24 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Athari ya serikali kuondoa amana kwa mabenki
 
2007-08-24 09:08:31
Na Felix Andrew

Hivi karibuni serikali ilitangaza bungeni nia yake ya kufunga akaunti zake zote zilizopo kwenye taasisi za kifedha nchini na kuzihamishia benki kuu (BoT).

Inawezekana uamuzi huo ukawa na matokeo mazuri kwa upande wa serikali lakini kwa upande mwingine utaathiri sana sekta ya kifedha ambayo ndiyo inategemea fedha hizo kukopesha watu au makampuni kwa ajili ya kuendeleza uchumi.

Inasemekana kuwa asilimia 25 ya fedha za serikali zipatazo zaidi ya shilingi trilioni moja zipo kwenye mabenki hayo na zinatumika kukopesha wananchi.

Endapo akaunti hizo zitafungwa ina maana kuwa mabenki yatapunguza kasi ya kukopesha na kuchochea ongezeko la riba inayotozwa kwa wakopaji.

Watalaam wa masuala ya kiuchumi wanaonya kuwa endapo serikali itashikilia msimamo wake basi unaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji uchumi wa nchi hii.

Akizungumza kwenye sherehe za ufunguzi wa tawi la Vijana la benki ya CRDB, Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo Dk. Charles Kimei, amesema uamuzi huo utaathiri sana sekta nzima ya kifedha.

Anasema mtiririko wa fedha kwenye uchumi wowote unaohusisha sekta zote tatu zinazotegemeana kupitia sekta ya mabenki yaani sekta ya mtu mmoja mmoja( households), sekta ya makampuni na sekta ya serikali.

Nakisi kwenye sekta mojawapo inazibwa na ziada kwenye sekta nyingine na hivyo kufanya sekta zote kwa pamoja kuwe kwenye uwiano.

Kuondoa sekta ya serikali kwenye mtiririko wa fedha kutapunguza mtiririko wa fedha na ukwasi kwa ujumla kwenye uchumi.

Anafafanua uamuzi huo utakuwa na athari kubwa kwani fedha za kukopesha zitapungua kwenye mabenki basi riba za kukopesha kile kidogo kitakachokuwepo zitaongezeka.

Mkurugenzi huyo anasema si kweli kuwa kitendo hicho kitashusha riba na kuchochea uwekezaji kama baadhi ya watu wanavyosema.

Kama kwa kufanya hivyo serikali itaopunguza au kusimamisha kabisa mauzo ya dhamana zake kwenye mnada basi soko hili la dhamana za serikali ambalo limelelewa kwa muda mrefu litakufa.

Licha ya sera ya hapo awali ya kulilea na kuliendeleza ili kusaidia sekta ya kifedha kuweza kusimamia ukwasi kwenye uchumi kwa kutambua ufinyu wa soko la kifedha hapa nchini.

Kama soko lisipokufa na serikali ikaendelea kuuza dhamana basi riba kwa dhamana hizo si lazima zipungue kwa vile kila mnaanda unakabiliwa na soko lenye ukwasi mdogo.

Fedha za miradi mbali mbali ya serikali zikikaa Benki kuu hazitatumiwa na serikali kwa shughuli yeyote nyinghine licha ya miradi husika na hivyo hazitasaidia uchumi katika kipindi cha utekelezaji wa miradi.

Fedha hizo zikikaa kwenye mabenki ya biashara zinaingia kwenye mtirirko na kuzisaidia benki kutoa mikopo kwa wateja wengine mbali mbali kwa vile mabenki yana uwezo wa kufanya kile kinachoitwa maturity transformation au kubadili fedha za muda mfupi kutumika kwa mura mrefu .

Kama nia ya serikali ni kukuza uchumi basi ione jambo la kuwa na akaunti hizo kwenye mabenki ya biashara kama njia mojawapo ya kuwawezesha wawekezaji.

Ukusanyaji wa kodi unapitia kwenye mabenki kwa vile walipa kodi ni wateja wa mabenki, sehemu kubwa ya kodi hasa za mapato zinalipwa mwisho wa robo mwaka.

Hii ndiyo sababu fedha za serikali zinazowasilishwa na mabenki kwenye benki kuu zinaongezeka sana mwishoni mwa robo mwaka.

