|
Dhuluma hii ya kunyatia mali za nduguyo au mkewe ya nini?
2008-03-16 10:45:23
Na Anti Flora Wingia
Dhuluma kwa tafsiri nyepesi ni ile hali ya mtu kutwaa kitu cha mwenzake huku ukijua fika kwamba siyo chake na ni kosa. Wapo wanaodhulumu hata kwa kutumia vitisho ilimradi tu atwae kile alicho na matamanio nacho hata kama ni mali, mkewe.
Mpenzi msomaji, hebu nianze na mfano mmoja unaodhihirisha jinsi wanadamu walivyo hodari katika kudhulumu wengine bila hata kujali undugu au fadhila. Unamtoa mtu kwenye dhika, shukrani yake inakuwa ni kukudhulumu.
Yupo kijana mmoja hivi majuzi alinisimulia kisa fulani kinachohusu familia yake ambacho kinaonyesha jinsi ndugu wanavyofikia hatua wanadhulumiana mali hivi hivi.
Kijana huyu ambaye kwa sasa ni fundi mwashi, anasema kuwa katika familia yao wamezaliwa wanaume wanne na wanawake wawili, yeye akiwa ni kitindamimba.
Kaka yao mkubwa anaishi nchini Marekani na amechukua uraia wa huko.
Kabla ya kuondoka kwenda ng`ambo alikuwa na shamba lake ambako alijenga pia nyumba ndogo. Akawaachia wadogo zake wawili wa kiume.
Wakati kaka mkubwa akiwa Marekani, huku nyuma wadogo zake wakajiimarisha na kujenga nyumba zao kubwa katika shamba la kaka yao.
Tena wakabadili hati za shamba na kusomeka ni mali yao. Kwa sasa wanaishi na familia zao na wameapa kaka yao asiwaguse kwani hata kama ni risasi, zitavurumishwa.
Kaka huyo mkubwa aligundua hayo alipokuja nyumbani kusalimia ndugu, jamaa na marafiki.
Wadogo zake hao wakamtolea nje kwamba eneo hilo ni mali yao. Kuona mambo yamebadilika na wadogo zake wamemgeuka, akatafuta eneo lingine la kujenga.
Alipopata akamshirikisha mdogo wake wa mwisho ambaye ndiyo aliyedokeza habari hizi. ``Kaka yangu huyu akajenga hapo nyumba na kuniambia nikae.
Naishi hapo hadi sasa…lakini hofu yangu ni moja, je, kaka akiamua kurudi nyumbani siatanitimua mimi ili nisije nikamdhulumu kama walivyofanya kaka wale wengine?, anauliza kijana huyu.
Swali lake lilikuwa la msingi sasa. Kwamba japokuwa ametoa kiasi fulani cha fedha kuungana na kaka kununua kiwanja chenye nyumba anamoishi kwa sasa, lakini kaka yake hatakuwa na imani naye kutokana na dhuluma aliyowahi kufanyiwa na nduguze, tena uzao wa nyumba moja.
Mpenzi msomaji, si unajua tena mtu aliyewahi kungongwa na nyoka kila atembeapo akiguswa na unyasi hushtuka akidhani ni nyoka yule tena?
Kaka mkubwa alidhani kuwa amewahifadhi kwa muda wadogo zake ili nao waangaze makazi yao lakini kumbe aliwatengenezea mazingira ya kuishi.
Hata kama ndivyo, kwanini hawakumuomba na badala yake kumtishia maisha kwa mali ambayo wanajua fika si yao (ni ya kaka)? Kwanini unogewe na kitu cha mwenzio wakati unajua fika kuwa si halali yako?
Hata hivyo, nilimshauri kijana yule kwamba ni vema kama inawezekana akatafuta kiwanja chake mwenyewe na aanze kujenga ili kama kaka mkubwa ataamua kurejea kabisa nyumbani asije akamtolea nje.
Kwa maelezo yake, tayari ameshanunua kiwanja chake na anakusanya nguvu za kujenga ili awe na amani. Ama kweli Maisha Ndivyo yalivyo.
Ipo mifano mingi ya watu waliodhulumu mali za wenzao lakini wakaficha dhambi hiyo kwa vitisho vikubwa. Ukiacha wanaodhulumu mali, wapo walio hodhari katika kudhulumu au nitumie neno lingine, \'kuhujumu\' himaya za wenzao.
Mtu anajua fika kuwa huyu au yule ni mke wa kaka yake, au mke wa rafiki yake mpenzi lakini anamnyatia kimapenzi. Huu ni ushetani usiosameheka.
Mbaya zaidi, akimnasa katika ndoano ndio kabisa anamteka hata kusahau wajibu wake kwa familia. Hii ni dhuluma iliyovuka mipaka.
Hali kadhalika kwa upande wa wanawake. Wapo walio hodari kurubuni waume za wenzao na hata kuwahamisha kabisa majumbani mwao.
Yaani mtu anaanza taratibu na kisha baadaye anatwaa kabisa na kufanya mali yake japokuwa kamwibia mwanamke mwenzie.
Dhuluma hizi mpenzi msomaji ni mbaya na zipo za aina nyingi. Kama nawe wazijua tafadhali nitumie kupitia email hiyo hapo chini tuzijadili kwa pamoja.
Mitikisito katika familia zetu inachangiwa na mambo mengi hivyo yafaa tuwekane sasa ili kurejesha amani na upendo miongoni mwetu.
Kwanini watu wafikie mahali waogopane, watishiane maisha, wanuniane, wadhulumiane.
Haya ni matatizo ambayo yafaa tuyachambue na kupata ufumbuzi wake, hatimaye tuwe na maisha yaliyo bora yaliyosheheni amani na utulivu.
Au siyo mpenzi msomaji wangu?
Endapo unayo maoni au tropiki kuhusu purukshani za kimaisha, tafadhali usisite kunikandamizia kwenye email yangu lapo chini.
kwa leo naishia hapa.
fwingia@yahoo.com
Wasalaam.
|