25 Aug 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Atakayeshinda kwa rushwa CCM tunamuondoa- JK
 
2007-08-25 09:53:23
Na Premi Kibanga, Kishapu

Kiongozi yeyote atakayebainika kutoa rushwa kwa ajili ya kupata uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), katika chaguzi zinazoendelea kuanzia ngazi za wilaya na mikoa ataondolewa mara moja.

Rais Jakaya Kikwete alitoa tahadhari hiyo katika mkutano wa hadhara wilayani Kishapu.

Rais Kikwete yuko wilayani humo kwa ajili ya shughuli za kikazi katika mkoa wa Shinyanga.

Chama cha Mapinduzi kinafanya uchaguzi nchini kote katika ngazi ya wilaya kuanzia leo na kesho na Septemba 10-11 katika ngazi ya mikoa.

“Napenda kutoa tahadhari kwa wanachama wote, hatutakuwa tayari kuwa na kiongozi aliyepata uongozi kwa kulipa. Toeni rushwa, lakini hamtaendelea kuwa viongozi.

Chama chetu hakiwezi kuendelea namna hii kwa viongozi wanaonunua uongozi,” alisema Rais na kutahadharisha kuwa ameweka vyanzo vyake tayari kumpa taarifa na kazi hiyo inafanyika.

“Na mara uchaguzi utakapokamilika, nataka kamati za siasa za wilaya na mikoa zifanyE tathmini, lakini kubwa nataka taarifa ya viongozi waliopata uongozi kwa kununua,” alisema na kutahadharisha kuwa hata yeye amejipanga vyema kupata taarifa hizo.

Kabla ya mkutano na wananchi Rais alizindua mnada wa kisasa kwa ajili ya soko la ng’ombe.

Mnada huo umegharamiwa na serikali kwa kushirikiana na Benki ya maendeleo ya Afrika kwa gharama ya Sh. Bilioni 14.4.

Mradi huo umejengwa katika eneo la Muhunze lenye mifugo mingi ili kuweka mazingira mazuri kwa wafugaji kupata faida kutokana na mifugo yao.

Rais pia ameelezea azma ya serikali ya kufufua kiwanda cha nyama cha Shinyanga ambacho kilishakamilika lakini hakijaanza kazi.

Tayari muwekezaji amepatikana na ataingia ubia na serikali wilayani Kishepu.

Serikali imeshatenga Sh. Milioni 160 kwa ajili hya kuongeza huduma ya maji wilayani Kishepu na pia kuna mpango mwingine wa maji ambao umeshaandaliwa, utakaohudumia vijiji tisa wilayani humo ili kupunguza na hatimaye kulimaliza kabisa tatizo la maji wilayani humo.

Wilaya ya Kishapu ni wilaya mpya na hivyo haina hospitali, lakini Rais alisema tatizo hilo limeshashughulikiwa na tayari wilaya imepata kiwanja cha kujengea hospitali na pesa zimeshatengwa kwa ajili ya ujenzi kuanza wakati wowote.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.