|
Serikali za Afrika zitumie utaratibu mpya kuondoa kero za wafungwa
2007-06-11 08:55:17
Na Timothy Kahoho
Siku ambayo Rais Jakaya Kikwete alitembelea magereza matatu katika Mkoa wa Dar es Salaam, alishuhudia kero kemkem za wafungwa kwenye magereza hayo.
Rais Kikwete aliweza kujionea mwenyewe na kuhuzunishwa sana na msongamao mkubwa wa mahabusu katika Gereza la Keko na pia na kusikitishwa mno na hali za wafungwa wengi katika magereza mawili ya Ukonga na Segerea.
Kusema kweli Kikwete amekuwa ni kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kabisa katika taifa letu tangu nchi yetu ipate uhuru mnamo mwaka 1961, aliyethubutu kuingia gerezani na kushuhudia taabu zinazowakabili wafungwa, ikiwa ni pamoja msongamano mkubwa wa watu hao waliokataliwa katika jumuia zetu.
Msongamano huo unaelezwa kuwa umechangiwa na dhana potofu kwamba mahali pekee pa kumkomesha mtu anayetuhumiwa kwa uhalifu au anayepatikana na hatia ya kosa la jinai ni gerezani.
Dhana hiyo inadhihirishwa na mahakimu na pia na majaji wanapotoa adhabu kwa washtakiwa wanapopatikana na hatia fulani.
Kwa kweli, hiyo ndiyo dhana inayopelekea magereza yoye nchini na katika nchi za Kiafrika yafurike kwa kiwango cha kutisha na hatimaye kusababisha serikali zetu zitumie gharama kubwa sana katika kuwatunza wakati wangali wanatumikia vifungo vyao.
Asasi moja nchini ijulikanayo kama Tanzania Prisoners Rights Foundation (TPRF), imekuja na ufumbuzi huo kwa lengo la kuwaelimisha Watanzania jinsi ya kupunguza msongamano kwenye magereza yetu na hatimaye kuwa mfano bora katika Afrika kwa ujumla.
Asasi ya TPRF ilisajiliwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Shein, kunako Juni 5, 2006, ambapo ilipewa hati ya usajili namba 00NGO/0115, chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Bw. Gaudiosius Ishengoma, na Makamu Mwenyekiti, Bw. Aden Rage.
Mwenyekiti wa TPRF, Bwana Ishengoma anabainisha kuwa asasi hiyo ina mikakati ya kupunguza msongamano wa watu hao kwenye magereza yetu kwa kuwapa kwanza msaada wa kisheria kuanzia Kituo cha Polisi hadi Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa TPRF, ni kwamba mtu anapokamatwa na Polisi kwa kutuhumiwa kwa kosa lolote lile, tayari ni mfungwa.
Hufikishwa kwenye Kituo cha Polisi na kuwekwa mahabusu kwa ajili ya kuhojiwa.
Kisheria, anaposwekwa ndani hujulikana kama mtuhumiwa na hivyo anatakiwa akae ndani kwa masaa yasiyozidi 24.
`Mtu anapotiwa mbaroni huwekwa mahabusu kwa masaa 24 tu, baada ya hapo anapaswa kupelekwa mahakamani,` anaeleza bosi huyo wa TPRF.
Hata hivyo, anasema kuwa kutokana na kutoelewa sheria hii, watuhumiwa wengi wamekuwa wakikaa kwenye mahabusu ya Vituo vya Polisi hadi wiki kadhaa bila kufikishwa mahakamani.
Anasema kuwa hapa ndipo umuhimu wa TPRF unapokuja kuonekana kwa kuwasaidia watuhumiwa tangu wanapokuwa kwenye Vituo vya Polisi kwa kuhojiwa.
Anaeleza kuwa watuhumiwa wanaokabiliwa na makosa madogo, kwa mfano wale wanaokamatwa wakiwa na misokoto miwili au mitatu ya bangi, wapika gongo, na kadhalika, si lazima wawekwe mahabusu kama wanao watu wa kuwadhamini wanaoaminika.
`Mtuhumiwa anapohojiwa na Polisi, ni sharti awepo ndugu yake kama shahidi au mwanasheria wake, kwa shabaha ya kuepuka malalamiko ya kubambikiziwa makosa ya jinai au mateso kwenye vituo vya polisi ili akiri kosa ambalo hakulitenda,` anadokeza.
Anasema mara nyingi watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani, huwalalamikia mahakimu kuwa wametwishwa makosa ya ujambazi na mauaji na hali wakati wa kukamatwa kwao walikutwa na bangi au lita kadhaa za gongo ama wakitembeza bidhaa zao mitaani.
`Ni jukumu la TPRF kulinda haki za watu kama hao wanapokuwa kwenye Vituo vya Polisi ili wasionewe kwa kubandikiziwa makosa ambayo hawakuyatenda,` akasisitiza Ishengoma.
Ishengoma anasema kuwa majukumu mengine ya asasi hiyo yatakuwa kuwasaidia kisheria washtakiwa ambao hawana uwezo wa kuwaajiri wanasheria.
Hii ni pamoja na kuwasaidia wakati wa kujibu mashtaka yao mbele ya mahakimu, kuwaombea dhamana, na kuendesha kesi zao hadi mwisho.
`Washtakiwa wengi wanapokuwa nje kwa dhamana, husababisha Gereza la Keko kuwa na mahabusu wachache sana na hivyo kuiwezesha serikali kugharimia kidogo kwa ajili ya chakula na matibabu,` anazidi kubainisha.
