|
Ufisadi ng`ambo ni sawa na kitendawili !
2008-03-23 10:58:08
Na Anti Flora Wingia
Wiki mbili zilizopita, katika safu hii nilijadili mabishano fulani yaliyohusu, `Nikipata ukubwa wazazi wangu nitawapiga shopping ya nguvu ili wasiniaibishe`.
Wapo wasomaji kadhaa waliotoa maoni yao kuhusiana na suala lile na ningependa niyawasilishe kama walivyonitumia kupitia email ya hapo chini.
Narejea kauli aliyotoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisisitiza uadilifu miongoni mwa viongozi kwamba, `yuko tayari kuona wazazi wake wakiishi katika kijumba chao kidogo cha sasa na si katika mazingira ambayo ni kinyume na madili\'.
Wasomaji kadhaa wametoa maoni yao kuhusu topiki ile kama ifuatavyo:-
Mmoja wao anasema hivi: ``Duh! hiyo ni kali? Hao jamaa waliokuwa wabishi hakika ni malimbukeni wakubwa. Mjini kuna malimbukeni watu wazima kibao.
Yaani haoni yule Mzee `Dad` wa Pinda na `Mom` walitoka bomba sana siku ile jamaa akiapishwa? Ile ndiyo inatakiwa kabisa wanawakilisha kitu muhimu sana, wenyewe hata afya zao zilikuwa FIT.
Sasa hao wabishi huoni wanaendeleza vitambi tu na kisukari kwa kunywa bia na kushibisha utumbo, ni kuendeleza mawazo ya kifisadi? Kama Mhe. Pinda angewahi shopping za nguvu kwa hao wazee wake si kwamba hana hela ila yale mawazo ya kifisadi bado yasingekatika chain (mnyororo).
Jamii ya Waafrika ‘especially’ Watanzania tusipobadilika kujenga nchi yetu ni ndoto, wachache matajiri wengi masikini. Ufisadi kila siku unasikika kwa vigogo ngazi za juu, ni kujidhalilisha viongozi wetu mbona mtoni kwa weupe ufisadi ni sawa na kitendawili? Mbona Mwalimu Nyerere ndiye pekee amebakiza living memory? Wengine mtakufa familia zenu zitatukanwa vibaya sana! Ngoja tu kwa leo nikomee hapa.
B. Mbwambo Kigali, Rwanda.
Mwingine naye anayo yafuatayo; Bi Flora, sijui kama utakutana tena na hao jamaa zako kwani mashitaka kwao, yawe ya kweli au porojo, hayatawafurahisha. Ukienda tena kwenye mgahawa au baa na kuwakuta, huenda wakakukimbia.
Lililo gumu hapa, ni kuendeleza fikra potofu za kuogopa waandishi kila wapitapo kwa madai kwamba kawaida yao ni kuandika lolote wanalosikia.
Mwandishi kubuhu kama wewe inabidi kupima unaumbua nini. Nia ilikuwa njema, kujaribu kumchambua Mhe Pinda kwa kigezo cha kuwaleta wazazi kushuhudia kuapishwa kwake.
Hao walikuwa mashahidi tu ili waweze kumuasa kijana wao asivuke mipaka na kuingia tamaa zisizofaa. Tumpe muda tuone.
Shabiki wa Magazeti
Mlee mwanao katika njia impasayo, naye hataiacha atakapokuwa mkubwa--. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.
Hivyo ndivyo Mizengo alivyolelewa na wazazi wake.
Anawaheshimu na kuwakumbuka katika kila hali.
Kwa kipindi kifupi alipopewa taarifa aliwakumbuka wazazi ambao malezi yao yamemfikisha hapo alipo.
Licha ya kuwa kwamba wameishi miaka ya mkopo (70+), bado anawaamini katika ushauri wao. Bado atawasikiliza na kwa njia hiyo atapata ushauri hata kutoka kwa walalahoi kupitia wazazi wake.
Kama walivyoonekana wazazi wa Mizengo, ndivyo wengi wetu tunavyotakiwa kuonekana.
Kununua mavazi ya London kwa malaki kupenda kuonekana tofauti na watu wengine si jambo la maana. Utafanya ufisadi tu hata kama wewe ni muhudumu.
Thamani ya mtu ni yale anayosema na jinsi anavyoyatekeleza kimatendo.
Maendeleo huanza nyumbani, kama huwezi kuwaangalia japo wazazi wako, vipi leo utatuletea maisha bora kila mtanzania..Sisemi uwe fisadi lah! lakini kivazi si kitu katika nafasi yake cha kusumbua
sack Mapambano
Mimi napingana na Waziri wetu mkubwa kuwaleta wazazi wake wakiwa katika hali ile kwani mtu kuvaa vizuri siyo lazima uwe na mshahara mkubwa sana. Pia siyo kuwa huwajali wazazi wako. Kama umekuwa katika uongozi kwa muda mrefu, kuwa na maisha mazuri ya kawaida siyo ajabu.
Alipaswa kuwa amewajengea nyumba nzuri ya standard ya kawaida siyo ya kifahari sana kwani alikuwa Waziri, na mshahara wake halali uliweza kufanya vitu vyote hivyo.
Mbona watu wenye kipato cha kawaida wana nyumba nzuri watoto wao wanasoma shule nzuri na wanavaa vizuri?
Kwa kauli yake anataka kutueleza kuwa mtu yeyote mwenye kazi serikali asiwajali ndugu zake ili kuonyesha kuwa siyo mwizi?
Mie nategemea mke wake atakuwa kwenye standard nzuri ukizingatia kuwa atakuwa anahudhuria mikutano mbalimbali, anaalikwa sherehe mbalimbali. Asije kudaganywa kwenda akiwa rafu ili ionekana hawana hela. Hatutamuelewa kwani mshahara wa Waziri Mkuu ni mkubwa.
Aganyira
Email ya kufunga pazia la topiki ile inasema, ``Ndugu mhariri napenda kukuunga mkono kutokana na maadishi yako. Pia kuhusu suala la kupata madaraka na kuanza kuwaibia wananchi ili kujinufaisha binafsi.
Watanzania tujifunze kuwatumikia wananchi tuepukane na tamaa kama tutakuwa mfano mzuri kimaadili na Taifa letu litaendelea sana.
Raia hawatapata shida sana, ingawa uchumi wetu mdogo, lakini kila kitu kinachofanywa kwa nia njema na Mwenyezi Mungu atatusaidia amin! Hamad Mkumba.
Mpenzi msomaji, niliona niwasilishe maoni ya wasomaji wapenzi wa safu hii kuhusiana na topiki hiyo, kisha wiki ijayo niwamegee kisa kipya cha mama mmoja aliyempoteza mwanae aliyegongwa na gari, pia ndoa kuyeyuka.
Kisa maneno yake eti `atamvua Yesu, amvae Shetani`` Ilikuwaje? Usikose Nipashe Jumapili ijayo.
HERI YA PASAKA.
Pia ukiwa nalo jambo ambalo wataka tuelimishane usisite kunikandamizia kupitia email ifuatayo;
fwingia@yahoo.com
Wasalaam
|