24 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Yosso wa Uganda si lolote kuipima Stars
 
2007-08-24 09:09:36
Na Mhariri

Chama cha soka cha Uganda (FUFA) kimeamua kuleta timu ya taifa ya vijana wadogo kwa mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars itakaofanyika Septemba 1 kwenye uwanja mpya wa Taifa.

Gazeti hili lilikariri tovuti ya gazeti la The Monitor la Uganda ikidai kuwa FUFA imeamua kuileta timu ya yosso ili kuipa majaribio Taifa Stars!

Mchezo huo utakuwa maalumu kwa ajili ya kuipima Stars inayojiandaa kuikabili Msumbiji kwenye mechi muhimu ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakayochezwa Septemba 8 kwenye uwanja mpya wa michezo jijini Dar es Salaam.

Stars inatakiwa kuifunga Msumbiji katika mchezo huo wa Kundi la saba wakati ikiomba Senegal isiifunge Burkina Fasso mjini Dakar kutokana na timu hizo kufungana pointi.

Kutokana na ugumu wa mchezo dhidi ya Msumbiji, ni kitendo cha kusikitisha kuona kuwa timu itakayokuja kuipima nguvu Stars inaundwa na yosso watupu.

Kikosi cha The Cranes kitakuwa na wazoefu wanne tu lakini watakaobakia watakuwa ni yosso tupu.

Ni wazi kwamba maandalizi ya mchezo wetu na Msumbiji yanaonekana kuingia dosari kutokana na ukweli kwamba Stars ilikuwa inahitaji mechi ngumu kabla ya kuivaa Msumbiji ili kuweza kupima kiwango cha timu yetu na kurekebisha makosa muhimu.

Tunafikiri kuwa mazoezi ya siku 18 barani Ulaya bila shaka yanamfanya Kocha Marcio Maximo kuhitaji mechi ngumu kwa ajili ya kuipima Stars.

Msumbiji walicheza na Zimbabwe, Jumanne iliyopita
na kutoka sare ya 1-1 ikiwa sehemu ya maandalizi kabla ya kuivaa Stars.

Stars baada ya mazoezi ya Ulaya ilikuwa inahitaji kucheza mechi na timu moja ngumu ya Afrika ili kuona kiwango chake na kurekebisha makosa muhimu yatakayojitokeza.

Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa soka ya Ulaya, tofauti na la Afrika hutegemea nguvu zaidi na fomesheni wakati Soka ya Afrika hutegemea zaidi vipaji vya wachezaji binafsi na fomesheni linakuwa jambo la pili.

Mazingira ya sasa ni sawa na wakati Stars ilipotoka Brazil, ambapo ilikwenda Senegal moja kwa moja na kufungwa 4-0, jijini Dakar, Senegal mwezi Machi mwaka huu, ambapo wadau wengi waliamini kipigo hicho kilichangiwa na timu hiyo kutocheza na timu angalau hata moja ya Afrika.

Cha kusikitisha zaidi ni kuwa Uganda wameamua kuleta timu ya yosso wakati TFF imeingia gharama za kuileta timu hiyo zinazofikia Dola za Marekani 15,000.

Ndio maana TFF inatakiwa kuwa makini katika siku zijazo inapoalika timu za kigeni kuja kucheza mechi nchini kwa kuhakikisha inaagizia timu kali zaidi kwa ajili ya kujipima nguvu.

Kwa vile muda uliobaki pia ni mchache tunaomba kamati inayohusika na maandalizi kuweza kubaini kasoro nyinginezo ambazo zinaweza kusababisha kipigo kwenye mechi yetu na Msumbiji.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.