21 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Walimu: Malimbikizo ya madai ni kikwazo cha elimu
 
2007-08-21 09:51:27
Na Moris Lyimo

Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kufafanua dhana ya elimu kuwa ni mchakato wa kuwawezesha binadamu kupata ujuzi na stadi muhimu kukabiliana na mazingira yake.

Kwa misingi hiyo, anasema mwalimu ni kioo cha jamii, mwandaaji wa taifa, chanzo cha maarifa na maadili, ubunifu, busara na mkuza mila na desturi.

Watu wengi wanahoji kulikoni mwalimu anakuwa mtu wa mwisho ingawaje ndiye mwandaaji wa taifa? Makala haya ya Mwandishi Moris Lyimo yaelezea zaidi.

Serikali katika kipindi cha 2007/08 imetenga kiasi cha shilingi trilioni 1 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu hapa nchini kutokana na kusuasua kwake licha ya kuwa ni nyanja muhimu na dira ya maendeleo ya taifa.

Mara kadhaa serikali imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali yenye lengo la kupata suluhisho la malalamiko mengi kwamba elimu inayotolewa haifai, haiwatayarishi vijana kwa maisha yao ya baadaye pamoja na walimu kuendelea kupuuzwa.

Kiasi cha trilioni 1 yumkini huweza kuwa suluhisho kwa kiasi fulani kwa kero hizo, ingawaje baadhi ya walimu wanasema si tegemeo kubwa kwao kwa kuwa mipango kama hiyo imekuwa ikiwekwa miongo kadhaa iliyopita wakati wa bajeti ya serikali kwenye sekta hiyo lakini hakuna mageuzi ya hali hiyo kuwa ya matumaini kwa waalimu walio wengi hasa vijijini.

Waalimu hawashirikishwi katika masuala ya mitaala, tathimini na sera, upangaji wa bajeti ya kitaifa, halimashauri za Wilaya na Manispaa na mambo mengine yanayohusu maendeleo yao ikiwemo kutopewa haki yao ya kuhoji, kujibu au kwa vyovyote vile ilimradi ni haki yake ya msingi kupata haki hizo.

Mwalimu wa siku nyingi Bw.Wambura Gaspar Maro anayefundisha shule ya Msingi Magomeni Lion katika Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam anasema hata wale wanaojaribu kudai haki zao hutishwa, huhamishwa vituo vya kazi, kutopandishwa madaraja, na kusimamishwa au kufukuzwa kazi kwa kusingiziwa makosa yasiyokuwa ya kweli.

Anasema lugha za matumaini na za kisiasa zisizokuwa na utekelezaji zimetawala zaidi huku waalimu wakiendelea kunyanyasika, kudharauliwa na kubezwa kwasababu ya kutojua haki zao.

Kwa matokeo hayo, ndiyo maana waalimu wanashindwa kudai haki zao kwa sababu ya hofu na hata kama watasaidiwa kwa kipindi fulani hudhani kuwa wamepewa ofa!.

Anasema tangu aanze kazi ya ualimu mwaka 1979 hajaona mabadiliko yenye heri kwa waalimu, ingawaje mabadiliko ya wastani yapo kwenye ujenzi wa madarasa, madawati na vifaa vya shule.

``Kujenga mdarasa mengi, si suluhisho kama mwalimu atakuwa na maisha ambayo hayamfanyi awe na moyo wa kufundisha.

Majengo mazuri yatakuwepo lakini kiwango cha elimu kitakuwa duni, je kuna maana gani ya kuwepo kwa majengo hayo?`` anahoji Mwalimu Wambura.

Anasema kazi ya ualimu hapa nchini haina thamani ukilinganisha na nchi nyingine duniani kutokana na ukweli kwamba serikali bado haijaweka mipango kamambe ya kuboresha maisha ya waalimu kwa maana ya kuwapa mishahara, na stahili nyingine kwa wakati bila usumbufu.

Hata pale ambapo serikali inawalipa madeni ya waalimu, waliopewa jukumu hilo hawafikishi kwa walengwa badala yake kutafuna fedha zao na kuishia kuwazungusha waalimu wanapodai, lakini hupewa vitisho mbalimbali na kuamua kusamehe madai husika.

Anasema mwalimu kama `kiwanda mama` cha mambo yote hapa nchini anastahili kutendewa haki na kuelimishwa juu ya haki zake kwa maana ya kupata watetezi, bila kutegemea kujua wajibu tu wa kazi zao bila kujua haki na namna ya kuzifuatilia.

