|
Utafiti wa mitandao ya kuhifadhi mazingira katika mazao misitu uungwe mkono
2008-03-27 08:32:15
Na Mwandishi Wetu
Ipo misemo mingi ya uhifadhi Mazingira na huleta ujumbe mzuri kwa wadau wa kutunza na kuhifadhi mazingira, misemo kama ``Tunza mazingira uongeze Mapato`` na ``Mazingira ni uhai`` huleta ufanisi na ujumbe mzuri katika suala zima la uhifadhi wa mazingira kwa wadau wote.
Katika Mkoa wa Morogoro, Wilayani Kilosa Mitandao mitano imefanya utafiti kuhusu mazao yasiyo Timbao ambayo yanapatikana misituni .
Timbao ni mazao yote yanayopatikana ndani ya misitu pasipo kuathiri misitu au kwa lugha nyingine yanaitwa (Non-Timber Forest Product).
``Mazao haya hayawezi kuathiri suala zima la uharibifu wa misitu kwa namna yoyote pia ni njia nzuri kabisa ya kufaidika na misitu bila ya kuathiri,`` anasema ofisa Habari wa programu ya kuzijengea uwezo asasi za kiraia ngazi ya pili (CBOs) katika usimamizi shirikishi wa misitu (EMPAFORM) Bi. Secelela Balisidya.
Programu ya EMPAFORM inaendeshwa katika nchi za Afrika Mashariki na kwa hapa nchini inaratibiwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili yaani (TFCG).
Bi Balisidya anasema alitembelea mitandao mitano ya MJUMITA iliyopo wilayani Kilosa, mkoani Morogoro na kuifanyia utafiti kuhusu mazao yasiyo Timbao kama wanayafahamu kwa kina.
Utafiti huo ambao ulilenga kufahamu na kutambua kama mwananchi wa kawaida au mkulima endapo anafaidika na mazao yasiyo timbao, na ni namna gani ambavyo anayatumia kunufaika na hayo mazao.
Utafiti huo ulifanyiwa na Mitandao ya AZIMIO uliopo kata ya Gairo,RUBEHO uliopo kata ya ukwimage,WAMAJUKUU uliopo kata ya Kilosa mjini.
Mitandao mingine iliyofanyiwa utafiti ni SITETIANA uliopo kata ya Ulaya na mtandao wa HIMAVIKIRU uliopo kata ya Mikumi.
MJUMITA ni Shirikisho la Mitandao ya Jamii ya Usimamizi wa Misitu ambalo hufanya kazi kwa kuwaunganisha wanajamii wanaoishi kando ya misitu.
Programu ya EMPAFORM inafanya shughuli zake kupitia shirikisho hilo kwani ndilo lenye mitandao inayofika katika ngazi ya chini kabisa ya jamii, hivyo walengwa kunufaika moja kwa moja.
Mazao yaliyotajwa kuwa siyo timbao ni asali mianzi, mbegu, matunda poli, udongo wa mfinyanzi, kuni,samaki, ukindu, dawa za asili, nyasi za kuezekea nyumba pamoja na uyoga kama kitoweo.
Ingawa mazao yaliyotajwa ni baadhi tu ya yaliyofanyiwa utafiti, lakini utafiti huo ulikuwa unalenga kujua asali inazalishwa kiasi gani katika mitandao na wanafaidika nayo vipi, jinsi gani wanahifadhi kwa kiwango cha ubora unaotakiwa katika ushindani wa kibiashara.
Kulingana na utafiti huo wa mitandao yote ya MJUMITA, kiwango cha uzalishaji asili hakikutofautiana sana, ikiwemo kipato, gharama, na matatizo yote pamoja na jinsi ya kurina na kuhifadhi.
Utafiti ulibaini kuwepo kwa matatizo ya masoko na vifaa vya kutumia wakati wa kurina asali hususani mavazi ya kuvaa wakati wa kurina, vyombo vya kuchujia kiutaalamu na vyombo vya kuhifadhia.
Maeneo yote yaliyofanyiwa utafiti yameonyesha kuwa, wafuga nyuki wameanza kubadilika na kutengeneza mizinga ya kisasa ambayo hutoa asali kwa wingi na kuachana na ile ya zamani ambayo ilikuwa ikitoa asali kidogo.
Katika mtandao wa AZIMIO, kata ya Gairo, katibu wa mtandao huo Bw.Adoni S.Sehaba alisema wana mizinga ya kisasa 75 na mizinga 982 ambayo ni ya asili.
Bw. Sehaba alisema kuwa, uzalishaji umeongezeka katika kata hiyo na mwitikio wa wafugaji pia umekuwa mkubwa kuanzia mwezi Mei mwaka jana hadi sasa.
Pamoja na hayo ameongeza kuwa kinachowakatisha tamaa ni soko la kuuzia asali hiyo.
