|
Bunge lichunguze Mkataba wa Kampuni ya Reli Tanzania
2008-03-26 09:36:51
Na John Ngunge
Kwa hakika tangu Serikali ilipoingia mkataba na Kampuni ya Rites ya India kukodisha uendeshaji wa lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kipindi cha miaka 25, kumekuwa na mambo mengi ambayo yanatilia shaka kuhusu mkataba huo ambao yafaa kuchunguzwa kwa makini na Bunge ili kujiridhisha kuwa mkataba huo ni safi na salama.
Hii ni kutokana na ukweli tu kuwa hivi karibuni Kamati Teule ya Bunge, iliyokuwa chini ya Dk Harrison Mwakyembe, ilifanya kazi ya kizalendo ya kuchunguza mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura uliopewa kampuni ya Richmond ili kuliokoa taifa kutokana na janga la ukame na ukosefu wa umeme, ambao ulikuwa unatishia mwenendo wa uzalishaji viwandani na hali halisi ya maisha ya watanzania kwa wakati huo mwaka 2006.
Uchunguzi huo wa kina na uliojaa uzalendo, ulibainisha kuwa kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa taratibu zilizosababisha kampuni isiyo na uwezo wa kuunganisha hata balbu kupewa kandarasi kubwa inayogharimu mabilioni ya fedha za wananchi bila ya sababu za msingi huku ikishindwa sio tu kuzalisha umeme kwa wakati ni pamoja na kushindwa kabisa kuzalisha umeme hata kidogo hadi sasa huku taifa likilazimika kulipia karibu sh milioni 152 kila siku kutokana na mkataba huo uliojaa ujairi wa kifisadi.
Mkataba wa Kampuni ya Reli Tanzania( TRL) ni muhimu sana ukachunguzwa kwa sababu kumekuwa na mambo mengi ambao hayaashirii harufu nzuri katika mkataba huo ambao wananchi wengi walitarajia kuwa utawezesha kuongeza kasi ya uboreshaji wa huduma hiyo, lakini badala yake hali imekuwa ngumu mno kuliko ambavyo ilikuwa chini ya uendeshaji wa serikali kwa wakati huo.
Mabehewa yamekuwa machache sana ambayo baadhi ni mabovu na yanayovuija, huku msongamano wa abiria ukiwa mkubwa sana ambao usalama wao na wa mabehewa ni wa kutilia shaka.
Kwa nyakati fulani imewahi kuripotiwa kuwa, treni imesafirisha abiria gizani au kukwama kusafirisha abiria kwa siku kadhaa katika maeneo mbalimbali hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa abiria wakiwemo wanawake na watoto.
Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni kampuni hiyo imeleta nchini injini chakavu zilizokarabatiwa ambazo zinasemwa kuwa zinakodishwa ili kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za shirika hilo na kwamba baada ya muda fulani wa mkataba zitasafirishwa kurejeshwa zilizokotoka na kuiacha nchi ikiwa patupu.
Tena basi, yasemwa kuwa baadhi ya injini hizo ni mbovu kiasi kwamba zinafanyiwa ukarabati mwingine nchini kabla ya kuruhusiwa kutoa huduma ambayo kuna kila dalili itakuwa ya kusuasua.
Baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni vimeripoti kuwa, baadhi ya vipuri vya hapa nchini vimebebwa na kupelekwa huko kusikojulikana ili vikafanyiwe ukarabati na kurejeshwa nchini katika kuhakikisha kuwa huduma za usafirishaji zinaimarishwa.
Hali hii inaashiria kuwa kampuni hii, kama ilivyokuwa kwa Richmond haina mtaji wa kutosha na hivyo inaokoteza mtaji hapa nchini kwamgobngo wa watanzania.
Sasa basi, kwa kuwa kila dalili zaashiria kuwa kuna ubabaishaji katika mkataba huo, ni muhimu sana Kamati Teule ya Bunge yenye wajumbe wazalendo hasa wakiwemo wanasheria na waandishi wa habari wabunge, ikaundwa na kuuchunguza mkataba huu ili waliohusika kama wapo katika kuiingiza nchi kwenye mikataba mibovu wakajulikana na kuwekwa katika mazingira ya kupima uzito wa hoja na kuamua nini cha kufanya.
Haiwezekani kila siku Kampuni ya reli (TRL) ikawa inatoa visingizio vya kuboresha huduma za usafiri huu ambao ni muhimu na tegemeo kubwa kwa mikoa mingi hapa nchini.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Miundo Mbinu,Dk Makongoro Mahanaga alitangaza kuwa kampuni hiyo, imeongeze muda wa kuboresha huduma toka ule wa awali uliofikiwa kwenye mkataba wa awali hadi miaka miwili ijayo.
Ina maana wakati mkataba huo ulipokuwa unajazwa au kufikiwa hakukuwa na upembuzi yakinifu wa kupata uhakika wa lini huduma hiyo itaboreshwa hadi sasa kuonekana umuhimu wa kuongeza muda? Je kuna nini katika mkataba huo?
Hivi karibuni wafanyakazi wa Kampuni hiyo ya reli, waliandaa mgomo wa kushinikiza maslahi yao yaboreshwe, hali ambayo ilisababisha baadhi ya treni kusimama kwa siku nzima na kuleta adha kubwa kwa abiria waliokuwa katika treni hiyo ikiwemo vituo vya Dar es salaam, Dodoma,Tabora na kwingineko hali ambayo ilisababisha mwekezaji huyo mpya kugwaya na kupandisha mishahara hadi kufikia sh 160,000 ambapo hadi kufikia Agost mwaka huu inatarajiwa kupanda na kufikia sh 200,000 kuwa ni kima cha chini cha mishahara.
Chondechonde Bunge letu kwa kuzingatia maslahi ya nchi na wananchi ni muhimu sana Kamati Teule ikaundwa na kuchunguzwa ili ukweli ubainike.
|