27 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Tuwe waangalifu katika wakati huu wa mvua
 
2008-03-27 08:33:17
Na Mhariri

Mvua za masika tayari zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni faraja kubwa kwa wananchi wanaoitegemea kwa ajili ya uzalishaji mali na hasa sekta ya kilimo.

Zipo sehemu ambazo wakulima walianza kukata tamaa katika miezi ya hivi karibuni kufuatia kipindi kirefu cha jua kali na ukame.

Bila shaka, wakulima ambao wameyaandaa mashamba yao vizuri, watazitumia mvua hizi ili kuweza kupanda mazao mbalimbali ya biashara na chakula.

Serikali hivi karibuni ilitangaza jinsi ambavyo baadhi ya maeneo nchini yanavyokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Hiki ni kipindi ambacho viongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia vijijini, wilayani hadi mkoani wakajikita zaidi katika kuwahamasisha wananchi kuzitumia mvua kulima mazao mbalimbali hasa yale yanayokomaa haraka katika maeneo yenye uhaba wa chakula.

Kwa upande mwingine, historia inaonyesha kwamba mvua za masika mara nyingine zimekuwa na madhara makubwa endapo tahadhari hazichukuliwi.
Tunachukua fursa hii kuwatahadharisha wananchi ambao bado wanang\'ang\'ania kuishi katika sehemu hatari za mabondeni ambazo ni rahisi kukumbwa na mafuriko.

Itakumbukwa kwamba mara kadhaa, mathalani, serikali katika Mkoa wa Dar es Salaam imekuwa ikiwahimiza wakazi wa maeneo ya mabondeni, hasa katika bonde la Msimbazi, kuyahama makazi hayo ambayo siyo salama hasa nyakati kama hizi za mvua kali.

Lakini kinachojitokeza ni wakazi hao kusema kwamba hawana sehemu nyingine za kwenda, hata kama makazi hayo ni hatari kwa maisha na mali zao.

Waswahili tumezoea kusema kwamba `tahadhari ni bora kuliko ajali`, tukisisitiza kwamba wanaoishi maeneo hatari, mijini na vijijini ni budi kuyahama makazi hayo ili kunusuru maisha yao.

Hatutarajii kusikia wananchi wakikumbwa na mafuriko kwa kujitakia wenyewe halafu wahitaji kupata misaada kutoka kwa wahisani au serikali.

Halikadhalika, tahadhari ni lazima ichukuliwe na wanaomiliki na kuendesha vyombo vya usafiri kama magari na usafiri wa majini kuwa makini zaidi katika kuzingatia sheria za usalama ili kujiepusha na ajali.

Yapo maeneo nchini ambayo barabara zake ni hatari mno kutokana na uharibifu unaotokana na mvua au utelezi wa udongo wake, ambapo madereva wanatakiwa kuwa waangalifu zaidi.

Wananchi nao wanalazimika kupunguza safari zisizokuwa na ulazima wowote hasa mikoani, katika maeneo ambayo barabara zake zina sehemu korofi ambazo zinaweza kulazimisha magari kukwama kwa muda mrefu na hivyo kuleta usumbufu mkubwa kwa abiria.

Tunaamini kwamba kila mmoja atajitahidi kuchukua tahadhari zinazostahili katika kujihadhari na ajali, huku wakulima nao wakizitumia mvua hizi vizuri kwa ajili ya kuzalisha mazao ya chakula na biashara.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.