24 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Waganga holela wa jadi wafichuliwe
 
2008-03-24 10:36:04
Na Mhariri

Huku wasiwasi wa mauaji ya albino ukiendelea kushamiri nchini, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Xavery Maketta, amefuta vibali vyote vya usajili wa waganga wa tiba asilia wilayani humo na kuagiza usajili huo ufanyike upya.

Mkuu huyo amechukua hatua hii kutokana na maelezo kwamba baadhi ya waganga wa jadi wanahusishwa na mauaji hayo ya kikatili.

Inasadikika kwamba baadhi ya waganga wa jadi huwadanganya wateja wao wanaosaka utajiri kwenye migodi ya madini na uvuvi katika Ziwa Victoria kwamba kwa kuwaua albino na kuwapelekea baadhi ya viungo watafanikisha azma hiyo.

Halikadhalika, jeshi la polisi mkoani Mwanza limetangaza kwamba wahalifu wanaojihusisha na mauaji ya albino na vikongwe kwa imani za kishirikina wajisalimishe wenyewe kwa kuwa siku zao zinahesabika.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Zelothe Stephen alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika kongamano maalumu la kujadili mikakati ya kupambana na mauaji ya albino na vikongwe lililofanyika mjini Mwanza.

Kamanda Stephen aliwaambia washiriki wa kongamano hilo kwamba mifupa miwili ya binadamu ilikamatwa katika mtaa wa Bugarika jijini Mwanza na mingine miwili ilinaswa katika harakati ya kuisafirisha nje ya jiji hilo.

Kamanda Zelothe alisema kwamba katika operesheni maalumu iliyofanywa na polisi mkoani humo, waganga wa jadi ambao idadi yao hakuitaja walitiwa mbaroni na Kikosi cha Kupambana na Ushirikina mkoani humo.

Kikosi hicho kinaundwa na askari kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Idara ya Usalama wa taifa na Jeshi la Polisi.
Wakati hayo yakiendelea, imeweza kubainika kwamba, zaidi ya waganga wa jadi 14,500 mkoani Mwanza pekee hawana usajili wala makazi ya kudumu.

Waganga hao ni sawa na asilimia 87.5 ya waganga wote wa jadi mkoani humo ikiwa ni takwimu zilizomo kwenye taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Tiba Asilia mkoani Mwanza, Dk. Charles Makoba katika kongamano hilo.

Kwa vile baadhi ya wananchi wanaamini waganga kama wanavyoamini dini, wingi huu wa waganga ambao uwazi wa shughuli zao hufanyika gizani ni jambo la hatari sana.

Ni rahisi, hata kama hatujafanya utafiti wa kisayansi, kuwa na nadharia kwamba hawa wanachangia kuwepo kwa mauaji ya albino na vikongwe kwa imani za kishirikina.

Kwanza tunapenda kutoa pongezi kwa jitihada ambazo zimeanza kuchukuliwa na wadau mbalimbali wa usalama wa wananchi kwa kuguswa na hatimaye kuchukua hatua zinazoelekea kuzaa matunda kuwakamata wahalifu hawa.

Huu huenda ukawa ndio mwanzo mzuri endapo tu kila mmoja katika nafasi yake, kuanzia wananchi wa kawaida hadi vyombo vya ulinzi na usalama vitatimiza majukumu yao kikamilifu.

Ingawa si kweli kwamba waganga wote wa jadi wanajihusisha na shughuli zinazopelekea mauaji ya albino, ni wazi kwamba baadhi yao wanahusika kutokana na ushahidi kama uliojitokeza ambapo baadhi yao walikutwa na viungo vya binadamu.

Bila shaka, pamoja na mikakati kama ya kufanya usajili mpya wa utoaji vibali vya waganga hao, ipo haja kwa serikali kupitia upya sheria zilizopo ili kuwepo vifungu vinavyolazimisha waganga wote wa jadi kulazimika kusajiliwa.

Idadi ambayo imejitokeza mkoani Mwanza ni mfano dhahiri kwamba waganga wa jadi walio wengi bado wanaendelea kufanya kazi zao kwa vificho na hivyo kupata mwanya wa kujihusisha katika vitendo vya uhalifu.

Tuliwahi kushuhudia, mathalani, baadhi ya waganga wa jadi ambao waliwahi kutiwa mbaroni mkoani Tanga wakifanya zindiko kwenye bunduki ambazo zilikuwa zikitumika na majambazi.

Sheria kama hizi ndizo ambazo zitatoa mamlaka kwa serikali za mitaa kuanzia mitaa, vitongoji, vijiji, kata, wilaya, mkoa hadi taifa kuwatia mbaroni waganga wote ambao watabainika hawana usajili rasmi na wala makazi yao hayajulikani.

Ni vyema ikaeleweka kwamba, mbali na juhudi za serikali, kila mwananchi ana wajibu wa kuwafichua waganga ama watu wanaojihusisha na uhalifu huo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.