|
Wenye uwezo wamechangia wingi wa watoto wanaozurura ovyo mitaani !
2007-06-10 10:00:35
Na Anti Flora Wingia
Kama nilivyoahidi wiki iliyopita, leo niwageukie watoto wetu hasa wale wanaojikuta katika maisha magumu, japokuwa wengine bado wako karibu kabisa na ama wazazi wao au walezi wao.
Tatizo la watoto wanaoishi mitaani huku wakijitafutia mlo peke yao, ingawa umri huo walipaswa kuwa shuleni, lina sura nyingi. Yapo mambo mengi yanayopelekea watoto hao kutaabika huku jamii ikitizama kana kwamba ni jambo la kawaida.
Baadhi ya watoto imeelezwa kwamba wapo mitaani baada ya wazazi wao kufariki, wengine baada ya kufarakana, kutengana au wengine kulazimishwa na wazazi au walezi wao kuingia mitaani kufanya biashara ndogondogo ili kupata kipato kwa familia.
Mpenzi msomaji, katika pitapita zangu hivi karibuni katika maeneo ninakoishi, nimegundua sababu nyingine iliyofichika ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu mitaani.
Hebu sikia kituko hiki nilichokishuhudia na kupata ukweli wa kile kilichokuwa kinaendelea. Nikiwa duka jirani na nyumbani kwangu nikipata soda, alifika bibi mmoja akimtafuta mjukuu wake.
Kuja kwake pale bibi huyu, ni baada ya kudokezwa kwamba mjukuu wake alionekana pale akitizama kipindi cha Ze Comedy kinachorushwa kwenye luninga ya ITV kila Alhamisi na kurudiwa Jumapili jioni.
Na kweli bibi yule kufika tu pale, mjukuu wake naye akawa amemuona na kuondoka taratibu. Wakati mtoto yule akiondoka kwenda nyumbani, nilimtafadhalisha bibi asubiri anieleze kulikoni anamfuatilia mjukuu wake wakati ule.
Bila kusita akasema, ``unajua mjukuu wangu huyu nilimtoa Tabora kwa mama yake ili nikae naye. Anasoma darasa la tano. Lakini amekuwa mtundu, mtoro shuleni na yupo mtoto mwenzie mtukutu sana ambaye ndiye aliyemharibu. Ndiye anayemshawishi wasiende shule wakaibe vitu majumbani mwa watu na kuuza kwa lengo la kujipatia hela.
``Nimejaribu kumrekebisha mjukuu wangu huyu nimeshindwa kutokana na kujiunga na makundi mabaya.
Sasa nimedhamiria kumwitia polisi wamkamate wajaribu kunisaidia kumtishia ili asome...ana akili sana lakini shuleni haonekani. Ataondoka asubuhi na madaftari lakini kumbe haendi shule” anasema kwa masikitiko bibi huyu.
Bibi akaondoka zake kumfuatilia mjukuu wake.Dakika chache baadaye, akajitokeza mtoto yule ambaye bibi alikuwa akimshutumu kwamba ndiye anayemharibu mjukuu wake.
Mtoto huyu aliingia pale kwa kasi na kuchungulia chumba kilichokuwa kimejaa vijana wakitizama Ze Comedy, akionyesha kumtafuta mtu, kisha akataka kuondoka.
Ndipo nilipomsimamisha na kutaka kujua anamtafuta nani na pia maoni yake kuhusiana na tuhuma nilizokuwa nimepata punde. Nilianza kwa kumhoji: We waitwa nani? Naitwa ...(jina kapuni).
Una umri gani? miaka 11. Unasoma darasa la ngapi? La tano. Lakini nimepata taarifa kuwa wewe mtoro sana...na sasa huendi kabisa shule...kwanini? Wazazi wangu hawanifuatilii. Unapenda shule? Ndio. Sasa kwanini unatoroka?(kimya).
Ni kweli unaharibu wenzako kwa kuwafundisha utoro na wizi? Siyo kweli wenyewe wananifuata.
Mpenzi msomaji, mtoto huyu ukimtizama anaonekana jasiri na mwenye kujibu maswali kwa uangalifu, jambo linaloashiria kuwa akilelewa vema anavyo vipaji vya kutosha. Lakini kwa mujibu na baba mmoja aliyekua pale na ambaye ni mjumbe wa mtaa jirani, mtoto huyu wa pili ameshindikana kabisa.
Hapo anapoishi yuko na mama yake mzazi anayeishi katika nyumba ya urithi. Nyumba hii imejaa wapangaji, wengi wakiwa wasichana wasio na kazi maalum.
Tena naambiwa wasichana hao wakati mwingine humtuma mtoto huyo kwenda kutafuta pesa kisha akirudi awagawie. Mtoto huyo pia amekuwa akiwahonga wasichana hao wakubwa na hata hudiriki kumtaka kingono. Hii ni hatari kubwa.
Utafiti niliofanya kwa wiki mbili hivi, nimegundua kuwa zipo familia nyingi maeneo ya nje ya Jiji la Dar es Salaam ambazo zimejihifadhi katika nyumba ambazo hazijaisha kujengwa kwa ajira ya ulinzi.
