|
Hongera majeshi ya AU Comoro
2008-03-26 09:38:44
Na Mhariri
Makamanda na wapiganaji wa jeshi la Shirikisho la visiwa vya Comoro wakisaidiwa na vikosi maalumu vya Umoja wa Afrika (AU) jana walianza kutimiza awamu ya kwanza ya majukumu waliyokabidhiwa na AU kukikomboa kisiwa cha Anjouan.
Kisiwa hicho, ambacho ni sehemu ya shirikisho la Comoro linaloundwa na visiwa vingine vya Moheli na Ngazija, kimekuwa kikikaliwa kimabavu tangu mwezi Julai mwaka jana na Kanali Mohamed Bakari ambaye alijitangazia utawala mwenyewe.
Uongozi wa muungano wa Comoro chini ya utawala wa Rais Ahmed Sambi, ukiungwa mkono na AU ulilaani vikali kitendo cha Kanali Bakari kujitangazia Urais mwenyewe na kuazimia kwa pamoja kuwa kilikuwa ni kitendo cha uasi.
AU kwanza iliamua kutumia njia za kidiplomasia na kuitisha jumla ya vikao 12 vya mazungumzo ya kutaka kurejeshwa hali ya amani kisiwani Anjouan ili hatimaye kufanyike uchaguzi huru na wa haki.
Baadhi ya vikao hivyo vilifanyika nchini Afrika Kusini, Ethiopia na Anjouan kwenyewe ambapo katika vikao vyote hivyo, Kanali Bakari alionyesha ukaidi na kiburi cha wazi kupinga kuachia madaraka kwa njia ya amani ili kupisha uchaguzi huru.
Jitihada za kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Anjouan ili Kanali Bakari aachie ngazi vilishindikana baada ya AU kubaini kuwa bandari pekee inayotumika na visiwa vyote vya Comoro ipo kisiwani Anjouan, hivyo vikwazo vingeviathiri zaidi visiwa vya Ngazija na Moheli na siyo Anjouan.
Kama hiyo haitoshi, AU ilimpa nafasi ya mwisho Kanali Bakari kwa kutoa siku tisa za kujisalimisha pamoja na askari wake wanaokadiriwa kufikia 300 lakini kwa jeuri kubwa aligoma kusalimu amri.
Ndipo AU ikafikia hatua ya tatu ya kuamua kutumia nguvu za kijeshi ili kuwarejeshea amani wananchi wa Anjouan kuweza kumchagua kiongozi wao.
Kitendo kilichofanywa na vikosi vya Comoro kwa kusaidiana na askari ya jeshi maalumu la AU ni kwa misingi ya kuwasaidia wananchi wa Anjouan kuweza kuimarisha muungano wao na kuondoa utawala wa kidikteta ulioongozwa na Kanali Bakari.
Bado tunakumbuka jinsi kiongozi huyo alivyowatia korokoroni baadhi ya viongozi na raia wa kawaida mara baada ya kujitangazia utawala wake wa mabavu mwaka jana.
Kiutawala kila kisiwa katika muungano wa Comoro kina Rais wake, huku Rais wa Muungano akichaguliwa baada ya kufanyika chaguzi kwenye visiwa vyote vitatu.
Wakati visiwa vingine vilikwishakamilisha chaguzi zake za kumpata Rais, Kanali Bakari kwa sababu zake za kidikteta aliamua kufanya uchaguzi haramu usiokuwa na wasimamizi na kujitangazia ushindi visivyo halali mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema mwezi huu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Benard Membe alisema kwamba operesheni ya kukikomboa kisiwa cha Anjouan iliandaliwa kisayansi kwa madhumuni ya kutoleta madhara yoyote kwa wananchi na mali zao.
Hii ndiyo hali iliyojitokeza ambapo hadi jana tulipokuwa tunakwenda mitamboni hapakuwepo na taarifa zozote za vifo, majeruhi au uharibifu wowote.
Tunawapongeza makamanda na wapiganaji wote ambao wameshiriki katika kazi hii muhimu yenye madhumuni ya kutetea haki za binadamu duniani na amani kisiwani Anjouan.
Tunaelewa kwamba suala la kumpata kiongozi
bora kisiwani Anjouan ni la wananchi wa Anjouan wenyewe.
Na jukumu hilo tunawaachia waamuwe wenyewe.
Hata hivyo, Kama alivyosema Waziri Membe ,vikosi vya AU vitaendelea kuwepo Anjouan hadi mwezi Mei mwaka huu, tukiwa na imani kwamba nidhamu na ukakamavu waliouonyesha tangu wafike Comoro utasaidia kulijenga jeshi jipya la Comoro na kuwawezesha wananchi wa Anjouan kuondoa tofauti walizonazo na kuungana ili kujenga taifa lenye umoja na mshikamano.
|