24 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Jamaa achachamaa... kisa dume mwenzie kamwambia `kunywa bia`
 
2008-02-24 10:44:53
Na Anti Flora Wingia

Mpenzi msomaji, yapo mambo mengine ukiyaona au kuyasikia utadhani ama ni mchezo wa kuigiza au ni ndoto. Yaani kama hukuyawekea tahadhari ya hali ya juu, yaweza kuzusha balaa juu ya balaa. Au siyo?

Lugha yetu ya Kiswahili ina mitego mingi katika tafsiri za maneno yake.

Na neno linapokuwa na maana zaidi ya moja, basi huingizwa kwenye misamiati kuikuza. Ndiyo maana maneno mengi yana maana zaidi ya moja.

Yupo jamaa mmoja aliwaacha hoi wanywaji katika sehemu moja ya burudani pale alipoambiwa na mwenzie, `kunywa bia` akichukulia kuwa amedhalilishwa.

Japokuwa si Mmasai, jamaa yule aliyekuwa eneo la kaunta aliruka juu, kisha kusimama juu ya vikanyagio vya stuli ndefu huku maneno yakimwagika ovyo. Ilikuwaje?
Naam.

Mimi nikiwa jirani na kaunta ile pamoja na mama mmoja rafiki yangu, pembeni pia akiwemo baba mmoja, alifika jamaa huyo na kusabahi kwa adabu na heshima.

Kumbe jamaa huyu walifahamiana sana na baba yule. Wakawa wanazungumza masuala mbalimbali ya kijamii na siasa kwa maelewano mazuri tu huku vinywaji vikizungushwa mduara.

Jamaa huyu katika mazungumzo kila wakati alitaka yeye azungumze zaidi kuliko wenzake. Mtu akianzisha topiki fulani, basi yeye ataichukua na kuitawala kuwa ni yake, hivyo atakuwa msemaji mkuu.

Wenzake katika hatua fulani, walikuwa wakinyamaza na kumwacha atoe lecture zake na akichoka hunyamaza. Ili mradi tu anatawala mazungumzo.

Yule baba mwenzie akamtamkia ``kunywa bia`` akimaanisha kuwa apunguze kusema ili afurahie bia yake.

Lo! jambo likazua jambo. Kumbe jamaa akachukulia maana nyingine kutokana na jinsi alivyong`aka.

``Ninywe bia kwani nimekwambia sina pesa?(huku akichomoa waleti yake na kuonyesha burungutu lililomo)...huwezi kuniambia ninywe bia, ukinitakia nini...siagiziwi bia na mwanaume mwenzangu mimi, tafadhali sana...

``Yaani umenionaje(akaruka juu na kisha kuparamia stuli akitaka kuipanda), mwanaume anipe bia? mama weeee...(sasa kila mnywaji katika eneo lile aligeuza shingo kuelekea kaunta kujua kulikoni).

Wapo watu waliocheka tukio lile huku wanywaji wengine wakinong`ona kwamba kwani jamaa yule alihisi nini alipoambiwa `kunywa bia` hata kufikia hatua ya kucharuka vile?

Hata hivyo, wakati wote jamaa akiporomosha maneno, mwenzake anayemtuhumu kwa kauli yake alikuwa kimya.

Hata mie katika hali ya kujiepushia shari, taratibu niliteleza na kuishia zangu kwani sehemu za ulabu zina vishindo vyake ambavyo mie siwezi kuvihimili.

Mpenzi msomaji, kisa ni tafsiri ya maneno yale ya Kiswahili (kunywa bia) ambapo jamaa alidhani kuwa mwenzie \'anamhonga\' bia wakati masikini yeye alikuwa akimtaka tu afurahie bia yake baada ya kumuona anaongea sana.

Ni ukweli kwamba katika mazingira ya kawaida kwenye ulabu mtu kutoa ofa kwa wenzake iwe ni wanaume au wanawake ni jambo la kawaida. Na wanywaji wengi wamejijengea utamaduni wa kuzungushiana raundi za vinywaji wanapokuwa wameketi pamoja.

Anaweza kuja rafiki au ndugu yako na mkakutana kwenye viwanja vya unywaji.

Katika kuagiza kinywaji akatamka, `mpe bia huyu na yule, zungusha raundi hapa au pale.

Haya ni mahusiano mazuri tu baina ya watu wanaofahamiana.
Lakini ukiona mtu aliyejumuika na wenzie kuwa-sensitive kama bwana yule niliyemgusia hapo juu, basi ujue analo jambo fulani.
Sina hakika.

Au pengine ni mzito katika kufsiri matamshi ya wenzake baada ya kupata kilevi au sijui nisemeje.

Msomaji wangu naomba mchango wako katika hili kwani hata mimi nilishindwa kumuelewa mwenzetu yule. Sikuona sababu kwanini acharuke kiasi kile.

Yaani akawa kama mtu aliyekwisha kung\'atwa na nyoka na sasa akiona unyasi anashtuka.

Lakini haya ni mambo ya kawaida.
Hivi mtu anatarajia nini kwenye viwanja vya ulabu? Siku zote mnywaji anapotinga katika viwanja hivyo anaonekana mpole, mnyenyekevu, mwenye adabu na heshima zake.

Anaagiza chupa ya kwanza, ya pili na inapoelekea ya tatu, ule ukondoo unatoweka na ibilisi wa pombe anachukua nafasi. Majidai yanaanza, sauti iliyokuwa ya chini awali sasa inatoka.

Mtu amempeleka mkewe au girl friend outing kwa upendo mkubwa, lakini baada ya mafundo kadhaa ya kinywaji kooni anamchenjia mwenzie. Kisa ibilisi wa pombe kashikilia daftari la mahudhurio ya watu wake.

Au siyo msomaji wangu?
Hayo ndiyo mambo ambayo hufikia hatua mtu asimuelewe mwenzake katika mazungumzo kama ilivyotokea kwa jamaa yetu niliyemzungumzia katika makala haya.

Lugha pale iligongana na wakati mwingine tukio kama lile laweza kuvunja kabisa mahusiano.

Ingawa siyo rahisi katika viwanja vya ulabu, uvumilivu unahitajika sana. Ukiona mwenzi anakuja juu, wewe kuwa mpole kwani watu hatulingani. Mkilipuka wote, hakika, kila mmoja atajutia baadaye.

Heri nusu ya shari kuliko shari kamili.
Wanywaji wengine japokuwa wanajitutumua, lakini hawawezi kuhimili pombe nyingi na matokeo yake huzusha vurugu ambazo zimesababisha madhara mara nyingi.

Wajua kwenye pombe kila mtu hujifanya mbabe, hutamba ana pesa, anajua kupigana na kadhalika. Hizo zote ni tambo za kishetani, zikwepe.

Kama ni lazima, basi kunywa kiasi na kisha kama ulivyoingia mtungini kusumbua ubongo, uondoke taratibu bila kusumbua wengine. Maisha ndivyo Yalivyo.

Kama unayo maoni kuchangia hoja hii, nikandamizie kwenye Email: fwingia@yahoo.com
Wasalaam.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.