Mwalimu Wambura anasema kwake yeye amebaini kuwa kushuka kwa elimu hapa nchini husababishwa na mambo mengi ikiwemo mitaala mibovu ya elimu isiyoeleweka miongoni mwa waalimu, hailengi elimu inayokusudiwa hapa nchini, na wala siyo mwalimu kutokuwa na taaluma.

Mambo mengine ni mipango mizuri isiyotekelezwa na ambayo haifai, mwalimu kutoshirikishwa kwa mambo mbalimbali yanayomhusu au kutoa maamuzi, kubadili muhtasari ya masomo mara kwa mara na kutowapeleka waalimu vyuoni ili kwenda na sambamba na badiliko hilo, kubadili vitabu vya kufundishia bila kujali muda na waajiri kutokaa na waalimu kujadili mikakati ya kazi.

Pia anaeleza kuwa kiwango cha elimu hushushwa na kutothaminiwa kwa waalimu wenye vipaji au mabingwa wa masomo na kuwashirikisha aidha kubadilisha mitaala au mihtasari kama inavyofanyika hivyo kwa waalimu wa shule za sekondari ambao pia hushirikishwa na Baraza la Mitihani kutunga mitihani.

Kukosekana kwa vifaa mashuleni na kutotosha vilivyopo licha ya kuwepo kwa mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) ambao ulipunguza tatizo na siyo kumaliza tatizo kutokana na matumizi mabaya ya fedha hizo miongoni mwa waliopewa jukumu hilo wakiwemo waalimu wakuu wa shule.

Mambo mengine ni waalimu kutokuwa na Ikama nzuri mashuleni, na kutokuwa na uwiano wa idadi ya waalimu na wanafunzi mashuleni, mishahara midogo na kutokuwa na marupurupu, kutohamishwa kwenye shule (vituo vya kazi) kwa waalimu waliokaa kituoni muda mrefu na kuzoeleka kwa jamii hivyo kuifanya shule kuwa mali yake.

Yapo pia matatizo kama kutofanyika kwa ukaguzi wa shuleni mara kwa mara ili kubaini makosa na kuyarekebisha kwa wakati muafaka.

Utafiti uliowahi kufanywa na shirika la Haki Elimu kwa kushirikiana na Chama cha Waalimu (CWT) (tafiti namba 2) juu ya ubora wa mazingira ya ufundishaji na ufundishwaji mashuleni ulionyesha kwamba mazingira yasiyoridhisha kwa kufundishia na kusomea ni chanzo kikubwa cha kuporomoka kwa kiwango cha elimu hapa nchini.

Utafiti huo ulioongozwa na Profesa Suleiman Sumra na Prof.Verdiana Grace Masanja pia ulibainisha kwamba waalimu ambao wanayo kazi kubwa ya kumuendeleza mtoto, wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu.

Miongoni mwa mambo hayo, Prof.Verdiana anasema katika utafiti huo kuwa ni waalimu kutopatiwa haki zao kama inavyofanyika kwa watumishi wengine wa umma pamoja na umuhimu wa mwalimu katika maendeleo ya nchi.

Haki hizo ni pamoja na kutokuwa na makazi (nyumba) karibu na vituo vyao vya kazi au zenye hali mbaya sana kwa baadhi ya maeneo yenye nyumba hizo.

Mratibu wa Chama cha Kutetea haki za Watoto nchini (CHAKUHAWA)Bw.Kelvin Shola anasema matatizo yanayozikumba waalimu wa shule za msingi yapo pia katika shule za awali.

Ingawa shule za awali ni kitegauchumi kinachoinua pato la waalimu wa shule hizo, lakini mazingira ya waalimu wa shule hizo ni magumu, kutokana na kupuuzwa kwa elimu hiyo wakati kimsingi ndiyo elimu ya kwanza kabla ya msingi, sekondari na mwishowe vyuo, na ndiyo kusema kimsingi `elimu ya awali ndiyo elimu ya msingi` .

Anasema waalimu hao, hupuuzwa, hudharauliwa hata pale ambapo kazi yao ni muhimu kwa jamii na taifa kwa ujumla. Wengi wao wanakosa ajira serikali na kusababisha kuwepo kwa utitiri wa vituo vya kulelea watoto wadogo na shule za awali zinazoendeshwa na watu binafsi.

``Kutokana na mapungufu haya, elimu hii inaendeshwa bila kufuata misingi ya elimu kutokana na ukweli kwamba sekta hiyo imevamiwa na watu wanaojiita waalimu bila kuwa na taaluma husika,``anasema.

Anasema wengi wao ama wanaziendesha bila kupata mafunzo au kwa kiwango kidogo cha elimu jambo ambalo ni hatari hasa kwasababu walengwa ni watoto ambao ni wepesi kupotoshwa.

