|
Bajeti imejitahidi kusikia malalamiko ya wananchi lakini
2007-06-15 08:40:27
Na Mhariri
Jana Waziri Zakia Meghji aliwasilisha bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2007/2008.
Hii ilikuwa ni mara yake ya pili kuwasilisha bajeti bungeni akiwa waziri wa wizara hiyo nyeti, na ikiwa ni bajeti ya pili ya serikali ya Awamu ya Nne, inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kumbumbu zetu zinaonyesha kuwa, hata bajeti iliyopita ya mwaka 2006/2007, ilikuwa ni bajeti iliyopongezwa na wengi, hata kama ilikuwa na mapungufu yake.
Kwa wale ambao hawakumbuki bajeti ile, magazeti kadhaa yalikuwa na vichwa vya habari kama `Bajeti ya Ari Mpya`, `Bajeti yauma na kupuliza sana`, `Bajeti ya Mama… Mishahara Juu` na mambo mengine yenye kuonyesha kwamba ilikuwa nzuri.
Hata kama kumetokea mapungufu katika kutekeleza bajeti hiyo iliyopita, lakini kwa ujumla wake ilionekana ni nzuri, kwa sababu hata majumbani mwetu, kupanga bajeti ni jambo moja na kuitekeleza ni jambo jingine.
Katika bajeti ya mwaka huu, kilichojitokeza ni kujitahidi kusikia kilio cha wananchi.
Wiki mbili tu kabla ya kusomwa kwa bajeti hiyo, mambo yaliyokuwa yakililiwa na wananchi, kama vile elimu, miundombinu, afya, kilimo, maji na ukali wa kodi ya mapato, yameangaliwa na bajeti hii.
Wengi walikuwa wakiona elimu ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa lolote, kwamba ilikuwa ikipata asilimia ndogo isiyoendana na unyeti wake.
Hata wakati huu tunaoendelea kujadili kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, hali ya uduni wa elimu yetu kulinganisha na wenzetu wa Kenya na Uganda, imekuwa ikijitokeza sana.
Hali kadhalika sekta za barabara, afya, kilimo na maji, kilio kimekuwa kile kile kwamba hazipewi kipaumbele cha kutosha kulinganisha na unyeti wake.
Kingine ambacho kimekuwa kikipigiwa kelele na wananchi na tunashukuru bajeti hii imekiona ni kodi ya mapato, hususan katika mambo kama mishahara na vyakula kuwa juu.
Tunashukuru kwamba bajeti hii imeliona hilo na kupunguza, hali ambayo itakuwa ni afueni kwa wafanyakazi na walaji.
Kingine ambacho tunaishukuru bajeti hii ni kuondoa
zabuni za serikali, ambazo inaaminika kuwa zilikuwa zikichangia mabenki kutoa riba kubwa sana kwa wakopaji.
Kwa mantiki hiyo, yapo sasa matumaini kwamba mabenki yetu yatapunguza riba, na hivyo wakopaji kupata faida.
Hata mgeni wa Rais Kikwete kutoka Bangladesh anayetembelea Tanzania, Profesa Yunus Mohamed, alishangaa sana kusikia mabenki yetu yanawatoza wajasiriamali riba ya kuanzia asilimia 20 na kuendelea.
Profesa huyo, mwanzilishi wa benki ya watu maskini nchini mwake na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya mwaka 2006, alisema kuwa wajasiriamali wa Tanzania hawawezi kujikwamua na lindi la umaskini (kwa kupata faida), endapo riba katika mabenki yetu haitakuwa chini ya asilimia 10.
Lakini pamoja na hayo yote mazuri, jambo moja ambalo linatuwangisha kichwa katika bajeti hii ni ongezeko la ushuru wa mafuta.
Mafuta, hususan petroli na dizeli vinapopanda vinasababisha kupanda kwa viti vingi, ikiwemo bidhaa za viwandani na usafiri.
Hata hivyo, tunaimani kwamba wabunge ambao mwanzoni mwa wiki ijayo, watakuwa wanaijadili kwa kina bajeti hii, wataifanya serikali iangalie upya jambo hilo, kwa kupanua wigo wa kodi katika maeneo mengine na kuachana na mafuta.
|