|
Kuanza kunyauka ajenda ya uwiano wa jinsia katika uwakilishi, uwaziri
2008-03-17 08:46:49
Na Ani Jozeni
Kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri na kusherehekewa Siku ya Wanawake Duniani, kumekumbushia hisia kuhusu hatma ya malengo ya mkutano mkuu wa wanawake duniani (Beijing plus five) ulioazimia malengo ya uwiano.
Ilitakiwa kuwa theluthi moja ya uwakilishi na uwepo katika Baraza la Mawaziri ifikiwe kwanza, na baada ya hapo hatua zichukuliwe kufikia nusu, au usawa halisi na wanaume. Malengo hayo bado yapo au huenda labda `yameota mbawa`?
Wasiwasi huu unatokana na kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri, ambalo tofauti na mabadiliko yaliyotangulia lilipewa muundo mpya, idadi ya mawaziri na mawaziri wadogo ikapungua kwa kiasi kikubwa.
Wzara takriban tano zilimegwa na nyingine, na nafasi takriban kumi za unaibu waziri nazo pia zikaondoka, hali ambayo imebadili kwa kiwango kikubwa sura ya baraza hilo.
Ile `faraja` iliyokuwepo baada ya uchaguzi 2005 na kuundwa baraza sasa hoi.
Kwa vile lengo la kuwa na malengo ya idadi ya uwakilishi na uwaziri si ya Tanzania peke yake, bali ni maazimio ya jumla ya nchi za SADC, na hata Afrika kwa jumla katika Bunge la Umoja wa Afrika, inafaa tuangalie na wengine hali yao ikoje.
Ulinganishi unaruhusu mizani bora zaidi kuliko kuangalia nchi moja na kuamua kama inafanya vyema au la.
Kufikia malengo hayo si kama mikataba ya biashara ambayo inazibana nchi kwa kuuziana bidhaa, ila ni changamoto ya kitamaduni yenye athari au tahadhari tofauti za kimawazo kwa nchi husika.
Wakati Tanzania ilionekana kuwa mbele katika kutekeleza azimio hilo, na awamu ya nne ikaweka malengo hayo pamoja na mengine, kwa mfano kutilia mkazo masuala ya mazingira, matokeo ya uelekeo huo wa `kushoto` haukuwa mwema.
Hali ya maisha kwa ghafla ilianza kubadilika ikilinganisha na awamu ya tatu, na badala ya kufurahia uwakilishi mwingi zaidi hasa katika Baraza la Mawaziri, wakaanza kuliona ni `mzigo.`
Hivyo `hali ya hewa ilipochafuka,` moja ya marekebisho aliyoamua kufanya Rais Jakaya Kikwete ni kupunguza baraza lake; hakukosa sababu za kutoa - ilikuwepo pia ile ripoti `mbaya` ya REDET.
Kwa jumla Rais alieleza kuwa baraza lake kubwa, lilikuwa `limeshindwa kuleta ufanisi,` msimamo ambao inabidi ukubalike kama ulivyo, lakini kielelezo chake cha karibu, au kilichomwezesha Rais kuzungumza vile, ni ripoti ya REDET.
Ripoti hiyo pia iliandaa mazingira ya Waziri Mkuu Edward Lowassa `kuachia ngazi,` baada ya REDET kusema ni asilimia takriban 10 ya wananchi wanaoona anafanya vizuri katika kazi yake. Baraza la Mawaziri lilipata asilimia 20, hivi.
Hapakuwa na masuala ya moja kwa moja ya utendaji wa mawaziri wanawake au manaibu waziri, lakini mazingira ya kuaminika na wananchi yanajionyesha katika uwakilishi kwa majimbo, kuwa wapo wanawake wanachaguliwa, lakini si wengi.
Bado uwakilishi katika Bunge umesimama zaidi kwa wanaume, na hivyo itatakiwa kuwa nafasi yao katika Baraza la Mawaziri itakuwa na nguvu kwa wakati wa karibuni.
