|
Waasi wauawa Anjouan
2008-03-27 08:42:07
Na MORONI, Comoro
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) jana lilikuwa katika siku ya pili kuwaongoza wapiganaji na makamanda wa Comoro wanaoungwa mkono na askari wa jeshi maalumu la Umoja wa Afrika (AU) huku ikiarifiwa kwamba askari watatu watiifu kwa Kanali Mohamed Bacar wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa, limeandika Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, jana.
Vikosi hivyo vya AU na Comoro juzi viliendesha operesheni maalumu ya kijeshi ijulikanayo kama `Operesheni Demokrasia` ambayo ilikomboa sehemu kubwa ya kisiwa cha Anjouan, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege na bandari.
Juzi kulikuwa na taarifa kwamba Kanali Bacar ambaye mwezi Julai mwaka jana alitangaza utawala wa mabavu kisiwani humo alionekana akiwa amevalia nguo za kike akijaribu kutorokea kisiwa jirani cha Mayotte kwa kutumia boti ndogo.
``Jeshi la Maendeleo ya Taifa linaendelea kumsaka Kanali Bacar katika maeneo yote ambayo tunadhani anaweza kuwa amejificha, tofauti na maeneo ambayo alionekana jana,`` Msemaji wa Rais wa Masuala ya Kijeshi, Mohamed Bacar Dossar aliliambia Reuters jana.
Reuters lilisema kwamba magari kadhaa ya kubebea wagonjwa yaliweza kuonekana jana yakiwapeleka majeruhi wa jeshi linalomuunga mkono Kanali Bacar hospitalini.
Msemaji wa serikali ya Shirikisho la Comoro, Abdourahim Said Bacar alisema serikali yake inatarajia kuunda serikali ya mpito kisiwani Anjouan kabla ya kumalizika wiki hii kwa ajili ya kufanya maandalizi muhimu ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu huru ndani ya miezi miwili hadi mitatu.
Alisema kwamba vikosi vya AU vitaendelea kuwepo Anjouan hadi utakapofanyika uchaguzi mkuu kisiwani humo.
Reuters lilisema jana kwamba pamoja na vikosi vya AU kupata ushindi laini juzi, palikuwepo na ushindani mdogo kutoka askari watiifu kwa Kanali Bacar.
``Askari wa Kanali Bacar wamejificha msituni na tuna wasiwasi mkubwa kwamba kama hawatakamatwa wanaweza kurejea usiku na kulipiza kisasi,`` alisema Roukia Halidi ambaye ni mkazi wa mji mkuu wa Mutsamudu kupitia kituo cha redio cha taifa.
Nchi za Marekani na Ufaransa zimeunga mkono operesheni hiyo ambayo imeongozwa na AU huku zikiituhumu Afrika Kusini kwa msimamo wake ambao umetaka kufanyike njia za kidiplomasia badala ya kijeshi.
Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini juzi alisema kwamba matumizi ya nguvu za kijeshi yanairudisha Comoro katika hali iliyokuwepo miaka mingi iliyopita na kushauri kwamba mgogoro huo ungemalizwa kwa majadiliano.
Msemaji wa serikali ya Comoro, Bw. Bacar alisema kwamba nchi yake imesikitishwa mno na kauli ambayo imetolewa na Rais Mbeki.
``Kauli yake inapingana na maamuzi ya AU na hasa Baraza la Ulinzi na Usalama na maamuzi yaliyofanywa na mawaziri wa mambo ya nje, Afrika Kusini,`` alieleza Bacar.
Wakati huohuo, Shirika la Habari la Uingereza, BBC jana jioni lilisema kwamba Makamu wa Rais wa serikali ya Shirikisho la Visiwa vya Comoro, Ikililou Dhoinine ameteuliwa kuwa kiongozi wa serikali ya mpito kisiwani Anjouan hadi kutakapofanyika uchaguzi mkuu.
``Ikililou Dhoinine ndiye atakayekuwa kiongozi mkuu wa kisiasa katika serikali ya mpito kisiwani Anjouan hadi kutakapofanyika uchaguzi mkuu,`` msemaji wa serikali kisiwani humo aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) jana.
Shirika hilo lilisema jana kwamba bado kulisikika milio ya risasi kisiwani humo wakati vikosi vya AU vikishirikiana na askari wa Comoro walipoendelea kumsaka Kanali Bacar na askari wake jana.
AFP lilisema kwamba makazi ya Kanali Bacar na ofisi yake Ikulu kulikuwa kumetelekezwa kabisa jana.
Mkuu wa Majeshi wa Comoro, Mohammed Desara alikaririwa na BBC jana akisema kwamba askari wake na wale wa AU walikuwa wakiendelea na kazi ya kuyashika maeneo yote ya kisiwa hicho.
Msemaji wa serikali ya Comoro, Bw. Bacar alithibitisha uteuzi wa Ikililou na kusema kwamba serikali ya mpito itaundwa rasmi wiki hii na kiongozi huyo mpya wa Anjouan alikuwa njiani kwenda mji mkuu wa kisiwa hicho, Mutsamudu.
Wakati huo huo, Lucy Lyatuu anaripoti kwamba Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange ameyapongeza Majeshi ya Umoja wa Afrika (AU) kwa kukamilisha awamu ya kwanza ya kukikomboa kisiwa cha Anjouan.
Kisiwa hicho kilikuwa chini ya majeshi ya muasi Kanali Mohamed Bacar Jenerali Mwamunyange alitoa pongezi hizo jana jijini Dar es Salaam wakati akiongea na makamanda wa JWTZ katika makao makuu ya jeshi kuhusu hali ilivyo katika visiwa hivyo.
Alisema kisiwa cha Anjouan kilikombolewa juzi na majeshi ya AU kutoka nchi za Comoro, Sudan na Tanzania.
Aliongeza kuwa kwa sasa kisiwa hicho kipo katika mamlaka ya serikali ya Muungano wa Comoro inayoongozwa na Rais Ahmed Sambi.
Jenerali Mwamunyange, alisema wanajeshi wa AU walipokelewa kwa shangwe na wananchi wa kisiwa cha Anjouan, tangu walipowasili na kuanza operesheni ya kukikomboa kisiwa hicho hali iliyoonyesha kuwa wananchi walichoka na utawala wa Kanali Bacar.
Aliongeza kuwa hadi sasa majeshi ya AU kutoka Comoro, Sudan na Tanzania yaliyomo kisiwani humo yapo salama na yanaendelea kuwasaka wafuasi wa Kanali Bacar, katika maeneo mbalimbali ya kisiwa hicho wakisaidiwa na wananchi.
Hata hivyo, alisema hali imeanza kurejea katika utulivu.
Alitoa wito kwa wananchi wa Tanzania kutokuwa na wasiwasi kuhusu hali ya usalama ya wanajeshi wao kwa kuwa operesheni hiyo imefanikiwa vizuri na inaungwa mkono na wananchi wa visiwa vya Comoro.
|