15 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Miaka miwili ya utawala, JK bado ana deni
 
2008-03-15 08:53:18
Na Abdul Mitumba

Wakati anahutubia taifa kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa kuongoza Jamhuri huru ya Tanzania, Rais Jakaya Kikwete alitamka kuwa kipaumbele cha kwanza cha utawala wake ni kuhakikisha mikoa iliyo pembezoni mwa nchi na ile iliyoachwa nyuma kimaendeleo inatazamwa mwa macho ya ziada.

Alisema lengo ni kujaribu kujenga nchi yenye usawa kiuchumi, kielimu na kiutamaduni hatimaye kila mtu popote alipo ajisikie yupo sawa na mwingine hivyo kuamsha morari katika ujenzi wa taifa linalohitaji nguvu za pamoja kufikia malengo.

Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisema ni jambo linalowezekana kwa asiye nacho kutafuta uwezekano wa kumwezesha kupata kuliko kumpokonya aliyenacho tayari.

Alisema mipango ya kitaifa inaweza kuwekwa na kusaidia wale waliokosa kwa sababu yoyote ile kupata kuliko kufanya mipango kuwapokonya walionacho ili kuwaongezea waliokosa.

Kauli hiyo ilipokelewa kwa mitazamo tofauti kwa Watanzania wengi, lakini ni dhahiri ilikuwa njema kwa watu wanaoishi katika mikoa ya pembezoni mwa Tanzania na wale ambao mikoa yao kwa sababu moja au nyingine ilijikuta ikiachwa nyuma kimaendeleo.

Alipokuwa akisema mikao ya pembezoni mwa nchi au iliyosahaulika au kuachwa nyuma kimaendeleo, bila shaka alikuwa akizungumzia Lindi, Singida, Kigoma, Rukwa na Mtwara.

Mikoa hiyo ndiyo inayotajwa kuwa ipo nyuma kimaendeleo kutokana na kutokuwa na miundombinu bora ya barabara za kuingia na kutoka, upatikanaji wa shida wa huduma za muhimu za kijamii na uwekezaji hafifu katika sekta ya elimu.

Kukosekana kwa mahitaji hayo muhimu kumesababisha hali ya watumishi wa serikali kuendelea kukwepa kwenda kufanyakazi katika mikoa hiyo kwa hofu ya kutofikiwa kirahisi.

Mfano mzuri ni taarifa za hivi karibuni za idadi kubwa ya walimu wa shule za msingi na sekondari waliokwepa kwenda kufundisha wilayani Liwale mkoa wa Lindi na kusaabisha sekondari nyingi za kata kukosa walimu.

Hali hiyo pia imekuwa ikizikumba shule na taasisi nyingine kama hospitali zilizo katika mikoa iliyotajwa hapo juu na kusababisha ugumu usio na kifani wa upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Ni kweli inakuwa vigumu katika kipindi cha miaka mawili ya utawala kwa nchi kubwa kama Tanzania kufanikisha mapungufu kama hayo, lakini ni vyema kuwepo na dalili au jitihada za wazi zinazochukuliwa katika kuondokana na mapungufu hayo.

Ukiangalia takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, hakuna ubishi bado utabaini mikoa hiyo ndiyo yenye shule chache cha Sekondari hadi sasa na ndizo zinaongoza kukwepwa na watumishi wengi wa serikali.

Kwa mtazamo wangu, serikali bado inayo nafasi ya kutekeleza ahadi ya JK juu ya kuitazama kwa macho ya ziada mikoa hiyo na mingine inayotaabika kutokana na kuwa pembezoni mwa nchi.

Nilidhani na imani inanipa kwamba, kauli ya JK ya kuitazama mikoa hiyo kwa macho ya zaida ililenga kuzipa upendeleo katika utoaji wa fedha za maendeleo, zikiwemo zile za mamilioni ya JK kwa ajili ya mikopo kwa wajasiriamali.

Au kwa kuzipa ziada ya kila kinachotolewa na serikali kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo kwa kila mkoa na kuongeza msukumo wa kustawisha jamii hatimaye kufikia malengo.

Ingawa najua serikali ina malengo mazuri juu ya kipaumbele hicho, lakini si vibaya mkazo ukawekwa katika kufanikisha azma hiyo ili kuiokoa mikoa hiyo inayoendelea kuchechemea angalau kwa kujenga vyuo vya ufundi ngazi ya kati ili kuzalisha mafundi mchundo ambao ndiyo wazalishaji mali.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.