Mtu anaomba kulinda nyumba fulani anaoa akiwa hapo kwenye lindo au anahamia na familia yake hiyo akitokea lindo lingine au nyumba ya kupanga. Mwenye nyumba anapohamia, bado familia hii hujengewa banda dogo pembeni ili iendelee kuishi.
Familia za aina hii ndizo baadhi ya watoto wake wamekuwa wakiranda mitaani na kufanya vitendo vya uhalifu. Hata bibi yule niliyemgusia awali katika makala hii pia amezeekea kwenye lindo kwa mtindo huo.
Familia za aina hii baadhi zimekuwa zikihama hama wakati mwingine kutokana na mwenye nyumba kuachana nazo baada ya kuhamia na kuzitaka zitafute sehemu nyingine. Matokeo yake hujikuta wakitafuta maeneo mengine ya kuishi jambo ambalo pia huathiri maendeleo ya watoto.
Kazi ya ulinzi kipato chake ni kidogo. Tena mwenye nyumba aweza kukupunja kwa kigezo kuwa hulipi kodi ya banda alilokuhifadhia. Ndio baadhi ya watoto huishia mitaani wakiombaomba kunusuru maisha.
Juzi niliona mama mmoja muuza vitumbua akiwa anakaanga vitumbua vyake huku watoto wa kiume wanne wakiwa wamemzingira. Wakati huo alikuwa akigombana nao kwa kuwa walitaka vitumbua vya bure bila kutoa fedha wakidai hawana fedha na wazazi wao hawajaandaa kifungua kinywa chochote.
Nilijongea na kumuuliza mama yule kulikoni akasema watoto wale wanataka vitumbua kwa nguvu huku wengine wakijichukulia wenyewe sufuriani baada ya kuwakatalia. Hata hivyo aliwapa kila mmoja kitumbua kimoja hivyo wakanyanyuka na kuondoka.
Mama huyu alisema watoto wale wanaishi eneo lile jirani na japokuwa wanao wazazi wao, lakini wanazurura baada ya wazazi kuwachoka kutokana na utundu pamoja na utoro mashuleni.
Wazazi wao ni wale wanaolnda nyumba za wakubwa wengine bado kuhamia na wengine wamehamia lakini wamewajengea mabanda kwa kazi ya ulinzi.
Kazi hiyo imewafanya wazazi hawa kubweteka na kuishia kujibana upenuni mwa matajiri zao bila kutambua athari za maisha ya aina hiyo kwa watoto wao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete akizungumza na wananchi kupitia kwa wahariri wa habari Jumatano wiki hii Jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine alizungumzia utoro mashuleni, moja ya matatizo yanayolisumbua taifa.
Akitoa takwimu za ongezeko la utoro shule za msingi, Rais Kikwete akasema mwaka 2005 wanafunzi watoro walikuwa 32,000. Mwaka jana idadi hiyo iliongezeka hadi watoto 44,742. Katika sekondari mwaka 2005 watoro walikuwa 6,912 lakini mwaka jana iliongezeka hadi kufikia 7,734.
Kitakwimu, hiyo ni idadi kubwa sana kwa utoro wa wanafunzi wetu. Wazazi na jamii kwa jumla yafaa kulitizama tatizo hili kwa mapana kuona nini kifanyike kunusuru rika hili ambalo ni tegemeo kubwa sana katika mwendelezo wa taifa.
Mfano familia nilizogusia ambazo maisha yake ni kutegemea hifadhi ndani ya familia zingine. Nini kifanyike? Uwezo wa familia hizi ambazo naweza kuziita ni pandikizi ni mdogo kujikimu kimaisha.
Serikali na vyombo vyake vinavyoshughulikia ustawi wa jamii vifanye utafiti kujua idadi ya familia za aina hii na kuona namna ya kuzikwamua ili hata matatizo mengine yanayochipuka ya wingi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu mitaani yaweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Jambo hili si la kupuuzia hata kidogo. Vinginevyo nchi itafikia mahali na kujikuta ikiwa na matabaka ya kutisha huku lile la juu likichekelea kwa neema na lingine likikodoa macho lisijue cha kufanya.
Watoto waliojitosa mitaani bado jamii inaweza kuwanusuru badala ya kuwatizama tu .
Mzazi wa mtoto aliyejitumbukiza katika uzururaji baada ya kutoroka shuleni asikate tamaa. Atafute ushauri katika vyombo mbalimbali kujaribu kumrejesha mtoto husika katika maisha salama na bora.
Hili linawezekana. Jamii ikiamua kukomesha utoro wa watoto shuleni, rika hilo litakuwa limeepushwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na vitendo viovu kama vile wizi, ngono toto na kadhalika.
Hata hivyo unahitajika mchango wa mawazo, maoni tujue nini cha kufanya.
Mpenzi msomaji, mimi ni mtohoaji au tuite mchokozaji tu katika safu hii. Je, nini maoni yako kuhusu nilichozungumzia katika makala hii? Tuma kupitia email hii hapa chini na yatachapishwa hapa hapa.
Wasalaam
Email: fwingia@yahoo.com
|