12 Jun 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Motisha kwa wanafunzi kama chachu ya elimu
 
2007-06-12 09:48:12
Na 

Serikali imetoa changamoto kwa Jumuiya na taasisi zinazoendesha elimu nchini kuongeza juhudi na mbinu katika uendeshaji ili kufanikisha utoaji wa elimu bora kwa wote. Moja ya mbinu hizo ni kuwapa motisha wanafunzi wanaofaulu mitihani kwa viwango vya juu.

Changamoto hiyo imetolewa na Waziri mwenye dhamana ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi.Margreth Sitta. Katika Makala hii Mwandishi ABDUL MITUMBA anaeleza chimbuko la changamoto hiyo.

Chimbuko la changamoto ya kuwapa motisha wanafunzi wanaofaulu ni Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao walibuni utaratibu wa kuwapa tuzo wanafunzi wanaofanya vizuri katika matokeo ya mitihani yao.

Jumuiya hiyo inamiliki shule za sekondari zaidi ya 80 kote nchini, zikiwemo zinazotoa elimu ya kidato cha nne na sita.

Mpango huo kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Margreth Sitta ni moja kati ya jitihada za ziada ambazo angependa kuona taasisi na jumuiya zinazoji-shughulisha na utoaji wa elimu zikichukuwa.

Waziri Sitta anaamini kwa kuwapa tuzo mbalimbali ikiwemo fedha wanafunzi vinara, kwa kiasi kikubwa inaweza kuongeza changamoto na morari kwa wanafunzi wengine kuibua mawazo mapya vichwani katika siku za usoni kielimu.

Bi. Sitta anasema , watu wanaopewa motisha kwa kufanya vizuri katika nafasi zao za kazi achilia mbali wanafunzi, morari yao inaongezeka mara dufu, hivyo kuibua ziada ya fikiri na kwa wakati muafaka.

``Sisi wakati tunasoma, ukifanya vizuri kama mlivyofanya ninyi hapa, tulikuwa tunapewa zawadi ndogondogo kabisa. Mfano wa zawadi hizo ni kalamu za wino, penseli, ngao na wakati mwingine sahani za udongo,`` alisema.

Akasema hali hiyo iliongeza chachu ya kufanya vizuri, tofauti na ilivyo sasa, ambapo wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani yao, hupewa zawadi nono.

``Achilia mbali mashirika, taasisi na Jumuiya mbalimbali, hivi sasa zawadi pia zinatolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kupitia wizara yangu, hali inayoashiria kwenda sambamba na wakati kulingana na mahitaji,`` anasema Waziri Sitta.

Aliongeza kuwa kitendo cha Jumuiya hiyo kubuni mpango wa kuwatunuku vyeti na zawadi nyinginezo wanafunzi wanaofanya vizuri ni hatua muhimu inayopaswa kuungwa mkono na kuboreshwa kila inapowezekana.

Waziri Sitta aliwakumbusha viongozi wa Jumuiya hiyo umuhimu wa kuzifanya shule zao kuwa bora hivyo kuwa kimbilio la wanafunzi, huku wakiboresha maslahi ya walimu na watumishi wengine kadri itakavyowezekana.

Kwa sasa shule ambazo wanafunzi wake wanafanya vizuri zaidi ni zile zinazomilikiwa na taasisi za kidini, nyingi zikiwa zile zinazomilikiwa na makanisa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi taifa, Bw.Abiud Maregesi alisema hatua ya kuanzisha mpango wa kutoa motisha kwa wanafunzi umeanza mwaka huu na utaendelea kila mwaka.

Anasema kwa kuzingatia umuhimu wa sekta ya elimu Jumuiya yake inakamilisha mipango ya muda mrefu ya kuwatunuku walimu wakuu na wanaofanyakazi ili kuwaongezea bidii ya kufundisha bidii ili kuweka uwiano wa motisha hatimaye kufikia malengo ya kukuza elimu.

Bw.Maregesi anasema ili kufikia malengo hayo na mengine, Jumuiya yake imebuni mikakati ya miaka mitano mitano ya kuboresha shule zake ikianza na miaka miwili iliyopita.

``Maboresho hayo ni pamoja na kuimarisha majengo ya shule zenyewe na vifaa vya kufundishia, kumalizia kazi ya ujenzi wa baadhi ya shule pamoja na kukarabati zile ambazo majengo yake yameanza kuchakaa ili ziwe za kisasa,`` alisema.

Bw.Maregesi aliwataja wanafunzi hao wa kwanza kupewa motisha na Jumuiya yake kuwa ni Jane Nelson kutoka sekondari ya Sangu mkoani Mbeya aliyepata pointi nne katika masomo ya HGL.

Wengine ni Erick Brighton (HGK) ya pointi nne na Hashim Mgandilwa (HGK) pointi nne wote kutoka sekondari ya Mbarali ya mkoani Mbeya ambapo kila mmoja alipewa cheti na kitita cha sh.300,000.

Aidha, Bw.Maregesi alisema waliotunukiwa vyeti na fedha sh.200,000 kila mmoja Joseph Issaya (HKL), Neema Mwaipyana (HKL) na Sauda Kazindogo (HKL) ya pointi tano wote kutoka sekondari ya Meta iliyopo mkoani Mbeya.

Kulingana na Bw.Maregesi, mwanafunzi pekee aliyetunukiwa cheti na fedha sh.200,000 kutoka sekondari ya Mombo iliyopo mkoani Tanga ni Yona Maiko ambaye alipata cheti na fedha sh.200,000 baada ya kufanya vizuri katika masomo ya HGK ya pointi tano.

Wanafunzi hao walitunukiwa vyeti vyao na Waziri Sitta, ambapo naye alitoa sh.50,000 na kuchangia katika fedha zilizotolewa na Jumuiya pamoja na sh.50,000 nyingine zilizotolewa na Bw.Maregesi kwa wanafunzi hao.

Naye katibu wa Jumuiya hiyo wilaya ya Kinondoni, Bw.Stanley Mkandawile anasema Jumuiya yake inakusudia kujenga shule ya sekondari mpya ya kidato cha kwanza hadi sita katika eneo la Wazo Juu ili kuwasogezea wanafunzi huduma ya elimu jirani.

Shule hiyo itakayokuwa na mchepuo wa kilimo na ufugaji, itajihusisha zaidi na mpango wa kuwaandaa wanafunzi kuwa wajasiriamali wasomi punde wanapomaliza kidato cha nne na sita.

Wakizungumza na Nipashe, wanafunzi Hashim na Erick walisema pamoja na kufanya vizuri katika mitihani hiyo, hawajawahi kuwa na wazo kuwa wangekuja kupewa tuzo na fedha na mtu yeyote.

``Lazima niwe mkweli, pamoja na matarajio yangu ya kufanya vizuri katika mitihani yangu ya kidato cha sita, sikuwa na wazo ningekutana na Waziri akanipa mkono na kunizawadia chochote kwa sasa,`` alisema Hashim.

Naye Brighton alisema kwa hakika tukio la Jumuiya kuwatunuku vyeti maalum na fedha, limewapa moyo zaidi wa kufanya vizuri katika masoko yao katika vyuo vikuu, ambapo yeye na Hashim wameomba kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani.

Akihitimisha mazungumzo yake katika hafla hiyo, waziri Sitta alishauri Jumuiya kufuatilia mienendo ya wanafunzi hao katika vyuo vikuu watakosoma ili kujua matatizo yao na nini wanahitaji ili kufikia malengo yao.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.