|
Bao 1 Stars = Mil. 322
2007-06-19 09:13:59
By Mwandishi Maalum, Dodoma
Ushindi wa bao 1-0 wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Jumamosi iliyopita dhidi ya Burkina Faso, umeipatia timu hiyo kiasi cha sh. milioni 322.5.
Pesa hizo zilipatikana jana baada ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuendesha harambee, ambapo wizara, watu na taasisi mbalimbali zilichangia ikiwa kama pongezi kwa ushindi huo.
Pesa hizo zimechangwa kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Burkina Faso katika mchezo uliofanyika Jumamosi katika kinyang’anyiro cha kusaka nafasi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Ghana mwakani.
Akitangaza matokeo ya harambee hiyo baada ya chakula cha mchana kilichoandaliwa kuipongeza timu hiyo, Waziri Mkuu alisema kama wakikaa na kupanga vizuri mambo yao wanaweza kufanya jambo kubwa kuliko kuzitumia katika starehe.
Naibu wa Waziri wa Michezo na Utamaduni wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo ambaye alikuwa kiongozi wa msafara alimweleza Waziri Mkuu azma ya vijana hao ya kutaka kuwekeza fedha zao ili wajengewe nyumba kupitia mifuko ya kijamii kama vile NSSF.
``Mheshimiwa Waziri Mkuu tukiwa njiani kutoka bungeni vijana wamejadili suala hilo na kuamua kuwa wakipata kama sh. milioni 200 watawekeza ili zitafutwe njia mahsusi za kuwasaidia wajenge nyumba…au hata kununua magari.``
Waziri Mkuu aliwashauri wawasiliane na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa Hifadhi ya Jamii, NSSF, Dk. Ramadhan Dau, ambaye pia alikuwepo katika hafla hiyo ili waangalie namna gani fedha zao zinaweza kutumika kwa manufaa zaidi.
Alisema bungeni wamepata sh. milioni 33 kutoka kwa wabunge wote, yeye (Waziri Mkuu) kapata milioni 47 kutoka kwa watu wanne tofauti, na Wizara ya Miundombinu imeahidi sh. milioni 70 ambayo jumla ilikuwa sh. milioni 150. Hivyo, aliwataka mawaziri waliokuwepo katika hafla hiyo fupi nao wachangie ili kuwasaidia vijana hao watimize azma yao.
Wa kwanza kuchangia alikuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge ambaye alisema wizara yake na taasisi zilizo chini yake wanaongeza sh. milioni 30. Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema wizara yake na makampuni yaliyo chini yake watatoa sh. 30.
Ahadi nyingine zilitolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Basili Mramba (sh. milioni 30); Waziri wa Kazi Ajira na Vijana, John Chiligati, (sh. milioni 10) na Waziri wa Nishati na Madini, Naziri Karamagi (sh. milioni 15). Pia aliahidi kutoa sh. milioni 15 kutoka kwenye makampuni yake binafsi.
Michango mingine ilitolewa na Mbunge wa Singida Mjini, Mohammed Dewji (sh. milioni 30); mmiliki wa Kampuni ya TIOT ambaye ametoa pesa taslimu sh. milioni 10 ambazo waliahidiwa kukabidhiwa mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam; na wakazi wa Dodoma walichanga pesa taslimu sh. milioni 2.5 ambazo kapteni wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa alizipokea kwa niaba ya wenzake kutoka kwa Waziri Mkuu.
Akizungumza mara baada ya harambee kukamilika, kocha wa timu hiyo, Marcio Maximo alimweleza Waziri Mkuu kwamba wachezaji wa Tanzania wanapokuwa uwanjani wanacheza na watu 22 badala ya watu 11.
``Kwa wenzetu kutoka nchi zilizoendelea, hawana wasiwasi wanapokuwa uwanjani kwa sababu wana uhakika na maisha yao na hivyo anapokuwa uwanjani akili inakuwa imetulia.
Lakini hawa vijana ambao leo hii tunawaita mashujaa, wanacheza na watu 11 huku wakiwa watu baki ambayo ni mawazo na matatizo kuhusu familia zao.``
``Waulize hawa hapa …wanapanda daladala kuja mazoezini, hawana hata magari, wengine hata vyumba vya kulala wanachangia na wenzao kwa sababu hawawezi kumudu kodi…,`` alisema huku akishangiliwa na wachezaji hao.
Alisema anawashukuru sana Watanzania wote kwa kuwatia moyo wachezaji wake na kwa mapokezi waliyoyapata tangu warejee nchini jana, na kuongeza kuwa ana imani kubwa na vijana wake.
|