27 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

JK azindua TBC na kuhimiza maadili kwa waandishi
 
2008-03-27 08:39:07
Na Mwandishi Wetu

Rais Jakaya Kikwete, amewahimiza waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kufuata maadili ya taaluma kwa kuandika habari za pande mbili na za uhakika.

Aliyasema hayo jana wakati akizundua rasmi Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) jijini Dar es Salaam.

Rais Kikwete alisema waandishi wanapaswa kuandika habari za kweli, sahihi na za pande mbili na kwamba kwa kufanya hivyo jamii itawaamini.

``Tumieni kalamu zenu kwa hekima, msizitumie kubomoa na kusababisha migogoro katika jamii… Vyombo vya habari vina nafasi nyeti hivyo kazi zenu mzifanye kwa kufuata maadili,`` alisema.

Aidha, Rais Kikwete alisema kuna umuhimu kwa wamiliki na waandishi wa habari kusimama imara kuhakikisha maadili ya taaaluma hiyo hayakiukwi ili isipoteze mwelekeo.

Alisema endapo watawaacha baadhi ya waandishi wa habari wanaotumia taaluma hiyo kufanya utapeli (makanjanja) kuendelea kuitia doa taaluma hiyo itakuwa vigumu kuirejeshea heshima yake kwa jamii.

``Mimi naipenda sana taaluma ya habari, msiiache mikononi mwa `makanjanja`, mkiwaachia wakaiharibu mtashindwa kuirejesha kwenye mstari,`` alisema.

Alisema serikali kwa upande wake itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na kuendeleza taaluma hiyo ili waandishi wawe na elimu ya kutosha.

Vile vile, Rais Kikwete alisema waandishi wa habari wanapaswa kuandika pia habari za maendeleo vijijini badala ya zile zinazowahusu viongozi pekee.

Alisema habari nyingi zinazoandikwa kwenye magazeti ni zile za mijini hasa zinazohusu viongozi, semina na makongamano.

``Ni mara chache sana kusikia habari za vijijini, ukisikia habari ya vijijini basi jua zinahusu maafa, njaa na mauaji ya kishirikina lakini zinazohusu maendeleo haziandikwi,`` alisema Rais Kikwete.

Alisema hata vijijini kuna habari za kufurahisha zinazohusu maendeleo ambazo alisema waandishi sasa waanze kuzipa kipaumbele.

Alisema kutopewa kipaumbele kwa habari hizo za vijijini si dalili njema kwa mustakabali wa Taifa, kwani nazo zina umuhimu katika ustawi wa jamii na ni kutowatendea haki wananchi wa huko.

Rais Kikwete aliwataka waandishi kuachana na fikra kuwa habari nzuri ni zile zinazowahusu viongozi au watu wa mijini.

``Mara nyingi mnasema mnafanya hivyo kwa kuwa soko lenu kubwa liko mjini lakini nawahakikishia hata kule vijijini soko lipo, mkiwapelekea magazeti watayanunua,`` alisema.

Mapema Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Bw. George Mkuchika alisema Shirika hilo litakuwa mstari wa mbele kuandika na kutangaza habari zilizo sahihi,zitakazoisaidia kujenga umoja wa kitaifa na kulinda maslahi ya taifa kwa kuwafichua wote wanaotumia nafasi zao za uongozi kulihujumu taifa.

Aidha aliviasa vyombo vya habari nchini kufanya kazi zao kitaalamu na kwa ufanisi mkubwa ili walinde heshima ya taaluma yao na taifa kwa ujumla.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache saba Afrika ambazo zimejaliwa kuwa na uhuru wa vyombo vya habari, na akawataka waandishi wote wazalendo kuulinda uhuru huo na kuutumia vizuri bila kuvuka mipaka.

Hata hivyo, alisema serikali haina nia wala haipendi kukiadhibu chombo cho chote cha habari, ama mwanahabari yeyote pasipo sababu za msingi.

``Lakini pale inapobidi, hatua sahihi na madhubuti zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo,`` alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TBC, Bw. Tido Mhando alisema shirika lake kwa sasa litakuwa likijitegemea kutokana na vyanzo vyake mbalimbali vya mapato badala ya kuitegemea serikali.

Alisema mbali na kubadilisha jina, shirika hilo limefanyia marekebisho vipindi vyake ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya wasikilizaji.

Bw. Mhando alisema shirika hilo linatarajia kuzindua vituo 11 vya radio vitakavyokuwa vikitumia masafa ya FM katika mikoa mbalimbali.

``Tunatarajia kupanua huduma zetu hadi Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya hadi ifikapo mwaka 2015.``

Alisema TvT kwa sasa itakuwa ikijulikana kama TBC 1, Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) itakuwa ikijulikana kama TBC-Taifa.

Pia alisema kutakuwa na TBC International itakayokuwa ikirusha matangazo yake kwa muda wa saa 12 kwa lugha ya Kiingereza na muda wa saa mbili kwa lugha ya Kifaransa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Nchini (MOAT), Bw. Reginald Mengi, aliunga mkono kauli ya Rais Kikwete ya kuwataka waandishi kuandika kwa kuzingatia kanuni na maadili ya taaluma yao.

Bw. Mengi ambaye ni mmoja wa wageni mashuhuri waliohudhuria hafla hiyo, alisema kuna umuhimu kwa waandishi wa habari kuhakikisha habari wanazoandika zinakuwa za pande mbili.

``Lazima tuzingatie maadili na kanuni za taaluma na tusipofanya hivyo tutayumba na tutaachana na uandishi wa kweli na kufanya uandishi wa kubabaisha,`` alisema Bw. Mengi.

Alisema endapo maadili na kanuni zitafuatwa, waandishi watairejesha taaaluma hiyo katika hadhi yake.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.