`Si kweli kwamba mabenki yanahifadhi fedha za serikali kwa muda mrefu bila kuziwasilisha benki kuu`, anasema Kimei.
Hata hivyo katika kujihami na changamoto mbali mbali , benki hiyo sasa inajiandaa kuorodhesha hisa zake kwenye soko la Hisa la Dar es Saaaam (DSE).

Hiii ni katika kuhakikisha kuwa shughuli za benki zinakuwa endelevu zaidi zinaendeshwa kwa uwazi na pia kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki hisa za benki na hivyo kufaidi gawio linalotokana na faida inayopatikana mwaka hadi mwaka.

Ili kampuni ikubaliwe kujiunga na soko la hisa, vigezo vinavyozingatiwa sana ni pamoja na kampuni husika kuwa na historia ya ufanisi mzuri pamoja na kupata faida .

Kampuni lazima iwe na menejimenti nzuri na yenye uzoefu wa kutoa gawio kwa wanahisa.

Akiwasilisha Bungeni taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2006 na mwelekeo wa muda wa kati 2007/08 na 2009/10 ,mwezi Juni mwaka huu, Waziri wa Mipango Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa amesema katika mwaka 2005/06, benki za biashara ziliendelea kutoa mikopo kwa sekta binafsi.

Mikopo iliyotolewa na benki za biashara katika mwaka 2005/06 ilikuwa shs. 1,656,837.8, sawa na ongezeko la asilia 35.9 ikilinganishwa na sh. 1,219,305.6 zilizotolewa mwaka 2004/05.

Hadi Desemba 2006 mikopo kwa sekta binafsi ilifikia sh. 2,027,196.3 milioni ikilinganishwa na sh. 1,425,062.3 milioni Desemba 2005, sawa na ongezeko la asilimia 42.3.

Sekta zilizopata viwango vikubwa vya mikopo ni ujenzi na majengo, uzalishaji, kilimo, usafirishaji, madini, viwanda na biashara nyingine.

Katika mwaka 2005/06, wastani wa riba zilizotolewa na benki za biashara kwa amana za akiba ulishuka kutoka asilimia 2.61 Juni 2005 hadi asilimia 2.54 Juni 2006, na ilipofika Desemba 2006, wastani wa riba hizo uliongezeka na kufikia asilimia 2.59.

Wastani wa riba iliyotozwa na benki za kibiashara kwa mikopo ulishuka kutoka asilimia 15.51 Juni 2005 hadi asilimia 15.44 Juni 2006 na kuongezeka hadi asilimia 16.43 Desemba 2006.

Ingawa ushindani baina ya benki za biashara umeongezeka, mwenendo wa riba katika benki hizo unaonyesha kuwa bado kuna tofauti kubwa kati ya riba za amana na za mikopo.

Tofauti hiyo ilikuwa asilimia 9.6 Juni 2006 ikilinganishwa na asilimia 10.7 Juni 2005, na kufikia asilimia 10.3 ilipofika Desemba 2006.

Aidha, tofauti hiyo ya riba kuendelea kuwa kubwa kiasi hicho, ni kiashiria kuwa bado gharama ya kukopa katika benki za biashara ni kubwa.

Dk Ngasongwa anasema serikali, kwa kupitia awamu ya pili ya Maboresho na Mageuzi katika Sekta ya Fedha, inashughulikia tatizo hilo ili kupunguza totauti hiyo, hivyo kuwawezesha wananchi wengi zaidi waweze kukopa kwa gharama nafuu zaidi kwa ajili ya kujiendeleza na kupunguza umaskini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha uamuzi huo utapunguza gharama zisizo za lazima zilizotokana na utanzaji wa fedha hizo.

Pia utaleta ushindani zaidi wa kibiashara miongoni mwa mabenki na hivyo kuongeza uwezekano wa kupunguza riba kwa wateja.

Itabidi mabenki sasa yaangalie uwezekano wa kuongeza wigo wa mikopo na kutoa vivutio vya aina mbali mbali ili kuweza kuwa na wateja wengi. Mojawapo ya kivutio ni kupunguza riba.

Endapo uamuzi huo, mipango yote ya maendeleo inayokusudiwa kufanywa na serikali hasa kwenye sekta ya fedha huenda ikakwama, ni matumaini kuwa serikali inaweza kubadilisha uamuzi wake.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.