25 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Elimu zaidi ya TB itolewa kwa umma
 
2008-03-25 09:04:02
Na Mhariri

Jana ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya Kifua kikuu Duniani (TB) ambayo imewekwa maalum ili jamii itafakari na kufikiria njia nzuri zaidi za kupambana na hatimaye kutokomeza ugonjwa huo hatari.

Hata hivyo, kilichojitokeza jana ni maadhimisho haya kuwa kimya sana kiasi kwamba wananchi wengi hawakuwa na habari.

Hii ni tofauti na tunapoadhimisha siku za magonjwa mengine kama Ukimwi.

Katika madhimisho yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam, jana, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kupitia kwa Meya wake, Bw. Jerome Bwanaussi, ilisema inakabiliwa na tatizo la utoro kwa wagonjwa wake walioko kwenye tiba ya dawa za kifua kikuu, hivyo kuchangia idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo sambamba na maambukizi zaidi.

Meya Bwanaussi hakueleza sababu za wagonjwa kutoroka dawa, lakini tunadhani kwamba, pamoja na sababu nyingi zinazohitaji utafiti wa kisayansi, wengine huacha matibabu kutokana na kutodhibitiwa vilivyo na wahusika wanaotoa dawa hizi na mikakati hafifu ya kuwafuatilia majumbani.

Halikadhalika kuna tatizo la elimu ya kutosha kwa wahusika na ndugu zao kuhusu umuhimu wa dawa.

Bila shaka wengine huacha tiba kutokana na ujinga tu wa kukimbilia kwa waganga wa jadi wakidhani wamerogwa.

Tatizo jingine ambalo linaambatana na TB ni wagonjwa kutengwa na ndugu zao hata kama wakiwa wameshaanza dawa
Tatizo jingine ni jamii hivi sasa kuuhusisha ugonjwa wa TB na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi (VVU) kama kaka na dada. Hali hii inawafanya wagonjwa kutokuwa wawazi wanachoumwa na wengine kukataa tiba.

Ingawa ni kweli wenye VVU ni rahisi kupata TB kutokana na kinga kupungua, lakini wataalamu wanatuambia kuwa TB inaweza kumpata mtu yeyote ambaye kinga zake zimepungua kidogo hata kama ni kutokana na lishe duni, magonjwa kama kansa ya damu na matumizi ya dawa fulanifulani kali.

Tunapenda kuungana na Meya Bwanaussi kuishauri jamii kuelewa kwamba hata kama tayari mtu ameshaambukizwa virusi vya ukimwi, kunywa dawa za TB anapona kabisa ugonjwa huo na kumrefushia maisha.

Aidha tunachukua fursa hii pia kuiasa jamii kutowatenga watu wanaogundulika kuwa na TB kwani wataalamu wanatuambia kwamba mgonjwa akishaanza kutumia tiba haambukizi tena.

Katika kupambana na TB tunashauriwa kuishi katika mazingira yenye hewa ya kutosha na kuepuka misongamano isiyo lazima ikiwa ni pamoja na kubanana sana kwenye vyombo vya usafiri.

Tukumbuke, kama alivyosema Meya Bwanaussi, kwamba licha ya TB kudhoofisha mwili wa mgonjwa, unaifanya jamii kuwa maskini kwani wagojwa wengi wanashindwa kufanya kazi zao za kila siku.

Wakati tunaiasa jamii kuhakikisha wagonjwa wa TB wanatibiwa mpaka mwisho kwani mtu hawezi kupona akiacha tiba, tunaomba wahusika, hususan serikali kuweka msukumo kwenye TB kama inavyofanya katika magonjwa mengine ukiwemo Ukimwi.

Hapa tunatazamia kwamba elimu zaidi ya TB itakuwa inatolewa mara kwa mara kupitia njia mbalimbali na tunatazamia maadhimisho ya mwaka kesho yatakuwa na mshindo zaidi.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.