26 Feb 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Tuwasaidie wenye njaa
 
2008-02-26 09:57:28
Na Mhariri

Habari kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika zimethibitisha kwamba kuna maeneo kadhaa hapa nchini ambayo yanakabiliwa na upungufu wa chakula. Maeneo hayo yamo katika mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Lindi, Manyara, Morogoro, Shinyanga na Singida.

Tathmini iliyofanywa na serikali Oktoba 2007 katika maeneo mbalimbali imebaini kuwa jumla ya wilaya zilikuwa na upungufu wa chakula.

Habari zinasema kwamba Wizara inafuatilia kwa ukaribu suala hilo na imeanza kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hilo.

Kwa mfano, serikali imeshatoa tani 539 za mahindi kwa wenye njaa katika wilaya ya Mbulu.Hata hivyo habari kutoka baadhi ya mikoa zinasema hali ni mbaya sana.

Katika Wilaya ya Ulanga, mkoa wa Morogoro kuna habari kwamba baadhi ya wananchi wanahemea maisha ya njaa hadi kufikia kuchimba na kula mizizi ya mimea mbalimbali.

Wananchi wa vijiji vya Tekateka na Luhombelo, katika Tarafa ya Mwaya, wilayani Ulanga ndio walioathirika zaidi na tatizo hili la kukosa chakula cha kutosha.

Jambo la kushangaza ni kwamba mkoa wa Morogoro katika msimu wa kilimo mwaka jana ulizalisha tani 759,000 za nafaka wakati mahitaji ya nafaka ya mkoa huo ni tani 460,000 .Kwa mahesabu ya haraka mkoa ulibakiwa na tani 290,000 za nafaka.

Inakuwaje takwimu zinaonyesha mkoa umezalisha nafaka za ziada wakati maeneo mengine ya mkoa yana njaa?

Uongozi wa Mkoa unawajibika kufanya kazi ya ziada kukabiliana na hali hii kwa sababu kuna uwezekano chakula kingi kiliuzwa nje ya Mkoa bila mpango.

Hata hivyo, jambo la muhimu hapa ni kwamba serikali inafuatilia tatizo na tayari imeshachukua hatua mbalimbali kukabiliana nalo. Takribani wiki mbili zilizopita serikali yetu ilipiga marufuku kuuza chakula nje ya nchi.

Aidha, Serikali imeshasema kwamba jumla ya tani 300,000 za nafaka zinaruhusiwa kuingizwa nchini bila ushuru kwa ajili ya kuuzwa kwa wananchi wenye upungufu wa chakula kwa bei nafuu.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa hadi sasa kitengo cha kuhifadhi chakula (SGR) kina akiba ya chakula tani 130,000 ambacho kimehifadhiwa katika maghala mbalimbali nchini.

Hakika kiasi hiki ni kidogo sana hivyo ni vema wafanyabiashara wakajitokeza kuagiza chakula nje kuziba pengo kubwa lililopo.

Kwetu sisi uhaba wa chakula kwa wananchi wetu ni suala la kufa na kupona ambalo linapaswa kupewa uzito unaostahili na kwa kuwa tatizo limeshaonekana wazi jambo lililobakia ni kulikabili kwa dhati.

Huko nyuma hali kama hii imewahi kutokea na wafanyabiashara wengi wakajitokeza kuagiza chakula kutoka nje kwa nia njema kabisa. Lakini kutokana na urasimu serikalini, chakula hicho kilichelewa kuwafikia walengwa.

Ama kilikwama kupakuliwa bandarini au kuchelewa kusafirishwa kutoka bandarini kwenda kwa walengwa.
Safari hii tunataka utaratibu uandaliwe mapema kuwasaidia wafanyabiashara ambao watajitolea kuagiza chakula toka nje.

Na meli yenye chakula cha njaa inapotia nanga bandarini ni lazima ipewe kipaumbele kupakuliwa na chakula hicho kisafirishwe mara moja kwenda kwa walengwa.

Wakati tunangojea chakula kuagizwa kutoka nje kile kiasi kilicho katika maghala ya Serikali ni vizuri kikagawiwa kwa uangalifu mkubwa. Ni vema kila mwenye njaa apate kidogo kuliko kukosa kabisa.

Kwa upande mwingine,baadhi ya maeneo ya nchi yamebahatika kuwa na neema ya chakula wakati wote.

Huu ni wakati neema hiyo inapaswa pia kuwafikia wenzao ambao hawakubahatika kuwa nayo.

Tunawapa changamoto wafanyabiashara wa ndani kusafirisha chakula kutoka sehemu zenye chakula cha ziada kukipeleka katika maeneo ya uhaba wa chakula.

Tunatumaini serikali yetu itaweka mikakati madhubuti kukabiliana na hali hii ili kuepusha vifo. Tunaamini kabisa uwezo wa kukabiliana na hali hiyo tunao.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.