Uwezo wa kuongeza idadi ya wanawake hasa ilihitaji baraza lenyewe kuwa kubwa zaidi, siyo ndani ya baraza dogo lililoundwa sasa.
Wakati Tanzania imefanya mabadiliko na kupunguza idadi ya mawaziri na hasa idadi ya wanawake katika nafasi za uwaziri na unaibu waziri, Rwanda hivi punde imechukua hatua tofauti na hiyo.
Rais Paul Kagame alifanya mabadiliko ya nguvu kiasi katika Baraza la Mawaziri na kuongeza wizara tatu, wakiwa zaidi ni wanawake waliofaidika katika mabadiliko hayo.
Katika mazingira ya vurugu yaliyotokea Kenya, si rahisi watu kuanza kuuliza wanawake ni wangapi.
Wala hakuna aliyewahi kusikia suala kama hilo likiibuliwa katika kuundwa kwa serikali ya Congo (Jamhuri ya Kidemokrasi) wakati uchaguzi mkuu wenyewe mapema mwaka jana uligubikwa na machafuko hasa jijini Kinshasa.
Baada ya `bwana vita` wa eneo hilo, Jean-Pierre Bemba kushindwa uchaguzi na Rais Joseph Kabila ambaye aliungwa mkono zaidi katika maeneo ya mashambani (au mikoani), kulizuka uasi, kama vile Bemba na watu wake wangeteka Kinshasa, ili kulazimisha kugawana madaraka.
Lakini kwa vile kura zilikuwa halali, fukuto hilo lilibakia la kijeshi, na si mkusanyiko wa watu kudai haki zao kama Kenya.
Kwa hali hiyo, inaelekea suala la idadi ya wanawake, ambalo limekuwa na sura halisi ya kuwekewa malengo nchini Afrika Kusini, Tanzania na sasa Rwanda, ni jambo ambalo linaonekana vizuri katika mazingira fulani.
Ni pale ambako hakuna ugomvi wa kiuwakilishi (na hivyo pia kuunda Baraza la Mawaziri) ndipo inakuwa `salama` kuzungumza habari za uwakilishi-uwiano kwa upande wa wanawake.
Pale migogoro inapozuka suala la uwakilishi-uwiano hubaki la vyama.
Ndiyo maana hata hapa nchini, licha ya kuwa hapakuwa na mgogoro wa dhati kwa maana ya kufanana na Kenya au Congo DR lakini kwa kiwango kile pia, ilitosha kuondoa kiwango cha uwakilishi.
Baraza linapokuwa dogo, vyama au vikundi muhimu katika uwakilishi na utii ndani ya vyama vinakuwa muhimu kuzingatiwa, kwani `uhai` wa mshikamano wa uchaguzi (mtandao) unakuwa upo mashakani pale watu muhimu wanapoachia ngazi, kama akina Edward Lowassa, Zakia Meghji, Basil Mramba na wengineo wengi. Waliobaki inabidi `watunzwe.`
Hali hii inawezesha `kutungiwa kanuni,` kuwa suala la viwango vya uwakilishi kwa upande wa wanawake, iwe ni katika Bunge au Baraza la Mawaziri, ni budi litazamwe kwa mapana na marefu `halisia,` na siyo ya kidhanifu.
Mkazo ambao vikundi vya wanaharakati jinsia vinaweka katika uwakilishi wanawake ni wa kidhanifu, kwani wanajaribu kuliinua suala hilo kuwa la msingi, kwa sababu tu ya kubeza tofauti na mivutano ya msingi zaidi katika jamii, inayohusu haki na nafasi ya jamii-lugha au jamii-tamaduni tofauti za nchi, katika utawala.
Pale ambapo tofauti hizo zinakuwa ndogo sana, hali ipo shwari, kunakuwa na nafasi ya kuangalia masuala ya uwiano-jinsia. Linakuwa siyo kama suala la msingi ila ni mwendelezo wa maridhiano na `faraja` katika serikali, yaani mahali pasipo na mivutano.
Hivyo ni kosa kuita uwiano-jinsia kuwa ni harakati, kwani ni 'nakshi.'
|