27 Mar 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wahanga wa Tabata Dampo kuandamana na CHADEMA leo
 
2008-03-27 08:40:20
Na Romana Mallya

Zaidi ya wahanga 400 waliobomolewa nyumba zao katika eneo la Tabata Dampo jijini Dar es Salaam leo wanaungana na CHADEMA katika maandamano ya kuishinikiza serikali kuwalipa fidia.

Maandamano hayo pia yanapinga ubomoaji huo wanaodai ulifanyika kinyume na taratibu na kutokuwa na imani na Tume iliyoundwa kuchunguza madai yao baada ya zoezi la kubomoa nyumba zao.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam katika mahema wanayojihifadhi, Mwenyekiti wa wahanga hao, Bw. Said Masoud, alisema wataunga mkono maandamano hayo kwa nia njema.

``Kama maandamano hayo ni kwa ajili ya kututetea tutayaunga mkono lakini kama CHADEMA wanataka kututumia kujipandisha kisiasa hatutawaunga mkono,`` alisema.

CHADEMA kimeandaa maandamano hayo yatakayoishia Ikulu ili kuishinikiza serikali kuwalipa fidia ya nyumba walizobomolewa.

Kuhusu kutokuwa na imani na Tume, Bw. Masoud alisema, yeye na wenzake wanne walipoitwa kuhojiwa walipewa vitisho badala ya kuulizwa taarifa mbalimbali kuhusiana na zoezi hilo.

Alisema Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Nchimbi alianza kumwambia kwamba yeye ni Mpemba, sio mmoja wa watu waliobomolewa nyumba na kwamba sio mkazi wa Tabata Dampo.

Bw. Masoud alisema, hakuna kitu chochote walichohojiwa na kukijibu bali waliambulia kupewa maneno ya kejeli.

Alimtaka Jaji Nchimbi kufanya kazi hiyo kwa haki kama alivyoagizwa badala ya kutaka kuingiza mambo mengine yasiyohusiana na sakata hilo.

Wakati huo huo, Nipashe ilishuhudia watu hao wakiwa wamekaa kwa kukata tamaa huku wakiendelea kunyeshewa na mvua za jana.

Mwenyekiti huyo alisema, hivi sasa baadhi yao wakiwemo watoto wamepewa hifadhi katika msikiti uliopo jirani na mahema yao.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzake, Bi. Consolata Peter, alisema jana walipika kwa shida kutokana na sehemu iliyozungushishiwa mahema kujaa maji.

Alisema kutokana na hali ya mvua walishindwa kupika chakula cha mchana na hivyo kuwalazimu kutumia muda mrefu kupuliza moto huku maji yakiwa yanawasumbua.

Aliomba serikali kufanya haraka kuwalipa fidia ili waweze kupata sehemu za kuishi kwani wanaishi maisha ya tabu huku wakiwa na watoto.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo hivi sasa wanawake wametengana na waume zao sehemu za kulala kwani wanaume wanalala peke yao na wanawake sehemu yao.

Wakati huo huo, Polisi jijini Dar es Salaam imeyaruhusu maandamano ya CHADEMA yanayotarajia kufanyika leo kuishinikiza serikali kulipa fidia familia 96 za Tabata Dampo, jijini.

Maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika saa 7:00 mchana, yatakayoanzia Tabata Dampo hadi Ikulu.

Kaimu Kamishna wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Liberatus Barlow, aliiambia Nipashe jana kwa njia ya simu kuwa, hawana nia ya kuzuia maandamano hayo, isipokuwa walikaa kikao na viongozi wa CHADEMA ili waweze kuafikiana njia watakazotumia katika maandamano hayo.

``Tumeruhusu CHADEMA kufanya maandamano, tulikaa nao na tumewataka waende waafikiane njia watakazotumia ili watuletee taarifa mapema tuweze kushirikiana,`` alisema.

Kamanda Barlow, alisema awali walipokea barua kutoka chama hicho ya kuomba kufanya maandamano hayo ambayo yataanzia Tabata Dampo kuelekea Ikulu.

Alisema chama hicho kiliomba maandamano hayo ili kuelezea uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu waliofanyiwa wakazi wa eneo la Tabata Dampo.

Wakati chama hicho kimekubaliwa kufanya maandamano hayo, Tume iliyoundwa kuchunguza sakata la bomoa bomoa hiyo iliongezewa muda wa kufanya kazi yake.

Hatua hiyo imekuja baada ya Tume hiyo kutoa ombi la kuongezewa muda kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Steven Wassira.

Hata hivyo, wakati juhudi zaidi zikifanywa na Tume hiyo misaada mbalimbali ya chakula imekuwa ikitolewa kwa wakazi hao ili kuweza kujikimu kimaisha.

Serikali pia iliwapa `ofa` wahanga hao ya kuhamia katika shule ya Msingi Kipawa ili kujikinga na mvua za masika ambazo zimeanza kunyesha lakini wameikataa.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.