13 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Albino mwenye kichanga auawa kikatili
 
2008-03-13 10:12:59
Na Renatus Masuguliko, Geita

Mwanamke mmoja ambaye ni albino, mkazi wa kijiji cha Nyalulu katika Wilaya ya Geita mkoani Mwanza, ameuawa baada ya kukatwa miguu na mkono wa kulia.

Wakati mwanamke huyo akiuawa na kufanya idadi ya waliouawa mpaka sasa kuwa zaidi ya wanane, jijini Dar es Salaam kundi la maalbino `walivamia` ofisi za gazeti hili ili kulaani maafa yanayowafika wenzao huku wakiwa hawaridhishwi na hatua zinazochukuliwa na serikali kuwanusuru.

Mwanamke aliyeuawa ametambuliwa kama Zawadi Madindo (21), ambaye alikumbana na kifo hicho cha kikatili usiku wa kuamkia juzi.

Watu walioshuhudia tukio hilo, waliiambia Nipashe kuwa, marehemu Zawadi, alishambuliwa na watu wasiojulikana, ambao walimvamia nyumbani kwa mama yake, alipokuwa anaishi baada ya kutengana na mume wake.

Kabla ya kifo chake, Zawadi aliachika kutoka kwa mumewe (jina lake halikupatikana), anayefanya kazi kwenye migodi ya madini iliyopo katika kijijini Matabe wilayani Chato.
Alikuwa akiishi kwa mama yake, akiwa na mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja, ambaye alijeruhiwa katika paji la kushoto wakati wa tukio hilo.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kasene, Bw. Ndalikwa Mwanzalima, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo.

Hata hivyo, mashuhuda wa tukio hilo, walisema kilio kilisikika kutoka kwa Zawadi, wakati wauaji walipokuwa wakimkata kiungo kimoja baada ya kingine.

``Tulimsikia akilia sana, tukadhani anapigwa katika ugomvi wa kifamilia, lakini baadaye kilio kilitoweka... Baadaye tukasikia mama yake akipiga yowe kuomba msaada,`` mmoja wa watu walioshuhudia alidai.

Taarifa zilidai kuwa, kabla ya kukata viungo vya Zawadi, wauaji walimtishia kifo mama yake mzazi, ambaye alitimua mbio kuokoa maisha yake.

Umati wa watu ulikusanyika katika eneo la tukio jana, huku hofu ikionekana kuongezeka miongoni mwa watu wa jamii ya albino.

Aidha, katika hali iliyoonyesha kubeba hisia za wakazi wa kijiji hicho, waliunda kamati ya watu iliyosafiri kwenda katika machimbo ya Matabe, kumkamata aliyekuwa mume wa marehemu Zawadi.

Ilidaiwa kuwa, kuna wakati mume huyo aliwahi kulalamikiwa na marehemu Zawadi, kwamba alikuwa akimtishia maisha.

Kuuawa kwa Zawadi, kumekuja siku chache baada ya mtoto, Bibiana Faustin (12), ambaye ni albino, kukatwa mguu wa kulia na vidole viwili vya mkononi.

Mtoto huyo amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Geita, akiwa na mdogo wake, Tindiebhwa Faustin (10) aliyeogopa kurejea kijijini kwa kuhofia kuuawa.

Hadi tunaingia mitamboni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.

Matukio ya kuuawa kwa watu wa jamii ya albino yamezidi kuongezeka licha ya wanaharakati wa haki za binadamu na serikali kukemea vitendo hivyo.

Watu wanaohusika kufanya mauaji hayo wanadaiwa kuchukua viongo vya maalbino kwa madai ya kufanyia mambo ya kishirikina ili waweze kufanikiwa katika biashara zao.

Naye Adam Fungamwango anaripoti kwamba baadhi ya maalbino jijini Dar es Salaam, wamelaani mauaji ya wenzao yanayofanywa na baadhi ya watu sehemu mbalimbali nchini kwa imani za kishirikina.

Wakizungumza katika ofisi za Nipashe jijini jana, walisema mauaji yanayoendelea kufanywa dhidi yao ni kielelezo cha unyama uliokithiri katika jamii.

Waliiomba serikali kulichukulia tatizo hilo kama janga la kitaifa na sio kama la kisiasa.

Mmoja wa maalbino hao, Bw. Toto Ntanga akizungumza kwa niaba ya wenzake tisa, alisema anashangazwa kuona kuwa taifa limeingia katika karne ya 21 ya sayansi na teknolojia, huku baadhi ya wananchi wakiendeleza ushirikiana kiasi cha kuwaua wenzao kwa vile tu wana ulemavu huo wa ngozi.

Bw. Ntanga ambaye pia ni kiongozi wa kundi la sanaa la maabino (Albino Revolution Culture Troupe) alisema wanaiomba serikali kuchukua hatua madhubuti kudhibiti vitendo hivyo.

Alisema kutokana na tishio la mauaji kwa maalbino, maisha yao yamo hatarini na wanalazimika kurudi mapema majumbani wakihofia kuuawa.

Pia alisema wameanza kuwaogopa marafiki zao huku wazazi wa watoto maalbino wakiwakataza watoto wao kwenda shule.
Alisema hata walimu ambao katika shule zao wanasoma maalbino, wameanza kuingiwa wasiwasi kuhusu usalama wa maisha yao.

\"Hivi sasa hata marafiki zetu tunaanza kuwaogopa, maana hujui ana mawazo gani kichwani, inawezekana akakuambia twende huku kumbe anakwenda kukuua ili apate utajiri,\" alisema Bw. Ntanga.

Bw. Tuweni Pazi, alisema hivi sasa amesimama kazi kwa muda akihofia kuuawa kwani yeye kazi zake ni kusafiri na malori mikoani.

``Tajiri yangu ameniambia kwanza nisimame kazi kwa sababu ya kukithiri kwa mauaji ya maalbino, anahofia naweza kuuawa halafu yeye akawa kwenye matatizo, kwa hiyo kaniambia nikae nyumbani kwanza hadi hali itakapopoa,`` alisema.

Maalbino hao walisema kuwa fikra kuwa viungo vyao vinasababisha upatikani wa utajiri na wengine kupata madini kwenye machimbo, au mikono yao kuwa chambo kwa uvuvi wa papa ni potofu.

Alisema fikara hizo zinapandikizwa na waganga wa kienyeji wenye tamaa ya kujipatia pesa kitapeli kutoka kwa wateja wao ambao nao huamua kuwa wanyama badala ya kuwaumbua washenzi hao.

Walisema kwa jinsi wanavyoona wao, Serikali bado haijalivalia njuga suala hilo kisawasawa kama inavyofanya kwenye masuala mengine na kama wangefanya hivyo, mauaji yangepungua.

``Kuwatia mbaroni wahusika, kutoa elimu kwa wananchi kwa kutushirikisha sisi maalbino wenyewe, hii ingesaidia kupunguza dhana hiyo kwa wananchi,`` alisema Bw Fadhili Kambi.

Bw. Ntanga alisema kundi lao hivi sasa lina mpango wa kuonana na Serikali pamoja na wafadhili wawape msaada ili wazunguke kwenye mikoa ambayo imekithiri kwa mauaji ya albino ili wakatoe elimu na historia ya kweli kuhusu maalbino ambao wengi wanawaona kuwa
si binadamu wa kawaida, wakati ni binadamu kama wengine.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.