|
Uangalifu uwepo wakati wa kumjadili Bw. Andrew Chenge
2008-04-20 11:46:57
Na Simon Mhina
Watanzania wameombwa kuacha Pupa na jazba wakati wa kumjadili waziri wa Miundombinu Bw. Andrew Chenge anayetuhumiwa kujilimbikizia mabilioni ya shilingi huko ughaibuni.
Vinginevyo, imeelezwa kuwa jazba, pupa na ushabiki vikipewa nafasi watanzania watakosa ``mwana na maji moto``.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya awamu ya kwanza na pili Bw. Venance Ngula, alisema haoni ajabu Bw. Chenge kumiliki dola milioni moja sawa na zaidi ya Shilingi bilioni moja.
Vilevile Bw. Ngula ambaye kitaaluma ni Mchumi, alisema sheria za Tanzania, ambayo alidai imejiingiza kichwakichwa katika biashara huria, hazimzuii mtu yoyote kufungua akaunti yake nje ya nchi na kulimbikiza mapesa yake huko.
``Mimi nimeamua kuzungumza leo ili niwasaidie ndugu zangu watanzania, ni kweli si walaumu kutokana na hasira wanazoonyesha na ushabiki wa vyombo vya habari, lakini baada ya makelele yote haya, kitakachosubiriwa ni utaratibu ufuatwe, maandamano na hutuba hazitasaidia juu ya jambo hili,``alisema.
Bw. Ngula alisema hatua moja na muhimu ya kushughulikia suala hili, lazima anayemtuhumu Chenge ajitokeze.
Alisema watanzania wanapaswa waelewe kwamba hadi sasa Serikali yao inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, haijamtuhumu kwa lolote Bw. Chenge.
``Wanaomtuhumu Chenge ni watu wa Rada huko Uingereza, na gazeti la huko ndilo limeanika hizo tuhuma. Ieleweke kuwa tuhuma hizo zimeanza siku nyingi na serikali ya Tanzania ilikuwa ikifahamu, lakini haikusema lolote.Hii inamaanisha kwamba hawana matatizo naye,``alisema.
Bw. Ngula alisema hatua ya pili inayofuata, ni kuchunguza kwamba Waziri huyo amepataje kiasi hicho cha fedha.
Alisema kwa hali ilivyo sasa inaonekana kwamba serikali inasubiri uchunguzi unaofanywa na waingereza pekee na kushangaa kwanini inashindwa kumchunguza mtu wake, hadi wazungu waseme.
Alisema kutokana na jambo hilo kuwa la kimataifa, basi likiisha kwa sheria na taratibu za kimataifa watu wasilalamike.
``Mimi kwa uzoefu wangu hili jambo linavyoshughulikiwa, moja kwa moja naona huko tuendako Chenge ataibuka mshindi katika sakata hili kwa vile hatupo makini..Hata kama hizi fedha ni za watanzania, basi kwa mtindo huu watazikosa watakosa Mwana na Maji moto``alisema Bw. Ngula.
``Kuna watu hawaelewi mambo wanadhani kuwa na pesa nje ya nchi ni kosa, kuwekeza pesa kwenye mabenki ni biashara nzuri ili kupata faida tofauti na angeziweka hapa nchini.
Hoja iwe amezipataje na kamwe sio kwanini ni nyingi au kwanini zimewekwa nje,``alisema.
|