21 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Miaka 10 ya Soko la Hisa Dar
 
2008-03-21 10:15:12
Na Theo Mushi

Ifikapo mwezi Aprili Soko la Hisa la Dar es Salaam litatimiza miaka kumi tangu lianzishwe. Kabla ya hapo serikali ndiyo ilikuwa inatoa mitaji ya kuwekeza katika mashirika ya umma.

Kwa sasa serikali imejitoa katika shughuli za biashara na uzalishaji. Sasa inaendelea kujenga mazingira bora kwa ajili ya wawekezaji kutoka sekta binafsi.

Katika mfumo wa soko huria na sekta binafsi kuwa ni injini ya ukuaji uchumi ni muhimu kuwa na soko la hisa kama Dar es Salaam Stock Exchange (DSE).

Soko la hisa linafanya Watanzania wawe na utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza katika hisa za makampuni yanayoorodheshwa katika soko la hisa.

Kwa mwekezaji ananufaika kwa njia mbili na mojawapo ni kupata gawio (dividends) kama kampuni iliyo orodheshwa itapata faida na wakurugenzi wataamua sehemu ya faida hiyo igawiwe kwa wenye hisa katika kampuni husika.

Vilevile jinsi kampuni inavyoendelea kujiendesha kwa ufanisi thamani za hisa zake hupanda na hivyo mwekezaji ambaye alinunua hisa kwa Tshs. 300 anaweza kuuza hisa hiyo kwa mkono kwa sh. 600 ambayo ni faida ya asilimia mia moja.

Vile vile ifahamike kuwa kwa miaka kumi iliyopita faida ya hisa za DSE (earnings per share) ni zaidi ya asilimia kumi na moja ambayo ni zaidi ya riba inayotolewa na mabenki kwa amana za muda maalum na vilevile riba za dhamana za serikali au Treasury Bills.

Ni muhimu DSE kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu faida za kununua hisa za makampuni yaliyo orodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam kwa sasa kuna makampuni saba yaliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, makampuni hayo ni TBL (bia), TCC (sigara), Twiga Cement, Tanga Cement, Swissport (DAHACO), TOL na TATEPA (Chai Bora).

Kuna makampuni mengine matatu ambayo yameorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam na Nairobi katika mpango unaotwa cross listing. Nayo ni Kampuni ya Bia ya Kenya (EABL), Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) na Diamond Jubilee Group.

Kwa makampuni yanayojiorodhesha ni njia rahisi ya kupata mitaji kuliko kukopa kutoka mabenki ambayo riba inayotozwa ni zaidi ya asilimia kumi na tano.

Makampuni yanayojiorodhesha kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam yanapunguziwa kodi ya mapato na gharama za kuandaa kampuni kujiorodhesha hupunguzwa katika kodi ya mapato ambayo kampuni inatakiwa kulipa. Hapo baadaye makampuni yaliyoorodheshwa katika soko la hisa yatapewa kipaumbele katika zabuni za serikali au public procurement.

Mwekezaji katika soko la hisa anaweza kutumia hisa zake kama dhamana ya kukopa kutoka kwenye mabenki ya biashara na taasisi za fedha.

Madhumuni makubwa ya Soko la Hisa la Dar es Salaam ni kujenga utamaduni wa kuweka akiba miongoni mwa Watanzania ili fedha hizo zielekezwe katika sekta za uzalishaji. Utamaduni wa kuweka akiba huchangia katika upatikanaji wa mitaji na kukua kwa uchumi wa nchi.

Uchumi wa taifa hauwezi kukua bila kuwepo kwa sekta ya fedha ambayo inajiendesha kwa ufanisi. Umuhimu wa sekta ya fedha katika uchumi wa nchi ni sawa na mafuta ya oil yanavyotakiwa katika injini ya magari.

Sekta ya fedha inawezesha fedha kutoka kwa walioweka akiba ziende kwa wawekezaji (deficit spending units) na kuongeza ufanisi katika kutumia rasilimali katika sekta mbali mbali za uchumi.

Masoko ya fedha yamegawanyika katika masoko ya muda mfupi (money markets) na masoko ya fedha ya zaidi ya mwaka mmoja yaani capital markets.