Akabainisha kuwa wafugaji nyuki hukosa soko na kuamua kuwauzia watengeneza pombe za asili au kutembeza mtaani na kuuza kwa bei ndogo.
Wafugaji hupeleka asali yao katika sehemu za Kibaigwa au Gomani ambapo huuza kwa shilingi elfu moja kwa lita bei ambayo ni ndogo kulinganisha na gharama .
Gharama halisi za kutengeneza mizinga katika mitandao yote ni kati ya shilingi 25,000 hadi 40,000 .
Pamoja na matatizo hayo kipato cha mrina wa asali kinakadiriwa kuwa ni kikubwa ambapo mfugaji nyuki anaweza kupata zaidi ya shilingi laki mbili tofauti na wengine.
Mkazi ambaye anajishugulisha na kazi za vitunga nyungo na mikeka anaweza kupata kiasi cha Sh.80,000 hadi Sh.100,000 kwa mwezi, ambapo anajishugulisha na uvuvi anaweza kuingiza kiasi cha Sh. 150,000.
Sekta ya nyuki ndio yenye kuonyesha mafanikio na kuleta matumaini miongoni mwa wafugaji wa nyuki ndani ya mkoa wa Morogoro, ambapo mfugaji nyuki anaweza kuwa na mizinga zaidi ya 150 na anaweza kujipatia kiasi cha lita 200 za asali.
Bw.Sebaba anasema wapo wafugaji ambao wamekua ni mfano mzuri na wa kuigwa katika mitandao hiyo.
Utafiti huo ulishuhudiwa na baadhi ya viongozi ambao ni Bw. Vitusi Membo ambaye ni katibu Mtendaji wa MJUMITA pamoja na Bi. Juliana Mwenda ambaye ni mweka hazina wa MJUMITA na pia ni Diwani wa Gailo, serikali iliwakilishwa na Mwakilishi wa bwana nyuki wa wilaya ya Kilosa , Edward Mkumbo.
Pamoja na kuambatana nao kwa ukaribu viongozi hao walikuwa ni chachu ya kutia changamoto mbalimbali katika mitandao yote ikiwemo kutoa hamasa kwa vikundi hivyo.
Viongozi hao wakawaomba wafugaji wasife moyo katika zao la asali na kuahidi kuwa matatizo yote ya ukosefu wa masoko pamoja na wadudu waharibifu wanaosumbua mizinga nayo yanatafutiwa mwafaka ikiwemo vifaa.
Hata hivyo,jitihada zimeanza kuonekana kwani serikali na wadau wamekuwa wakisaidia sekta hiyo.
Mitandao kadhaa imepata misaada ya mizinga kutoka asasi mbali mbali ambapo mtandao wa MAJUKUU umepokea msaada wa mizinga 100 kutoka TASAF, Mtandao wa HIMAVIKIRU wamepokea mizinga ya kisasa 30 kutoka asasi ya WWF yote ikiwa ni ya kisasa.
EMPAFORM kupitia mradi wake wa MJUMITA umetoa mafunzo mbalimbali katika mitandao mingi ya kuhifadhi mazingira hapa nchini, lakini kuna matatizo yanayowakabili wananchi wa maeneo husika ikiwemo suala la kipato, elimu juu ya suala la uelimishaji wa kutosha katika maeneo husika, wadudu waharibifu kama mnyama aitwaye Nyegere na tatizo la masoko.
Watalaam wa masuala ya misitu wanasema zao la timbao linaweza kubadilisha hali ya wananchi kiuchumi pasipo kuathiri misitu.
Zao la timbao litakuwa mkombozi wa kila mkazi katika eneo husika, Mitandao yote mkoani Morogoro kupitia MJUMITA itanufaika kutokana na utafiti huo wa ufugaji nyuki,ikiwemo mazao yote yaliyotajwa kuwa hayawezi kuathiri misitu.
Utafiti huo umegundua yapo mazao ambayo yameonyesha kuwa na uwezo wa kumwingizia kipato kikubwa kutokana na mazao hayo ya msituni,mazao hayo yaliyotajwa kama chachu ya kujikwamua na umasikini.
Mazao hayo ni mianzi, samaki, milala, pamoja na ukindu ambayo hutumika kutengenezea vitunga, nyungo ambavyo ni vitendea kazi katika jamii nzima, ikiwemo samaki ambayo hutumiwa kama kitoweo.
Kilio cha wafuga nyuki wengi mkoani Morogoro ni juu ya masoko ya bidhaa zao hususan zao la asali ambalo limeonekana ni zao linalozalishwa kwa wingi na lenye kuweza kumwondolea umasikini Mwananchi wa kawaida kwani mpaka sasa hakuna mwenye soko la uhakika na bidhaa zake.
Wameomba wadau mbalimbali kutoka ndani na nje wajitokeze kusaidia juu ya bidhaa zao ambazo sio timbao.
|