|
Viongozi waliiponza Simba - Mziray
2008-03-26 08:42:58
By Mwandishi Wetu
Kocha wa zamani wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars na Simba, Syllersaid Mziray amesema kuwa `kipigo` cha mabao 4-0 ilichopata Simba kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Enyimba ya Nigeria kilitokana na uzembe wa viongozi.
Mziray alisema kuwa kitendo cha viongozi kushindwa kuwalipia wachezaji wake wawili wa kulipwa vibali vya kufanyia kazi nchini na kusababisha hati zao za kusafiria kuzuiwa na Idara ya Uhamiaji kilichangia kupunguza morali ya wachezaji wengine waliobakia.
Wachezaji hao ambao hati zao zilipatikana jioni huku muda wa saa za kazi katika ofisi za ubalozi wa Nigeria zikiwa zimeshaisha ni Ramadhani Wasso na Moses Odhiambo.
Mziray ambaye haogopi kutoa maoni yake pale anapoona kuna ukweli alisema kuwa ni jambo la aibu kwa klabu ya Simba kuondoka na mchezaji ambaye hakuwa na viza ya kuingia katika nchi wanayokwenda na kuongeza kuwa ni aibu kuendelea kutafuta visingizio vingine.
``Matokeo yale yametokana na uzembe wa viongozi, ni aibu kuzungumzia jambo hilo, unamsajili mchezaji wa nje kwa fedha nyingi halafu unashindwa kumlipia kibali chake,`` alihoji Mziray.
Wakati huo huo, Simba ilirejea nchini jana mchana ikitokea Nigeria na kuingia moja kwa moja kambini kujiandaa na mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara na mchezo wa marudiano uliopangwa kufanyika Aprili 6 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ili Simba isonge mbele inahitaji ushindi wa mabao 5-0 jambo ambalo kwenye soka linawezekana lakini ni lenye nafasi finyu.
|