Bw. Shola ambaye ni mwalimu kitaaluma anasema kutokana na kasoro hiyo, pia shule hizo huendeshwa kwa mfumo ambao si rasmi kwa kutokuwepo kwa uongozi na mfumo mzuri wa andalio la somo, hivyo watoto kutokuwa na maendeleo yoyote ya uelewa hali ambayo huwafanya wazazi wasiwe na imani na waalimu hao na kuzidi kushusha hadhi ya sekta hiyo.

Badala yake, amewataka waalimu wa shule hizo wajiendeleze na wale wasiokuwa na taaluma hiyo kwenda kupata mafunzo angalau ya muda mfupi.

Anasema watoto wanapashwa kupata elimu sahihi ikiwa ni hatua ya kuwajengea msingi wa uelewa mzuri watakapoanza elimu ya msingi, sekondari na hatimaye vyuo vikuu.

Juu ya ukosefu wa vifaa na matumizi ya mitaala ya kigeni katika shule za awali, Bw Shola anawakata wenye shule hizo kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo ili kujenga imani ya wazazi juu ya vituo vya elimu ya awali.

Mwenyekiti wa Muungano wa mashirika nane ya kimataifa ya haki za walemavu duniani ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa Kisheria na Uchumi kwa Walemavu (DOLASED) Dk.Gideon Mandesi, anasema walemavu wa Tanzania wanakabiliwa na matatizo mengi likiwemo ukosefu wa elimu.

Ili kutokomeza matatizo ya walemavu, Tanzania imejumuika na nchi nyingine 34 duniani kusaini mkataba wa kimataifa wa Haki za Walemavu wenye lengo la kusaidia walemavu kushiriki kikamilifu katika nyanja zote za maisha, kusikika na kupata fursa sawa kwa watu wote wenye ulemavu.

``Pia unalenga kupambana na udhalimu dhidi ya walemavu, kwa mfano kudhalilishwa kwa kubakwa na kulawitiwa jambo ambalo limekuwa likiwapata walemavu kwa kukosa misingi ya maelewano katika jamii, kwa mfano viziwi, kwa jamii hiyo kutopata elimu ya lugha inayotumika kuwaunganisha,``anasema Dk.Mandesi.

Anasema kupitishwa kwa kusainiwa kwa mkataba huo kutakuwa ni mapinduzi ya kuangalia walemavu kama suala la haki za binadamu na kuhakikisha kanuni za kutathimini utu, usawa na kutobagua.

Mambo yanayopewa kipaumbele katika mkataba huo ni pamoja na kukataza ubaguzi dhidi ya walemavu katika nyanya zote za maisha, kuweka bayana haki zote za binadamu kwa kuzingatia ulemavu, ushirikishwaji na kujumuishwa jamii ya walemavu katika ajenda za maendeleo ya kijamii.

Dokta Mandesi anasema mkataba huo unaelekeza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) kuchukua hatua za kisheria na za kiutawala kuhakikisha kwamba walemavu wanapata haki za msingi za binadamu na uhuru.

``Nchi hizo pia zinaelekezwa na mkataba huo, kuyaweka wazi masuala ya haki za walemavu katika katiba ya nchi, sheria na sera za kimataifa.

Maana yake ni kwamba masuala yote ya maendeleo, haki na sheria lazima ziwahusishwe walemavu hasa katika utungwaji wa sheria na uundwaji wa sera,``anasema.

Kupitishwa na hatimaye kusainiwa kwa mkataba huo, anasema huenda ikawa faraja kwa walemavu nchini ambao wengi wao wamekosa matumaini kutokana na kunyimwa haki zao za msingi, kwa kubaguliwa na namna nyingi zinazowafanya wakose haki zao kama vile kubaguliwa wakati wa utoaji wa ajira na elimu.

Meneja wa programu ya Utengamao wa jamii wa shirika la CCBRT la Jijini Dar es Salaam Bw.Arboast Kajuna anasema ni asilimia moja hadi mbili tu ya watoto wenye ulemavu katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania wanaobahatika kupelekwa shule.

Hali hiyo anasema, imezifanya jamii za walemavu kurudi nyuma kimaendeleo, kupuuzwa katika jamii na wakati mwingine watoto wengine huwacheka na kuwatenga hali inayowafanya kukosa ujasiri wawapo darasani.

Aidha, Mkurugenzi wa Mtandao wa Watoto, Vijana na Wanawake (CHIYOWONET) Bw. Jackson Millengo aliishauri serikali kujenga mazingira mazuri ya elimu kwa watoto na waalimu wao ili kupata viongozi wazuri wa baadaye.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.