|
Kila la kheri Wabunge
2007-06-12 09:47:27
Na Mhariri
Bunge la Serikali ya Muungano ya Tanzania leo linaanza kikao chake cha kila mwaka cha bajeti kwa mwaka 2007/2008 kuweka dira ya mwelekeo wa makadirio ya mapato na matumizi ya serikali ambayo hugusa maisha ya kila mwananchi.
Umuhimu wa kikao cha bajeti unamgusa kila Mtanzania hasa ikizingatiwa kwamba ni katika bajeti hiihii ambapo serikali hutangaza unafuu au kupanda kwa gharama za bidhaa mbalimbali zitumikazo ndani ya jamii.
Ni katika kikao hikihiki ambapo Waheshimiwa Wabunge kuanzia leo wanatakiwa kuangalia kwa makini mustakabali wa bajeti za kila wizara, kuzihoji na hatimaye wanaporidhika kuzipitisha.
Jukumu hili ambalo wamekabidhiwa Wabunge ni kubwa mno kwa vile ndiyo kielelezo cha maisha ya Watanzania kwa kipindi cha mwaka mzima.
Siyo kusudio letu kurejea kukumbusha majukumu yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wanastahili kufanya wawapo kwenye kikao hiki muhimu hasa tukiamini kwamba kila mbunge aliyechaguliwa na wananchi amekula pia kiapo cha kuwatumikia Watanzania wote kwa uaminifu, uadilifu na nguvu zote.
Hatutarajii kuona katika kikao kama hiki kinachoamua masuala mazito na nyeti ya Watanzania, panakuwepo na Wabunge `wasindikizaji` ambao ushiriki wao bungeni siyo kamilifu na hauwawakilishi inavyostahili wapigakura wao.
Tumekuwa tukishuhudia katika vikao vilivyotangulia baadhi ya Wabunge wakisifika kwa tabia za kuwa ‘watoro sugu’ ambapo muda mwingi wa kikao hicho hufanya shughuli zao binafsi badala ya kuhudhuria vikao vya bunge la bajeti.
Hata hivyo inasikitisha kwamba Wabunge haohao bila aibu huchukua malipo yote yanayohusiana na vikao hivyo huku wakijua fika kuwa kufanya hivyo ni sawa na wizi.
Halikadhalika tumeshuhudia pia Wabunge kadhaa ambao huishia kuchapa usingizi hasa baada ya chakula cha mchana ndani ya ukumbi wa Bunge, kitendo ambacho kinashusha hadhi na heshima ya Wabunge hao binafsi, waliowachagua na bunge zima kwa ujumla.
Ni vizuri katika kikao hiki cha bajeti Mheshimiwa Spika akawa karibu zaidi katika kuhakikisha kuwa Wabunge wote wanashiriki kikamilifu kuchangia mawazo yao mazuri badala ya kubaki kama wasikilizaji tu.
Tunahitaji kuona bunge lililochangamka, bunge ambalo siyo tu linakubali kupokea na kupitisha bali pia kuhoji pale panapoonekana kuwepo kwa mushkeli kwenye bajeti zinazofikishwa bungeni.
Hata kama bajeti zinazowasilishwa na wizara mbalimbali ni sahihi, ni vizuri usahihi huo ukapata baraka za dhati badala ya kuzipitisha bajeti katika staili ya ‘bora liende’ na hatimaye kuzua mizigo mizito kwa wananchi.
Ni matarajio ya Watanzania walio wengi kuwa Waheshimiwa Wabunge wataendeleza hekima na ufahamu mkubwa walionao katika kufanya maamuzi sahihi kwenye kikao hiki cha bajeti mwaka huu wakilenga zaidi katika kuinua ubora wa maisha ya Watanzania.
|