|
Uvutaji bangi humfanya mwanamke kuzaa mtoto taahira
2007-08-22 08:28:52
Na JACQUELINE MOSHA
Zaidi ya watu Milioni 1.6 wameripotiwa kutumia bangi duniani kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2003 mpaka 2005 ambapo umri unaoathirika zaidi umetajwa kuwa ni kuanzia miaka 15 mpaka 64.
Hili ni tatizo kubwa hasa ikizingatiwa kuwa vijana wanaotumia kilevi hicho au kileta njozi, wanahitajika zaidi katika kusaidia uwajibikaji na kujenga nchi kwa kufanya kazi.
`Nilijisikia kama kichaa, kila kitu kilionekana cha ajabu, sikuweza kuongea na akili yangu ilikuwa inaelea, nilifikiri na kuona mambo ya ajabu, kama kusikia muziki tofauti, nilipata hisia zisizoelezeka,` anasema mtumiaji mmoja wa bangi.
Bangi ni mmea wenye rangi ya kijani, ambao hutoa majani, maua na mbegu ambavyo hutumika kama kilevi. Mmea huu husitawi karibu katika maeneo yote hapa nchini Tanzania na hutumika zaidi kuliko dawa nyingine za kulevya.
Bangi inaripotiwa kupatikana kwa wingi katika mikoa ya Mara, Iringa, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Tabora, Tanga, Kagera na Mbeya.
Pia bangi huweza kupatikana kwa sura tofauti ikiwemo katika mfumo wa mafuta, bangi kavu na iliyosindikwa.
Yapo majina mbalimbali yanayotumika huko mitaani yakimaanisha bangi.
Mitaani bangi hujulikana kwa majina kama msuba, ganja, daga, jani, stiki, ndumu, kaya, msokoto na mengineyo.
Bangi imo katika kundi la dawa ambazo ni vileta njozi (Hallucinogens), na katika kundi hilo pia kuna dawa zingine zenye aina fulani ya uyoga.
Dk. Hussein Mtiro anasema kuwa, uvutaji wa bangi humfanya mvutaji kubakiza moshi mwingi kwenye mapafu kwa muda mrefu na kwamba moshi huo unapoingia kwenye mapafu hutengeneza kitu kama lami ambayo huganda na kuathiri utendaji kazi wa mapafu.
Mtaalamu huyo anasema kuwa, uvutaji huo wa bangi huchangia mvutaji kupata kemikali zenye sumu inayosababisha saratani zaidi hata ya tumbaku (Sigara).
Saratani za koo, mapafu ndizo zinazowakabili kwa kiwango kikubwa watumiaji wa bangi.
Dk. Mtiro, anasema kuwa, bangi huleta madhara mengi kwenye mfumo wa fahamu. Bangi (Vileta njozi) huathiri ubongo na kumfanya mtumiaji kutoa tafsiri potofu ya hisia na kujisikia kama vile yupo nje ya dunia hii. Hisia huwa na nguvu zaidi.
`Muda mfupi baada ya kutumia ambayo ni matumizi kwa kiwango kidogo husababisha mtumiaji kuzubaa, kuhisi furaha kuliko kawaida, kuongezeka kwa hamu ya kula.
Kadhalika, matumizi kwa kiwango kikubwa husababisha mtu kuwa kichaa, kutapika, wasiwasi, kuwa na hamaki, kupumbaa, kutetemeka kwa nguvu kama kifafa, kuzimia na kupatwa na shinikizo la damu,` anasema Dk. Mtiro.
Aidha mtaalamu huyo, alikumbusha kuwa, matumizi ya muda mrefu husababisha mtumiaji kupata ugonjwa wa akili, mabadiliko ya maono, hisia na mtizamo usiyoisha, kuharibika kwa ubongo na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kukumbuka na kufikiri, kukosa ari ya maendeleo na mabadiliko ya ina yoyote ile.
Usugu na utegemezi kwa mtumiaji wa bangi uwezekano huwa wa wastani lakini kwa vileta njozi vingine uwezekano huwa mkubwa.
Madhara ya kuacha ghafla kwa matumizi ya bangi hakuna dalili za wazi isipokuwa mtu huwa na msononeko tofauti na vileta njozi vingine ambapo athari zake hujirudia kwa maluweluwe hata bila kutumia vileta njozi, msononeko pia huwepo.
Yapo madhara yatokanayo na uvutaji wa bangi yakiwamo ya kuumwa koo na kupata kikohozi na saratani ya mapafu, kuathirika kwa mfumo wa uzazi ikiwa ni pamoja na kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo na mabadiliko ya hedhi kwa wanawake.
Madhara mengine ni mvutaji kuchanganyikiwa, kuwa na tabia za ukatili, ukorofi, uhalifu na nyingine mbaya zinazofanana na hizi.
Tatizo lingine ni lile la kupunguza kinga ya mwili, kupoteza kumbukumbu.
