23 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Bunge kuongeza muda wa vikao ni hatua nzuri endapo...
 
2007-08-23 10:35:52
Na Mhariri

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeongeza muda wa vikao vyake ikiwa ni miongoni mwa kanuni mpya za Bunge zilizofanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya sasa ya Bunge hilo.

Spika wa Bunge, Bw. Samwel Sitta alikaririwa juzi akisema kuwa Bunge lijalo la Bajeti litakutana kwa siku 50 ikilinganishwa na siku 35 za sasa na mikutano ya miezi ya Oktoba, Januari na Aprili sasa itafanyika kwa wiki tatu badala ya wiki mbili.

Sisi tunaipongeza hatua hii kwani tunaamini kwamba itatoa nafasi kubwa zaidi kwa wabunge katika kuchambua masuala mbali mbali ya taifa letu.

Tunaamini kwamba muda huo utasaidia kuwafanya mawaziri kutoa majibu ya ufasaha na yanayojitosheleza na wabunge kuuliza maswali yenye manufaa kwa taifa kwa ‘kujinafasi’ zaidi.

Pengine muda huu utatumiwa pia kuwafanya mawazi kusoma hotuba zao za bajeti kwa vituo pale wanapoziwasilisha, badala ya hali ya sasa ambayo tumekuwa tukiwasikia wakisoma haraka haraka sana ili kukimbizana na muda.

Hali kadhalika kuongezwa kwa muda tunaamini kwamba sasa kutasaidia kutomfanya Spika ama naibu wake kuwataka mawaziri kujibu maswali kwa ufupi wakati maswali yanayoulizwa bungeni ni masuala nyeti na muhimu katika taifa letu ambayo hayana sababu ya kujibiwa kwa ufupi ili kukimbizana na muda.

Pia muda huo tunaamini utatumiwa pia na wabunge kuulizwa maswali ama kujadili mambo ya taifa letu kwa nafasi, badala ya kukatizwa katizwa eti kwa sababu ya kufukuzana na muda.

Siyo kwamba tunashauri kusiwe na muda maalum wa wabunge kuongea, lakini tunadhani kwamba muda huo nao utaongezwa baada ya siku za Bunge kuongezwa.

Hata hivyo, kuongeza siku za Bunge ina maana pia kuwatwisha mzigo zaidi walipa kodi wa nchi hii kwani pesa zao ambao zingeweza kutumika, tuseme kwa kuwajengea barabara, zinaenda kulipa posho za wabunge.

Kwa mantiki hiyo, tunatazamia wabunge wetu kufanya kile walichotumwa na wananchi wanaowawakilisha kwa manufaa ya taifa letu na si vinginevyo. Mambo hayo ni pamoja na kuihoji serikali, kuishauri na kuisaidia kutupatia maisha bora na kututungia sheria zenye manufaa kwetu.

Tunajua si rahisi kukwepa wabunge kuwa na misimamo fulani fulani kutokana na itikadi ama sera za vyama vyao. Lakini taratibu tunaanza kuwa na wasiwasi kwamba Bunge letu linaonyesha dalili ya kuingiliwa na siasa za makundi.

Tuna hofu kwamba kama hali hii itaendelea, mijadala katika Bunge inaweza kuwa ya kulinda maslahi ya makundi fulani na si ya taifa na hivyo kufanya muda ulioongezwa usiwe na manufaa tunayoitarajia isipokuwa hasara.

Lakini kwa vile wabunge wetu wanaelewa dhamana kubwa walio nayo na umuhimu wa kutuwakilisha katika chombo hicho muhimu, bila shaka watatumia muda ulioongezwa vyema kwa maslahi ya taifa letu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.