|
Kupiga hatua zaidi: Bajeti ipunguze utegemezi kutoka nje
2007-06-15 08:38:36
Na FELIX ANDREW
Pamoja na kuwa bajeti ya serikali kwa kipindi cha mwaka 2007/08 imetoa kipaumbele katika maeneo kadhaa, bado wananachi wamekuwa wakitoa mapendekezo zaidi ya namna ya kuifanya bajeti hiyo kuwa yenye kuleta maendeleo.
Mapendekezo yanayotolewa yanalenga kuboresha sekta za miundombinu, elimu na rasilimali watu na pia kupunguza bajeti tegemezi.
Sekta binafsi imeeleza msimamo na matarajio yake kuhusiana na bajeti ya serikali ya mwaka huu wa fedha 2007/2008 ambayo tofauti na miaka mingine imeamua kutoa kipaumbele katika maeneo fulani ikiwa ni nia ya serikali kuweza kuyaboresha maeneo hayo na hivyo kupata kasi katika suala zima la kuinua uchumi wa nchi.
Wakizungumza katika mahojiano baadhi ya wadau wa sekta binafsi wameonyesha kuwa na matumaini na bajeti hiyo na kupendekeza mambo kadhaa ambayo yanaweza kusaidia maendeleo ya uchumi wa nchi yetu.
Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta binafsi nchini (TPSF) Bw. Louis Accaro amesema ili bajeti hiyo iweze kusaidia kukua kwa uchumi lazima iangalie sehemu tatu.
Amependekeza kwa serikali kuweka msisitizo zaidi katika kufufua au kuendeleza miundombinu hasa maeneo ya vijijini.
`Kwa sasa moja ya jambo kubwa ambalo sisi kama sekta binafsi tumeliona linakwamisha maendelo ni ubovu wa miundombinu ya nchi yetu ,kwa kweli inapaswa kuwekewa fungu la ziada ili kuifanya nchi iendane na wakati.
Miundombinu inayozungumziwa ni mawasiliano, barabara, maji na madaraja`,amesema.
Anasema hilo ni eneo la muhimu sana ,wao kama sekta binafsi wameona kuwa serikali inatakiwa kuiangalia kwa makini, anasema na kuongeza kuwa tayari chama hicho kilikwisha peleka mapendekezo hayo serikalini kabla ya kusomwa kwa bajeti.
Kitu kingine ambacho chama hicho kimeona kinastahili kupewa kipau mbele ni kwa serikali kupunguza utegemezi wa bajeti yake kutoka kwa wafadhili.Kwa sasa karibu asilimia 40 ya bajeti ya serikali inatoka kwa wafadhili kitu ambacho siyo kizuri kwa maendeleo ya nchi yetu.
Ili kuepukana na utegemezi huo, amependekeza serikali ianzishe vyanzo vingi vya kodi ambazo zitatumika kwa ajili ya maendeleo na kuachana na fedha za masharti.
`Inatakiwa tuanze kupunguza kwa taratibu utegemezi wa wafadhili kwani kwa kodi ambazo serikali inaweza kuzianzisha na zitatusaidia sana katika mambo yetu, anasema .
Kitu cha mwisho kuhusiana na bajeti ya mwaka huu amesema kuwa inatakiwa kuelekezwa katika kusaidia ujuzi wa elimu na rasilimali watu.
Accaro alisema kuwa elimu na kuendeleza rasilimali watu kunachangia kwa kiasi kikubwa uendelezaji wa uchumi wa nchi yeyote duniani, bajeti zaidi inatakiwa kuelekezwa huko kama tunataka kubadilisha uchumi wetu.
Hata hivyo alikuwa na matumaini na serikali kuwa itaongeza bajeti yake katika sekta hizo kwani zimefanyiwa utafiti wa kutosha na kuonekana kuwa kwa sasa ndio injini ya uchumi.
Kwa upande wake, Rais wa chama cha wakadiriaji majengo nchini(TIQS) Bw Joseph Tango Anasema kuwa chama chao kimekuwa kikitarajia kuwa bajeti ya mwaka huu itaangalia zaidi katika kodi ambazo zimo kwenye sekta ya ujenzi na umeme nchini.
