|
Mazingira ya utumishi wa wafanyakazi sekta ya afya yaboreshwe
2007-08-25 09:40:12
Na Jackson Kalindimya
Maisha na mazingira ya wafanyakazi wengi wa sekta ya afya hayaridhishi na kufikia hatua ya kuwakatisha tamaa au kushusha morali yao ya kazi.
Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari vya mikoani (UTPC) umefanya uchunguzi katika mikoa minane nchini ili kujaribu kupata sababu. Makala hii ya Mwandishi Wetu, Jackson Kalindimya yachambua uchunguzi huo.
``Wafanyakazi wa sekta ya afya nchini, karibu wote wamevunjika moyo, morali yao ya kazi kushuka kutokana na kufanya kazi katika mazingira magumu na kwa muda mrefu, upungufu wa wafanyakazi, mishahara midogo kulingana na gharama za maisha, hawalipwi marupurupu na wanaolipwa yanachelewa sana kuwafikia “ alisema Bw Abubakar Karsan.
Kwa wafanyakazi walio tayari kufanya kazi vijijini, wanasema wanatumia muda wao mwingi kufanya biashara au kazi zingine ili wapate fedha za ziada, ambazo zitawasaidia kuzitunza familia zao ambazo huziacha mjini.Walikiri kuwa ufanisi wao umeshuka kabisa.
Hali hiyo, ilibainishwa kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, ikiwa ni matokeo ya msingi ya uchunguzi wa kihabari juu ya maisha na utumishi wa wafanyakazi wa sekta ya afya uliofanywa katika mikoa minane hapa nchini.
Uchunguzi huo, ulifanywa na Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari mikoani (UTPC), baada ya kupata ufadhili wa Shirika la Utu Mwanamke (WDP).
Lengo la uchunguzi huo wa kihabari ni kubaini matatizo yanayowakabili wafanyakazi wa sekta ya afya makazini na katika maisha yao ya nyumbani.
Bw Karsan ambaye ni mwenyekiti wa UTPC, akizungumzia tathmini ya uchunguzi huo uliofanywa kati ya Oktoba 2006 na Februari 2007, alisema umehusisha wafanyakazi 230 wa kada zote za afya wakiwemo madaktari,wauguzi,wahudumu na wafanyakazi wengine.
Mikoa ambayo uchunguzi huo umefanyika na wilaya zake kwenye mabano ni Mtwara (Mtwara mjini na Masasi),Kigoma (Kigoma mjini na Kasulu), Shinyanga(Shinyanga mjini na Maswa).
Mingine ni Ruvuma (Songea mjini na Tunduru),Manyara ( Babati na Hanang), Rukwa (Sumbawanga mjini na Nkasi),Arusha (Arusha mjini na Arumeru) na Dodoma (Dodoma mjini na Kongwa).
Katika uchunguzi huo, imebainika kuwa, asilimia 90 ya wafanyakazi waliohojiwa hawapewi nyumba na waajiri wao. Ni wafanyakazi wachache sana wanaopewa nyumba za kuishi ambao ni madaktari.
“Wauguzi na wataalamu wengine hawafikiri kabisa kupewa nyumba.Wafanyakazi hao wanatumia sehemu kubwa ya vipato vyao kulipia nyumba za kupanga.Ipo nafuu kidogo kwa wafanyakazi wa mijini ambako nyumba zipo. Kwa upande wa vijijini nyumba hakuna.” Ilibainika na kuendelea.
“Mathalani wafanyakazi wa zahanati ya Endasaki wilayani Babati wanatoka saa 4 ya usiku.Wanaishi mbali na zahanati hiyo na hivyo wanalazimika kulala hapohapo kwa hofu ya kuliwa na simba waliojaa kwenye bonde la Endasaki ambalo maana yake ni bonde wanaloishi simba”.
Kwa upande wa huduma za kijamii kama elimu, maji na barabara, wafanyakazi wa mjini wana nafuu ikilinganisshwa na vijijini ambako hawapati huduma za maji safi, umeme na shule kwa ajili ya watoto wao.
“ Hata kwa matibabu yao wanalazimika kwenda mijini kutafuta huduma kwa sababu zahanati za huko zina uhaba mkubwa wa madawa na vifaa vya tiba.Wanavunjika moyo na morali yao ya kufanya kazi imeshuka sana.
Wanadai kuwa, hawapendi kabisa kufanya kazi vijijini, hivyo wanapopata uhamisho kwenda huko, wanafanya kila njia kutokwenda” uchunguzi umebainisha.
Kuhusu mazingira ya kikazi,wafanyakazi wengi walioajiriwa wamesema kuwa wanasikia kuwa kuna mikataba ya kazi, lakini wao hawajawahi kuiona licha ya kuwa wanajua kanuni na maadili yao ya kazi.
Baadhi ya wafanyakazi wa sekta binafsi walisema hupewa barua tu za kuajiriwa na wengine wamesema huajiriwa kwa mdomo tu.
Kwa upande wa mishahara,wafanyakazi karibu wote, wamelalamikia mishahara midogo wanayolipwa kiasi cha kutomudu gharama za maisha.
Mathalani muuguzi mmoja aliyeaajiriwa katika hospitali binafsi alisema mshahara wa muuguzi ni kati y ash 30,000 - 50,000 ikitegemea uhusiano baina yake na mwajiri, elimu na ujuzi.