Masoko ya mitaji yanaendeleza mitaji kutoka kwa wananchi na taasisi za fedha kwenda kwa wawekezaji katika sekta mbali mbali za kiuchumi.

Katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ambalo ni `secondary market\' watu hununua au kuuza hisa kupitia madalali au brokers. Hawa wamepewa mafunzo maalum katika biashara ya ununuzi au uuzaji wa hisa na hati fungani (corporate bonds).

Hawa ni kiungo muhimu kati ya wauzaji wa hisa na wanunuzi. Baadhi ya makampuni hayo ni Orbit Securities, Vertex, Tanzania Securities, Solomon Securities, Core Securities na Rasilimali Ltd.

Zaidi ya kusajili hisa Soko la Hisa la Dar es Salaam limesajili hati fungani za BIDCO, Standard Chartered, Barclays Bank na EADB. Vile vile dhamana mbalimbali za serikali au Cooperate bonds za muda mrefu zimesajiliwa DSE ambapo wawekezaji wengi ni taasisi za fedha.

Hivyo Soko la Hisa la Dar es Salaam hurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara. DSE hurahisisha uuzaji wa hisa na hati fungani za makampuni kwa gharama ya chini na kuwezesha makampuni hayo kujiendesha kwa faida zaidi kuliko kukopa kutoka kwa mabenki.

DSE hujenga utajiri kwa watu ambao wanawekeza katika makampuni yaliyoorodheshwa katika soko la hisa.

Tangu Soko la Hisa la Dar es Salaam lianzishwe faida ya hisa kwa wawekezaji ni zaidi ya asilimia kumi na moja ambayo ni juu ya mfumuko wa bei ambapo kwa sasa ni asilimia 6.4.

Zaidi ya hapo Soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya kuwaelimisha watu wanunue hisa za makampuni yaliyoorodheshwa limesaidia kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza katika hisa na hivyo kupanua wigo wa uwekezaji ambapo hapo awali haukuwepo.

Baada ya uhai wa miaka kumi kuna umuhimu wa DSE kuendelea kutoa elimu kwa makampuni kujiorodhesha katika soko la hisa.

Makampuni yaliyoorodheshwa katika soko la hisa yana utawala bora kwa sababu mambo yote kuhusu utendaji lazima yawekwe bayana kwa kutoa taarifa kuhusu utandaji katika soko la hisa na katika vyombo vya habari.

Makampuni yaliyosajiliwa katika soko la hisa hulipa kodi ya mapato ya asilimia 25 badala ya asilimia 30 kwa kipindi cha miaka mitatu mradi hisa asilimia 35 ziwe zimeuzwa kwa wananchi.

Gharama zote za kusajili kampuni soko la hisa na kuandaa `prospectus\' hupunguzwa katika kodi ambayo kampuni hulipa ili faida ya kampuni isiathirike.

Katika biashara ya hisa kodi ya `stump duty` ni sifuri ukilinganisha na asilimia sita kwa makampuni ambayo hayajasajiliwa.

Kodi ya zuio ni asilimia tano ukilinganisha na `with holding tax` ya asilimia 10 kwa makampuni ya kawaida. Hakuna kodi ya zuio kwa faida au riba inayotolewa na hati fungani.

Kama hisa ikipanda thamani hakuna kodi inayotozwa ukilinganisha na `capital grown tax` ya asilimia 10 kwa makampuni mengine. Mapato yanayopatikana kwa uwekezaji katika Umoja Fund hayalipiwi kodi.

Faida za kuwekeza au kujisajili kwa kampuni katika soko la hisa ziko wazi kabisa. Sasa hivi limeanzishwa soko la pili DSE kwa makampuni madogo na ya kati (SME) ambalo linaitwa Enterprise Growth Market.

Hii ni fursa kwa makampuni madogo kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Katika soko hili si lazima kampuni iwe imekuwepo kwa miaka mitatu na siyo lazima iwe na historia ya kuwa na faida kwa miaka miwili.

Siyo lazima kutumia gharama kubwa za mawakala na wahasibu kusajili makampuni katika Enterprise Growth Market.

Huu ni wakati wa makampuni ambayo yamekuwa yakisaidiwa na SIDO kupata mitaji na masoko kuanza kujitayarisha kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salam.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.