|
Malalamiko ya raia dhidi ya polisi kugeuza vituo miradi yasipuuzwe
2008-03-22 09:25:06
Na Abdul Mitumba
Kwa muda mrefu sasa, malalamiko ya raia dhidi ya baadhi ya askari polisi kwamba wanageuza vituo vyao vya kazi na kuwa miradi ya kujipatia fedha kutoka kwa watuhumiwa, yamekuwa yakisikika kila wakati.
Wakati mwingine hali hiyo imekuwa ikitishia kuwepo kwa upotevu wa amani kutokana na baadhi ya watu kuwachukia polisi kiasi cha kukataa kuwapa ushirikiano ambao ungesaidia kufichua wahalifu.
Ni wazi kuwa hivi sasa kila utakapopita au kukutana na watu katika vikao mbalimbali, lalamiko kubwa utakalosikia ni jinsi raia wasivyotendewa haki na baadhi ya askari polisi ambao wamekuwa wakipelekewa malalamiko ya kuwepo kwa vitendo vya uhalifu, lakini hawawajibiki.
Malalamiko hayo pia yamezusha hofu ya kuwepo kwa uhusiano bora kati ya polisi wanaojihusisha na vitendo hivyo na raia wema ambao wengi wao wanaishi pamoja mitaani katika nyumba za kupanga.
Vitendo vinavyofanywa na polisi hao pia vimekuwa vikisababisha utekelezaji wa majukumu ya jeshi hilo kupuuzwa na wananchi waliowahi kufanyiwa vitendo hivyo vya aina hiyo, hivyo kuliweka pabaya jeshi la polisi.
Hata hivyo, kuwepo kwa malalamiko hayo hakuna maana kuwa jeshi zima `limeoza` la hasha, bado kuna askari waadilifu ingawa ni ukweli usiofikika kwamba kila idara inayojihusisha na vitendo vya rushwa, inapoteza imani kwa wananchi ambao ndiyo msingi wa kwanza wa kuwepo kwake.
Nimeanza na maneno hayo kutokana na ukweli kuwa, malalamiko hayo yanazidi kila kukicha kiasi cha baadhi ya wananchi kuamua kuyasema wazi katika vikao na mikutano ya wananchi pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali.
Mfano wa hivi karibuni ni pale wananchi wa kata ya Hananasif, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, waliposimama mbele ya viongozi wa mitaa, kata na wilaya kueleza kinagaubaka jinsi askari polisi wa vituo viwili vya kata hiyo wanavyokiuka maadili ya kazi yao.
Wakiwa mbele ya Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Bi.Zuhura Almas, Diwani wao Bw.Abbas Tarimba na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, DC Fabian Massawe katika mkutano wa hadhara wa kusema na kusikiliza kero za wananchi, raia wema walisimama na kuanza kutapika `nyongo`.
Mmoja wa wananchi waliosimama mbele ya DC kueleza kero na mienendo ya pilisi katani humo ni Bw.Stephen Gwaka, ambapo alisema inashanganza kuona polisi wanakumbatia watuhumiwa licha ya kwamba wamekuwa wakifikishwa katika vituo hivyo kila siku.
Hata hivyo, alisema baada ya muda mfupi watuhumiwa hao wengine wakiwa sugu katani humo, utawaona wakirandaranda mitaani na kuendelea na uporaji tena uliopitiliza kwa sababu huwa wanawalenga waliotoa taarifa za kukamatwa kwao.
Nipashe ilikuwepo katika mkutano huo, ambapo ilimsikia Bw.Gwaka alieleza bila woga kuwa polisi hao wamekuwa na tabia ya kuwafuata baadhi ya watu majumbani au vijiweni na kuwakamata kisha kuwatoa `upepo mifukoni` na baadaye kuwaachia.
Kibaya zaidi, alisema utaratibu wa kuwaachia watu wanaokutwa na vitu vya wizi bila kuwafikisha mahakamani umekuwa ukuwakasirisha mno watu hasa wale wanaoibiwa mali zao hatua inayochochea uhasama kati ya raia wema na watuhumiwa hao.
Kufuatia malalamiko hayo, DC Massawe aliagiza maafisa wake ngazi ya kata na wananchi kuweka mitego dhidi ya askari hao ili kuwanasa hatimaye wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria.
Alisema kama itawawia vigumu kutengeneza mitego inayowezesha kuwanasa watu hao kupitia wananchi, DC Massawe ameagiza waiarifu TAKUKURU ili ije kuwatia mbaroni wote wanaojiusisha na `biashara` hiyo isiyo na mtaji unaoeleweka,
Zaidi ya hayo,DC Massawe akionyesha kukasirishwa na taarifa hiyo, alitoa namba yake ya simu kwa kila mtu mkutanoni hapo ili kutoa nafasi kwake kwa kila mwenye tatizo linalofanana na polisi kujihusisha na vitendo vya rushwa nje na ndani ya vituo vya kazi.
Kwa maoni yangu, hatua hiyo ya DC ni hatua ya kwanza ya kupambana na tatizo hilo, lakini hatua ya pili iende kwa raia wema kutoacha kufichua polisi wanaojihusisha na vitendo hivyo na hatua ya tatu ni kusambazwa kwa TAKUKURU au vyombo vingine vya haki hatimaye kuzima kabisa `biashara` hiyo.
|