|
Stars ina nafasi kubwa ya kushinda leo
2007-06-16 10:19:40
Na Mhariri
Leo timu yetu ya taifa, Taifa Stars inajitupa Uwanjani kupambana na timu ya Burkina Fasso, jijini Ougoudogou.
Stars au `JK Boys` kama ambavyo wengine wanapenda kuwaita, wanacheza ugenini, ikiwa ni mechi ya marudiano, katika kutafuta tiketi ya kufuzu kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Bila shaka, kila Mtanzania na hata majirani zetu wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, wangepeda Stars ishinde mchezo huo mgumu.
Iwapo itashinda, timu yetu ya taifa itakuwa imefikisha pointi nane na kisha itahitaji ushindi katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Msumbiji ili iweze kufuzu kama mshindi wa kwanza katika kundi hilo.
Kwa kushinda mechi ya leo, bila kujali matokeo ya mechi yake na Msumbiji, inaweza kuwa pia ni sababu ya Stars kuweza kuwemo kwenye moja ya timu tatu zitakazoshika nafasi ya pili zikiwa na rekodi nzuri.
Katika kupata tiketi kupitia mshindi wa pili, Tanzania inachuana na Uganda, Sudan na Zambia ambazo kwa bahati mbaya kwetu zote zimeshafikisha zaidi ya pointi saba.
Hata hivyo, kinachotia moyo katika mchezo wa leo ni ari ya wachezaji waliyokuwa nayo, pamoja na kocha wao wakati wanaondoka nchini kwenda kuivaa timu ya Burkina Fasso, maarufu kama Stallions ya kuona wana kila sababu ya kushinda.
Na hasa kwa vile Stars waliifunga timu hiyo hapa Dar es Salaam, tuna imani kuwa watacheza kwa kujiamini zaidi, jambo ambalo ni muhimu sana katika kupata ushindi.
Wengi wanaweza kuwa na mashaka kutokana na mchezo wa kujipima nguvu baina ya Stars na Chipolopolo ambao, Stars walionekana wakifanya makosa machache, lakini ikumbukwe kwamba ulikuwa ni mchezo wa kirafiki tu, na pia ulitakiwa usisababishe majeruhi kwa upande wetu.
Kwa mantiki hiyo, hata kama wanacheza ugenini, bado tunaona kama nafasi kubwa ya ushindi ni yetu, kama wachezaji wetu watacheza `jihadi` na kuacha kujibweteka.
Kwa mantiki hiyo, kila Mtanzania mahala alipo awatakie mema na kuwapa kila morari vijana wetu hawa.
Tunawaomba Watanzania walioko nchini Burkina Fasso kwenda kwa ujumla wao kuwashangilia kwa nguvu zao zote vijana wetu ili wapate morari zaidi.
Na kwa wachezaji wenyewe tunarudia tena kuwaomba wasijibweteke kwa kudhani kwamba kwa vile waliishinda Burkina Fasso basi ni timu rahisi. Ukweli ni kinyume chake.
Pamoja na hayo, tunapenda kutahadharisha mapema kwamba katika mchezo, lolote linaweza kutokea.
Tunaweza tusipate ushindi, kama tunavyotarajia. Lakini hii isiwe sababu ya kuwabeza na kuwavunja moyo vijana wetu, hususan watakapokuwa wanarejea.
Tusije tukasahau kwamba, pamoja na mafanikio ambayo yameanza kuonekana, lakini timu yetu bado iko katika mchakato wa kusukuwa upya na kocha Marcio Maximo na kwa kweli amefanya kazi kubwa katika kipindi kifupi sana.
Inshallah Mwenyezi Mungu leo ataibariki timu yetu kuibuka na ushindi ugenini.
|