupunguza kero kubwa za watumishi zinazotokana na vipato vidogo.
Hata hivyo uanzishaji wa miradi kama hii lazima iambatane na kujitoa kwa wanachama wenyewe kujua kwamba amana zao ndizo ambazo zinaweza kuwaletea manufaa ya baadaye.
Pamoja na hayo inatakiwa viongozi ambao wanachaguliwa kuviongoza vyama hivyo na miradi hiyo kuwa watu waaminifu ambao lengo lao kubwa ni kutafuta maslahi bora kwa kila mwanachama na siyo wao binafsi.
Haijalishi mradi ni mkubwa kiasi gani, iwapo utatawaliwa na viongozi wezi, wabadhirifu, wadanganyifu, wavivu na wazembe hakika hauwezi kufika popote na wanachama wake kamwe hata kama watajitoa namna gani wataendelea kuwa maskini.
Tunawapongeza walimu kwa juhudi kubwa kama hizo ambazo zimeweza kuonyesha mfano mwema ambao unastahili kuigwa.
Hata hivyo uboreshaji wa maisha ya walimu utategemea zaidi jinsi miradi hii itakavyosimamiwa na kupanuliwa jinsi siku zinavyozidi kwenda mbele.
|