25 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Vita dhidi ya Microsoft ni muhimu kwa watumiaji?
 
2008-03-25 09:03:19
Na Nimi Mweta

Uamuzi mwingine umefikiwa katika baraza la kuzuia ukiritimba wa biashara la Umoja wa Ulaya kuwa kampuni kubwa ya programu za kompyuta zinazotumika karibu kila ofisi duniani ilipe dola bilioni 1.3 kwa kukaidi maagizo yake.

Maagizo hayo si mapya, yaliwahi kuamuliwa na mahakama za Marekani katika ngazi za rufaa, karibu na kufikishwa katika Mahakama Kuu ya nchi hiyo, Supreme Court, ambayo ina uwezo wa kufuta vipengere vya Katiba kwa uamuzi unaogusa Katiba, kama kuhusu adhabu ya kifo, utoaji mimba n.k.

Umoja wa Ulaya ulidaka suala hilo kutoka Marekani, ikalipania.

Kinachogomba katika suala hilo ni kuwa Microsoft inatakiwa itoe vianzio halisi vya programu zake muhimu kwa mfano ile ya 'Windows' inayotumika katika kuendesha takriban asimilia 90 ya programu za kiofisi kote duniani.

Mawakili wa washindani wao kadhaa wanadai kuwa kutokutolewa wazi kwa vianzio hivyo 'kunazuia kampuni shindani kulifikia soko,' hali ambayo imekuwa ikiwashangaza wafuatiliaji wengi.

Na ni wengi sana huko Marekani, Ulaya na kwingineko wanaoshangilia maamuzi hayo ya mahakama.

Kwa ulinganisho, ni kama kampuni ya CocaCola ingeamriwa kutoa vianzio halisi vya utengenezaji wa kinywaji chake, kwani kampuni shindani kama Pepsi au nyinginezo zinapata taabu kuchukua sehemu 'inayofaa' ya soko la vinywaji baridi, kwa sababu ya ukiritimba wa kampuni moja.

Kianzio muhimu zaidi wanachotumia mawakili wa kampuni hizo ni kuwa programu za kumpyuta inatakiwa 'kuingiliana,' yaani mtu awe na uhuru wa kutumia kwa mfano 'kitafutaji' (browser) ya kampuni moja au nyingine, kwa kompyuta yake ambayo inatumia 'windows,' yaani programu ya Microsoft. Wamepiga kelele sana kuwa watu wanahitaji kununua 'browser' ya Microsoft, hivyo ni kulea ukiritimba, n.k.

Nje ya hicho kitafutaji cha njia tofauti kwenye Internet, ule mtandao wa watoa habari na picha, mikanda au mikunsanyiko ya maandishi, filamu na mengineyo, mengine inaelekea hayapigiwi kelele sana.

Uamuzi wa Umoja wa Ulaya uliambatana na madai ya awali yaliyowahi kufikishwa mahakamani nchini Marekani, ambako Microsoft ilishindwa lakini haikutekeleza maamuzi hayo, hata kama ililipa faini.

Ni hali hiyo inayojirudia Ulaya, na haielekei kuwa hivi sasa faini hiyo inatosha kuibadili Microsoft.

Kwa nchi kama Tanzania suala hilo linaleta picha tofauti mbili, kuwa kiitikadi watu wengi wanaunga mkono juhudi za mahakama au washindani pale makampuni makubwa yanapokuwa yanahusishwa, kwani kwa jadi watu wanaogopa ukiritimba wa makampuni kama hayo.

Kinachosahauliwa ni kuwa ni pale ambapo inatokea kampuni kama hiyo, ikaunda vyombo vya kompyuta ambayo vinaenezwa dunia nzima kwa bei ya chini kabisa ndipo watu wa kawaida (kwa viwango vya mapato ya kimataifa) wanafaulu kununua.

Hata hapa matumizi ya Internet café yamewawezesha vijana wengi kuwasiliana na wenzao walioko ng'ambo kutafuta nafasi za masomo, kazi, wafadhili tarajiwa, n.k. Yako pia maeneo 'hasi' ambako mawasiliano hayo yanakuza uhamiaji wa umalaya, n.k.

Ila kama ilivyo kwa simu za mkononi, ambazo zimerahisisha sana mawasiliano na kukuza biashara kwa kiwango kikubwa, ushindani na kupungua bei kunawezesha karibu kila mtu kuwa na simu ya mkononi akitaka. Tatizo hilo la miingiliano na utumiaji wa vifaa vya aina moja tu hata kwenye simu lipo, kwa mfano huwezi kutumia kifaa cha kurudishia chaji ya umeme cha Nokia kwenye simu ya Motorola, Samsung au Siemens, n.k. Sasa kama mtu ataenda mahakamani kwa hilo, si ataonekana kidogo ana wazimu?

Labda ambacho kinafuatana zaidi na ugomvi kuhusu Microsoft ni kuweka 'line' ya simu katika simu nyingine, kama ni mtandao tofauti, ili kupata mawasiliano au kuboresha mawasiliano kama hayo.

Hapa kinachohusika siyo tena aina za simu kutoka kwa wale watengenezaji,lakini kampuni za kutoa huduma ambazo zinatakiwa 'line' ziingiliane kupunguza matatizo pale mteja anapohitaji kubadili 'line.'
Mtego unaokuja ni kuona kama hili linatakiwa pia kwenye programu hiyo ya 'browser,' au hilo ni suala tofauti.

Ugomvi wa 'browser' ya Microsoft unahusiana kwa kiwango fulani na ugomvi mwingine wa kibiashara uliosikika kwa nguvu katika miaka iliyopita, ingawa sasa unafifia, katika sekta ya kilimo. Unahusu matumizi ya mbegu zenye virutubisho, kuinua lishe kwa watumiaji, lakini mbegu zake inabidi zinununuliwe kwani virutubisho havinakiliwi kikamilifu mbegu zikipandwa, mazao kutokea na kukuza mbegu nyingine.

Harakati zikaanza kote duniani, kwamba wakulima watanyonywa na makampuni ya mbegu hizo.

Wakati mgogoro huo unafukuta karibu kila mahali, na hata hapa nchini katika miaka ya 90 katikati, la kushangaza ni kuwa kilo moja ya mbegu-virutubisho ilikuwa inauzwa shilingi 200 tu, na mkulima alikuwa hahitaji zaidi ya kilo takriban 10 kwa eka moja, kama si pungufu.

Sasa unajiuliza kuwa hivi ni bora zaidi kutumia mbegu za asili za virutubisho haba na madawa ya kupuliza kibao, ambazo zinavunwa shambani, au labda wakulima wahamie mbegu-virutubisho, na kuzinunua dukani kila msimu?

Hivi hilo ni suala gumu sana kufikiri, na kuhitaji maandamano, au ni 'damu mbaya' dhidi ya makampuni makubwa duniani, kuwa yanafaidi? 'Browser' si chombo tu, kama 'mouse'? Sasa kuna haja ya maandamano kuhusu kununua 'mouse' za Microsoft, eti 'kila siku'? Na kama wako wanaotaka 'mouse' zao ziingie sokoni, wakashindwa, lazima kulaumiana?

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.