Akitolea mfano amesema kuongezeka kwa bei ya saruji kunakotokana na sababu mbali mbali ikiwemo kodi kunasababisha watu kushindwa kujenga nyumba au hata madarasa.
Alisema bajeti inatakiwa kuangalia bei ya umeme ambayo imekuwa ikiongezeka mara kwa mara kwani imechangia sana kupandisha bei za bidhaa mbali mbali.
Kwa mujibu wa mkadiriaji huyo, sekta ya ujenzi inaajiri watu wengi na serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi kwa ajili yake.
Kuongeza kodi kwenye sekta ya umeme , mafuta au vifaa vya ujenzi kutarudisha nyuma juhudi za serikali za kuwawezsha wananchi wake, na kwenda kinyume na malengo ya serikali ya awamu ya nne.
Akizungumza awali,Bw Kiramuu Mbowe, mwalimu mkuu wa shule ya Sekondari Mbezi Beach amesisitiza kuwa bajeti ya mwaka huu inatakiwa kulenga sana katika sekta ya elimu.
`Tunatarajia kuwa serikali itatenga fedha nyingi sana katika sekta hii ambayo tunafikiri itasaidia sana katika kuendeleza uchumi wa nchi hapo baadaye`, amesema Bw Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha walimu wakuu wa shule za sekondari mkoani Dar es Salaam (Tahossa)
Alisema miaka michache iliyopita serikali ilijenga shule nyingi sana za sekondari ambazo kwa sasa zinakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo ukosefu wa wafanyakazi na vifaa.
Bajeti ya mwaka huu inatakiwa kuangalia namna ya kurekebisha shule hizo ambazo zilijengwa na serikali kwa ushirikiano na watu ili kuinua kiwango cha elimu.
Waziri wa Fedha, Bi. Zakia Meghji alipokuwa akielezea mwelekeo wa bajeti yake mapema mwezi huu, alisema matumizi katika bajeti ya mwaka huu yamepanda kutoka shilingi trilioni 4.85 za mwaka 2006/07 hadi trilioni 6.1 katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha.
Wahisani watagharimia asilimi 39 ya bajeti hiyo ambapo wachambuzi wa mambo wanasema ni kiasi kikubwa sana.
Hata hivyo watalaam wameshauri kwamba kuna haja ya kupanga bajeti ya taifa inayotumia dola za Marekani badala ya Shilingi ambayo inaanguka thamani na kuathiri bajeti kila mara , mhadhiri mwandamizi wa Chuo cha Ardhi na Usanifu wa Majengo (UCLAS) cha Dar es Salaam, Bw. Issa Mundeme amekaririwa akisema.
`Kila kitu tunaagiza kutoka nje Inabidi tununue dola ili tuagize, karatasi, mafuta, magari na vipuri. Matumizi yetu pamoja na bei yanabadilika kila siku kutegemeana na viwango vya dola,` alisema.
Bw. Mndeme ambaye pia ni mthamini wa ardhi na majengo anasema haamini kama kuna chochote katika bajeti ya hii kwa kile alichodai kuwa bajeti za wizara nyingi hazitoi picha halisi ya mahitaji ya taifa.
`Tunatengeneza bajeti ambayo ni ya kisiasa zaidi ili isije kukwama bungeni. Tunapeleka bajeti inayopita kwa urahisi yenye posho za viongozi, semina, safari lakini imeficha ukweli wa mahitaji sahihi ya wizara. Matokeo yake ni kuomba tena pesa pembeni,`alisema.
Hata hivyo watalaam wa masuala ya uchumi wanasema serikali haitafanya maajabu sana katika bajeti yake mwaka huu kama watu wengi wanavyofikiria kutokana na sababu mbali mbali zilizoipata nchi hii mwaka jana.
Wanasema mwaka jana Tanzania ilikabiliwa na majanga ya asili yaliyosababisha ukame, pia tatizo la umeme, ,kupanda kwa bei ya mafuta ya kuendeshea mitambo, ugonjwa wa homa ya bonde la ufa, mafuriko na upungufu wa chakula.
|