27 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wafanyakazi kuandamana kupinga bei ya umeme
 
2008-03-27 08:36:55
Na Thobias Mwanakatwe, PST Mbeya

Zaidi ya wafanyakazi 10,000 wa mkoani Mbeya, wamepanga kuandamana Jumamosi hii kwa kuvishirikisha vyama vyote vya wafanyakazi nchini kupinga pendekezo la Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) la kuongeza bei ya umeme.

Tamko la kufanyika kwa maandamano hayo, lilitolewa jana kwenye Mkutano Mkuu wa viongozi wote wa matawi kutoka vyama shiriki vya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (TUCTA) uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Wafanyakazi jijini Mbeya.

Mkutano huo uliowajumuisha wajumbe kutoka wilaya zote za mkoa huo ambao kwa kauli moja walikubaliana kuandamana ili kupinga nia ya Tanesco kuongeza tena bei ya umeme na kuwaongezea wananchi ukali wa maisha.

Wajumbe wa mkutano huo walisema katika maandamano hayo watashinikiza pia wale wote waliohusika kwenye kashfa ya mikataba mibovu ya umeme kushughulikiwa haraka badala ya siasa za vyama kuingizwa kwenye masuala mazito ya kitaifa na kuwaacha wananchi wakiendelea kuumia.

Mratibu wa mkoa wa TUCTA, Bw. Thomas Kasombwe, alisema kuwa uamuzi huo wa kuandamana kwa amani wameona kuwa ndiyo njia pekee itakayoweza kuifikishia ujumbe serikali kuwa wakati wa mafisadi kuendelea kuitafuna nchi unaelekea kikomo.

Alisema mbali ya kuitaka serikali isitishe mara moja ulipaji wa fedha hizo kwenye kampuni hewa ya Richmond kwa upande mwingine waliipongeza serikali kwa hatua iliyochukua ya kuanza kushughulikia suala la kampuni hiyo na kutaka wote waliohusika kuchukuliwa hatua kali.

Kasombwe alisema kuwa maandamano hayo makubwa na ya aina yake yatahudhuriwa na wananchi wa kawaida ambao kwa kiasi kikubwa ndio waathirika wa kwanza hasa ikilinganishwa kuwa vipato vyao ni vya chini na hawawezi kumudu kabisa kuendelea kulipia gharama kubwa za umeme.

Mgeni rasmi katika maandamano hayo atakuwa Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Taifa Bw. Nicolaus Mgaya, atakayepokea maandamano yao katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine pia yataongozwa na vikundi kadhaa vya burudani.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.