Mvutaji pia hupata hisia, kusikia na hata kuona vitu visivyokuwepo kabisa katika sehemu aliyopo kwa wakati huo anapovuta.
Utegemezi na usugu, macho kuwa mekundu, na wakati mwingine mtumiaji wa bangi kuridhika na hali duni ya maisha aliyonayo hivyo kukosa mwamko wa maendeleo huku akijihisi ni mwenye mafanikio makubwa.
Kwa mwanamke mjamzito anayetumia bangi zipo athari kubwa na za hatari zitakazomkabili ambazo ni kuharibika kwa mimba, kuzaa mtoto njiti na hata kuzaa mtoto mwenye mtindio wa ubongo na matatizo ya ukuaji.
Zipo imani na hisia potofu kuhusu uvutaji wa bangi kwamba huongeza uwezo wa kusoma na kuelewa zaidi, jambo linalokanushwa na Dk. Mtiro na kutanabaisha kwamba badala yake bangi hufanya mishipa ya ubongo kusinyaa na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiria na kukumbuka.
Aidha utafiti umebainisha kuwa wanafunzi waliovuta bangi kwa matarajio ya kujiongezea uwezo wa kusoma vizuri katika masomo yao darasani waliishia kufeli vibaya.
Njia nyingi zimebainishwa za jinsi ya kumfanya mtu kujiepusha na utumiaji wa bangi na kati ya hizo ni kujiepusha na makundi ya watumiaji wa bangi, kushiriki kwenye michezo na kujifunza stadi za maisha.
Lakini Bw. January Ntisi anasema kuwa, sheria za nchi zinasisitiza kuwa, kutumia, kuuza, kusafirisha, kuhifadhi au kujihusisha kwa namna yoyote ile na bangi ni kosa la jinai na adhabu kwa makosa hayo hufikia hadi kifungo cha maisha.
`Endapo tayari mtu ameshaanza kutumia bangi ni vyema akaenda kwenye kituo cha afya au cha ushauri nasaha kilichopo karibu kwa ushauri zaidi. Na kama bado mtu hujaanza kutumia bangi jiepushe na mambo yatakayokushawishi,` alisema.
Ofisa huyo anaeleza kuwa vijana wengi wameshaathirika sana na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi na kwamba Tume ya kudhibiti madawa ya kulevya inajitahidi kwa hali yoyote ile ili kusaidia kuwaondoa mtegoni walioanza kutumia dawa hizo na kuepusha watumiaji wapya kuongezeka.
`Vijana wengi wanaotumia dawa hizi huwa ni vigumu sana kwao kuacha kabisa kutumia kwakuwa kati ya asilimia 100 ya watumiaji waliokwisha athirika na dawa hizo, basi asilimia 5 tu ndio labda wanaweza kuacha kabisa kutumia baada ya kupatiwa tiba toka hospitalini na kupewa ushauri nasaha,` alisisitiza Bw. Ntisi.
Lakini Bw. Ntisi anasema idadi hiyo ya asilimia 5 kwa wanaokisiwa kuweza kuachana na matumizi ya dawa hizo ni ndogo sana ukilinganisha na asilimia 100 ya watumiaji wote, hivyo juhudi za dhati zinatakiwa kufanywa kwa kushirikisha jamii na Tume hiyo ili kuepusha janga lisizidi.
`Tatizo linalochangia kuongezeka kwa matumizi haya ni kwamba mtu aliyezowea kutumia dawa za kulevya hushindwa kuishi bila ya kuzitumia, anapokuwa hana hela , atatumia njia yoyote ikiwemo wizi, uporaji na vitendo vingine vya kihuni ili tu apate pesa kidogo ya kununulia dawa hizo ili ajitibu,` alibainisha Bw. Ntisi.
Aidha Bw. Ntisi amesema kulikuwa na jumla ya watu 162,400,000 ambao ni sawa na asilimia 3.9 ya watumiaji wote wa bangi duniani ambapo idadi ni kuanzia mwaka 2003 mpaka 2005, huku takwimu zilionyesha kuwa bara la Ulaya kulikuwa na idadi ya watumiaji bangi 30,800,000 sawa na asilimia 5.6.
Sambamba na hilo, takwimu zingine zinazojumuisha kiwango hicho ni kutoka Ulaya Magharibi na Kati (23,400,000 sawa 7.4%), Kusini Mashariki (1,900,000 sawa 2.3%), Ulaya Mashariki (5,500,000 sawa 3.8%), Bara la Amerika (36,700,000 sawa na asilimia 6.4, Amerika ya Kaskazini (kulikuwa na watumiaji 29,400,000 ambao ni sawa na sawa 10.3%, wakati Amerika ya Kusini 7,300,000 sawa 2.6%.
Nyingine ni za kutoka Bara la Asia watu waliokuwa wanatumia walikuwa 52,100,000 sawa 2.1%, Australia na New Zealand 3,200,000 sawa 15.3%, kwa upande wa Afrika kulikuwa na watu 39,600,000 ambao ni sawa na asilimia 8.1.
|