Hata hivyo, ilisemwa kuwa hakuna utaratibu mzuri wa ajira katika hospitali au zahanti za binafsi. Muuguzi mmoja wa taasisi ya dini, alisema analipwa mshahara kati ya sh 80,000 – 83,000.
Tatizo jingine ambalo limelalamikiwa ni ucheeleweshwaji wa mishara ambayo maara nyingi wanaipata baada ya muda mwingi kupita.
“Mfano, serikali hulipa mishahara kupitia benki ya National Micro Finance ambayo haina matawi sehemu zote nchini.
Hivyo, wafanyakazi walio kwenye wilaya ambazo hazina matawi ya NMB,wanawajibika kusafiri hadi kwenye makao makuu ya wilaya kufuata mishahara yao.
Hali hii inawafanya watumie fedha zao nyingi kufuata mishahara na kupoteza muda wao mwingi wakiwa nje ya vituo vyao vya kazi.”
Kwa upande wa marupurupu, wafanyakazi wote wa serikalini na sekta binafsi karibu asilimia 70 wamesema kuwa hawalipwi marupurupu na asilimia 30 wamesema wanalipwa ila malipo yanachelewa sana.
Uchunguzi umebainisha kuwa, upandishwaji vyeo hakuna utaratibu ulio wazi unaotumika kuwapandisha vyeo na hata wale wanaopata bahati ya kupandishwa vyeo mishahara yao inabaki ileile.
“Kuna baadhi ya wafanyakazi wameonyesha wasiwasi wao mkubwa, kwamba kuna harufu ya rushwa ya mali na ngono katika upandishwaji vyeo”.
Wafanyakazi wa serikali wamelalamika kuwa nafasi za masomo ya kujiendeleza, hazipatikani bila ya rushwa kwa baadhi ya wakuu wao ili wapangwe kwenye orodha ya kupewa nafasi ya kujiendeleza.
Katika hospitali za serikali, imebainika kuwa kuna upungufu mkubwa wa vifaa vya kazi na madawa ambapo upatikanaji wa vitu hivyo si mzuri hali inayofanya wafanyakazi wafanye kazi katika mazingira magumu.
“Viongozi wa hospitali hizo, waliohojiwa wamesema Medical Store Department ambayo ndiyo inayowapa vitu hivyo, inafanya kazi chini ya matarajio”.
Uchunguzi umebainisha kuwa, katika hospitali,vituo vya afya na zahanati zote zilizotembelewa, kuna upungufu mkubwa wa wafanyakazi. Hali hii inafanya wafanyakazi kuchoka sana kwani wanawajibika kufanya kazi kwa masaa mengi bila ya kupumzika.
“Maeneo ya vijijini tatizo hili ni kubwa sana, kwani wafanyakazi wengi hawapendi kufanya kazi huko kutokana na ukosefu wa huduma za kijamii.
Mathalani katika hospitali ya Mkomaindo wilayani Masasi,daktari mmoja anahudumia wagonjwa 100.
Na hospitali ya mkoa ya Mtwara ambayo hufanya kazi kama hospitali ya rufaa haina daktari bingwa hata mmoja. Zahanati nyingi za vijijini wauguzi hufanya kazi kama waganga pia”
Kwa upande wa utawala na uongozi, wafanyakazi walioajiriwa na serikali wamesema kuna dalili za uongozi mzuri kwenye hospitali zao.
Mathakani wafanyakazi wa hospitali za mkoa wa Arusha wanasema kuwa, kutokna na mfumo wa Open Rehearsal and Appraisal System(OPRAS), kuna uwazi mkubwa kiasi ambacho wanakutana na kujadili matatizo yao.
Ukiacha hospitali ya mkoa wa Arusha, hospiatli zingine za binafsi na serikali zimeonyesha udhaifu kwenye maeneo ya uongozi na utawala.
``Udhaifu uko kwenye mgawanyo wa vitendea kazi na madawa, utunzaji wa taarifa za wagonjwa na wafanyakazi.Pia namna ya kushughulikia matatizo ya wafanyakazi yanapotokea``
Vyama vya wafanyakazi,uchunguzi umeonyesha kuwa wafanyakazi wote wa sekta hii, wamelalamika kuwa hawaya chama ambacho kinaweza kutetea maslahi yao.wanasema kuwa vipo vyama vingi vidogo vidogo ambavuo havina uwezo wa kutetea maslahi yao.
Kufuatia hali hiyo inayowakabili wafanyakazi wa sekta ya afya, walipendekeza mishahara iongezwe na kima cha chini kiwe sh 500,000 na cha juu kiwe 2,500,00 kwa kada ya udaktari.Wauguzi wamependekeza mishahara yao ianzie sh 400,000 na sh 800,000.
Wafanyakazi wote, bila ya kubagua kada zao, wapewe nyumba au posho ya nyumba.
Halikadhalika, malipo ya ziada kama vile posho ya ziada ya muda wa kazi,posho ya mazingira magumu na posho ya likizo yalipwe kwa wafanyaklazi wote kwa muda uliopangwa.
Na mfumo wa ajira,ufanyiwe marekebisho ili kuondoa utata baina ya wafanyakazi wa serikali kuu na wale wa serikali za mitaa kwa kuzingatia mikataba ya kazi,tofauti za mishara,kupandishwa vyeo,mafunzo na tofauti za marupurupu.
|