23 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Nguvu sasa zielekezwe ujenzi wa madarasa kidato cha tano na sita
 
2008-03-23 10:56:03
Na Mhariri

Juhudi kubwa za serikali katika kujenga madarasa kwa ajili ya wanafunzi wanaojiunga na sekondari zimeonekana. Katika kipindi kifupi tangu serikali iagize ujenzi wa sekondari kata, mafanikio makubwa yamedhihirika sehemu mbalimbali nchini.

Hata hivyo, juhudi hizi, hakika, zilipaswa kwenda sambamba na nyongeza ya shule kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne kuingia kidato cha tano.

Kutokana na kutofanyika hilo, ndio maana sasa tunashuhudia wingi wa wanafunzi waliofaulu kuendelea kidato cha tano kukosa nafasi katika ngazi hiyo.

Wiki hii Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jumanne Maghembe ametangaza matokeo ya wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha tano katika shule za serikali, vyuo vya ufundi na Chuo cha Maji Rwegarulila.

Akasema kuwa kati ya wanafunzi 24,946 waliofaulu, 16,222 wamekosa nafasi kujiunga kidato cha tano.

Mbali na idadi hiyo kubwa ya wanafunzi kukosa nafasi za kujiunga shule za serikali, Profesa Maghembe amesema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano mwaka huu ni wengi kuliko mwaka jana.

Waziri huyu ametaja sababu za wanafunzo hao kukosa nafasi kidato cha tano kuwa kunatokana na shule zilizotarajiwa kutokuwa na miundombinu iliyokamilika kuweza kupokea wanafunzi.

Akashauri waliokosa nafasi kuomba kujiunga na vyuo vya ualimu ambapo kwa sasa wizara imetenga nafasi 6,000 kwa ajili ya mafunzo ya ualimu daraja la tatu. Aidha akashauri wajiunge na kidato cha tano shule zisizo za serikali.

Inavyoonekana, serikali yetu bado haijajipanga vema katika kuwapokea wanafunzi wanaomaliza kitato cha nne na kufaulu kuingia kidato cha tano.

Msukumo na msisitizo zaidi umeelekezwa katika ujenzi wa shule za sekondari hasa kuwapokea wanaofaulu darasa la saba kuingia kidato cha kwanza. Zoezi hili, hakika limeonyesha mafanikio makubwa.

Tatizo sasa linakuja katika nafasi za wanaomaliza kidato cha nne kuingia cha tano na cha sita.

Ngazi hizi yafaa zitizamwe kwa makini na hatua madhubuti zichukuliwe.

Kimantiki ilitakiwa wakati mkazo unawekwa katika ujenzi wa madarasa ya sekondari, hali kadhalika, ungeenda sambamba na nyongeza ya madarasa ya kidato cha tano na sita ili wanafunzi wanapofikia ngazi hizo wasikwame.

Si hilo tu, bali mafunzo kwa walimu wa kutosha ni muhimu ili wanafunzi katika ngazi hizi wasiwe na uhaba wa wataalamu hao wanapokuwa madarasani.

Siyo siri kwamba hata katika shule hizi za sekondari zlizojengwa kwa wingi katika muda mfupi, nyingi hazina walimu wa kutosha na wenye ujuzi.

Uchache wa walimu katika nyingi ya shule zetu ni dhahiri, hivyo serikali yetu yafaa iweke miakakati madhubuti kuhakikisha kuwa fani hiyo inasimamiwa kikamilifu ili kuondoa aibu hii ya wanafunzi wetu kuchemsha bongo na kufaulu, lakini wanaishia kuambiwa nafasi za kuendelea hazipo au walimu ni wachache.

Ni matarajio yetu kwamba tatizo hili la wanafunzi kufaulu halafu wanakosa nafasi ya kusonga mbele litatatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuwapa moyo wa kusoma vijana wetu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.