25 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Busara itumike suala la Kaduguda leo
 
2007-08-25 09:41:31
Na Mhariri

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la soka nchini (TFF) leo inatazamiwa kukutana ili kujadili suala la Katibu Mkuu wa Simba, Mwina Kaduguda.

TFF imechukua hatua hiyo kufuatia matamshi ya Kaduguda aliyodai kwamba shirikisho hilo lilipewa Sh. milioni 40 kama sehemu ya makubaliano ya kuandaliwa kwa michuano ya soka ya Kombe la Tusker yaliyomalizika.

Shirikisho hilo limeeleza wazi kuwa linataka Mwina athibitishe madai yake kwa ushahidi.

TFF imedai kwamba endapo atashindwa kuthibitisha madai yake itamwadhibu kwa uzushi.

Katika kuonyesha kwamba haina masihara na suala hili, TFF tayari imetupa utetezi wa Kaduguda ulioandaliwa na uongozi wa Simba.

Suala hili limeleta vurugu hususan kwa upande wa Simba waliojitoa kwenye michuano ya Tusker na sasa wanaona kuwa TFF ina njama za kudhoofisha uongozi wao.

Mvutano huu kwa kweli umetoka katika ajenda na kuwa mvutano baina ya klabu ya Simba na TFF.

Uongozi wa Simba unazidi kudai kwamba klabu nzima inatakiwa kuadhibiwa kama TFF inadhani kuna kosa na sio Kaduguda pekee kwani msimamo wa Kaduga ulikuwa ni wa Simba.

Hali hiyo sasa imesababisha wanachama wa Simba kutishia kwenda kujazana kwenye ofisi za TFF ili kushinikiza Kaduguda asiadhibiwe, huku TFF ikieleza kuwa anayetakiwa ni Kaduguda na si timu uongozi mzima wa timu ya Simba.

Katika kuongeza ‘chumvi kwenye kidonda’, Kaduguda amedai atavurumisha mabomu zaidi wakati wa kikao cha kamati ya utendaji.

Sisi tunashauri kwamba ni vyema busara ikaachwa itumike katika suala hili badala ya vitisho na malumbano yaliyopo sasa ambayo sisi tunaamini hayana manufaa katika maendeleo ya soka nchini mwetu.

Kinachotakiwa hapa ni kanuni na sheria viachwe vitumike, lolote litakalotokea upande utakaoshindwa ni vizuri ukafuata taratibu wa kukata rufaa kama unadhani umeonewa.

Tunachotaka kusema hapa ni kwamba viongozi na wanachama wa Simba ni bora wakatulia na kama ikitokea Katibu wao akaadhibiwa kwa kile ambacho wao hawariodhiki nacho, basi zipo taratibu za kufuata ambazo ni kukata rufaa ngazi kwa ngazi.

Sisi tunaona kama kwamba wakiamua kuandamana kwenda TFF inaweza kutishia amani na hata kutokea vurugu ambazo hazina ulazima wowote wakati kuna sheria na taratibu zilizo wazi zinazoweza kumaliza mzozo huu.

Hatuna budi Watanzania kujifunza kufuata sheria na taratibu badala ya misimamo na matakwa yetu kwani huo ndio ustaarabu wa dunia ya leo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.