Anasema washtakiwa wa makosa madogo wanapaswa kupewa dhamana na mahakama kwa masharti nafuu ili kupunguza msongamano wa mahabusu katika Gereza la Keko na kwingineko.
Anaeleza kuwa si busara kwa mahakimu kuweka masharti magumu ya dhamana kwa washtakiwa wa makosa madogo, kama vile kukutwa na Polisi na misokoto kadhaa ya bangi, kupika na kuuza gongo, wizi wa fedha hadi kufikia sh. 5,000,000.00 na kadhalika.
Anafafanua kuwa Kikwete alikuta huko Keko zaidi ya nusu ya mahabusu wanashtakiwa kwa makosa kama hayo na kukaa kwa zaidi ya miezi sita bila kesi zao kusikilizwa.
Anasema kama washtakiwa hao wangepewa dhamana na mahakama kwamba, angekuta mahabusu wachache sana na wenye kesi nzito.
Kuhusu kufurika kwa wafungwa gerezani, kiongozi huyo wa TPRF anasema inatokana na mahakimu na majaji kutofuata taratibu za mwenendo wa kesi za jinai na kutozingatia ushahidi wa pande zote mbili katika kuwatia hatiani washtakiwa.
`Ndiyo maana TPRF ina jukumu lingine la kuwakatia rufani wafungwa ambao hawakuridhika na hukumu zao,` anadokeza.
Ametoa mfano wa kesi moja ya mshtakiwa, Adam Gamsho Saddam, iliyosikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu hadi kuhukumiwa na kupewa kifungo cha miaka 30 kwa kupatikana na hatia ya kosa la ujambazi.
Anadai kuwa Saddam alihukumiwa mnamo Aprili 4, 2006, kwa kosa la unyang\'anyi kwa kutumia silaha na kumpa adhabu hiyo pamoja na kuchapwa viboko 12.
Anasema, TPRF ilimkatia rufani katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ambapo rufani yake hiyo ilisikilizwa na Jaji Aboud mpaka adhabu ya kifungo chake ikabatilishwa hapo Aprili 30, 2007, na kusababisha awe mtu huru.
`Wako wafungwa wengi wanaotumikia vifungo vyao kwa kubambikiziwa makosa ya jinai na kisha kukosa msaada wa kisheria kwa sababu ya umaskini wao,` alizidi kubainisha.
Alieleza pia kuwa asasi hiyo ilifungua Rufani ya Jinai Na. 68 ya mwaka 2007 katika Mahakama Kuu hivi karibuni ya mwanamke mmoja, Sarah John, aliyehukumiwa na mahakama hiyo mnamo Aprili 10, 2007, kwa kupatikana na hatia ya kuvunja na kuiba kunako Septemba 14, 2006.
`Mnamo Mei 18, 2007, tulimkatia Sarah rufani kwenye Mahakama Kuu, kufuatia uchunguzi wetu kuwa mwanamke huyo alihukumiwa kwa kosa ambalo hakuwa amelitenda,` amedai Ishengoma.
Anaeleza kuwa alishtakiwa na mwajiri wake kwa kudaiwa kuvunja saluni siku hiyo ya tukio wakati alikuwa anauguza mtoto wake.
Anadai kuwa hakimu wa mahakama hiyo alimwona kuwa na hatia ya kosa la kuvunja ofisi ya mwajiri wake na kisha akamwadhibu atumikie kifungo cha miaka mitatu.
Kadhalika, anasema hakimu huyo alimtia hatiani kwa kosa la pili la wizi wa vitu mbalimbali katika saluni hiyo vyenye thamani ya Sh. 800,000/= na kumpa adhabu ya kifungo cha miaka mitano.
Mbali ya rufani hizo, Ishengoma anasema TPRF imekuwa ikimsaidia mshtakiwa mmoja, Joseph Shira Mashini, anayekabiliwa katika Mahakama ya Kisutu na makosa mawili, moja likiwa la utapeli, na lingine la kujipatia kiasi cha Sh. 5,000,000/= kwa njia ya udanganyifu.
`Mashini alifikishwa mahamani tangu Novemba 16, 2004,` anabainisha.
Anaeleza katika jitihada za asasi hiyo kushughulikia kwa vitendo kero za wafungu, itaendelea kutoa msaada wa kisheria kwa watu wanaokabiliwa na kesi za jinai na pia kuwakatia rufani wafungwa wasio na uwezo wa kuwaajiri mawakili.
Anasema hivi sasa asasi hiyo inaangalia uwezekano wa kuanzisha kambi za kurekebisha tabia za wahalifu ili wawe raia wema na kuendeleza vipaji yao kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.
`Tuna kifungu cha 105 cha Sheria ya Magereza iliyotolewa kwenye G.N. Na.77 mwaka 1968,` anabainisha na kuongeza kuwa \"kama inatumiwa vizuri inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wafungwa kwenye magereza yetu`.
Anaelezea sheria hiyo kuwa inaruhusu kuwepo kambi za wafungwa zinajulikana kwa kimombo kama camp for extra-mural prisoners, kwa ajili ya wenye vifungo vya muda mfupi kutumikia adhabu zao kwa kuishi nje ya magereza.
Anahitimisha kwa kusisitiza kuwa ni wajibu wa Serikali za Afrika kutumia utaratibu mpya kuondoa kero za wafungwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Bara la Afrika.
|